TCRA yatoa onyo kali maudhui ya kufikirika kuhusu imani za kidini

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa onyo kwa vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikisambaza taarifa fupi zilizo kwenye mfumo wa “video clips” zinazozungumzia masuala yanayohusu mawazo fikirika yanayogusa imani za kidini.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Machi 21, 2023 na Mkurugenzi Mkuu,Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dkt.Jabir Kuwe Bakari.

"Siku za hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa taarifa fupi zilizo kwenye mfumo wa “video clips” zinazozungumzia masuala yanayohusu mawazo fikirika yanayogusa imani za kidini.

"Mawazo hayo yamekuwa yakitolewa kwenye vyombo mbalimbali vya utangazaji ikiwa ni pamoja na Redio na Televisheni (traditional media), Vyombo vya Utangazaji Mitandaoni (Online TV & Radio) na kwenye makundi ya mitandao ya kijamii.

"Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inapenda kuchukua nafasi hii kutoa ufafanuzi kwamba masuala kama hayo yanayohusu imani za dini ni masuala binafsi ya mtu na hivyo mahali sahihi ni kwenye nyumba za ibada na sio kwenye Vyombo vya Habari na Utangazaji.

"Vyombo vya Habari na Utangazaji vina wajibu wa kufuata misingi na maadili ya taaluma zao kwa kutoa taarifa zilizofanyiwa uchambuzi, za kuaminika na za kweli. Hii ni pamoja na kutoa taarifa kwa kufuata Sheria, Kanuni, miongozo na maadili katika kutoa Huduma ya Utangazaji nchini.

"Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Utangazaji wa Redio na Televisheni), 2018 na Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta Maudhui ya Utangazaji Mtandaoni), 2022 zimeelekeza watoa huduma ya utangazaji kujiepusha na maudhui ya upotoshaji na yanayogusa Imani za watu.

"Hivyo basi, taarifa zozote zinazotolewa kwa umma kupitia vyombo vya Utangazaji ziwe za ukweli, uhakika na zitoke katika vyanzo vinavyoaminika ili kuepusha upotoshaji kwa jamii.

"Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inakemea vikali hali hii ya taarifa za mawazo ya kufikirika,na yenye utata kuhusu imani za kidini ambazo zinaendelea kushamiri kwenye vyombo vya utangazaji vya mitandaoni na vile vya redio na runinga za kawaida (traditional media) na inaagiza kuacha mara moja kurusha maudhui ye yote ya kufikirika ambayo yanaleta utata kuhusu imani za kidini kwenye jamii.

"Aidha, TCRA itachukua hatua kali za kisheria kwa chombo chochote cha utangazaji ambacho kitabainika kuendelea kurusha taarifa zenye maudhui kama hiyo,"amefafanua Dkt.Jabir kupitia taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Safi sana, maana siku hizi kila mtu mchambuzi.....ingepigwa marufuku na mihadhara

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news