Waziri wa Afya ataja ugonjwa ulioua watu watano mkoani Kagera

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema, uchunguzi wa Serikali kupitia Maabara ya Taifa umethibitisha uwepo wa Virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa wa Marburg Virus Disease (MVD) mkoani Kagera.

Mheshimiwa Ummy ameyabainisha hayo leo Machi 21, 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu ugonjwa huo ambao hivi karibuni ulisababisha vifo na wagonjwa wengine kulazwa.

"Uchunguzi ambao tumeufanya katika Maabara yetu ya Taifa ya Afya ya Jamii umethibitisha uwepo wa virusi vya Marburg ambavyo vinasababisha ugonjwa unaojulikana kama Marburg Virus Disease(MVD).

“Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO), ugonjwa huu wa Marburg uligundulika kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1967 katika Mji wa Marburg na ndio asili ya jina la ugonjwa huu, ugonjwa huu ulishawahi kuripotiwa katika nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya.
 
Zinazohusiana
“Ugonjwa huu huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hususani kwa njia ya kugusa majimaji ambayo yanaweza kuwa mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi yatokayo kwenye maiti au mgonjwa mwenye dalili, maambukizi pia yanaweza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula au kugusa mizoga au wanyama walioambukizwa,”amefafanua Mheshimiwa Waziri Ummy.

Amesema, ugonjwa huo umegundulika katika kata za Maruku na Kanyangereko zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo hadi sasa jumla ya kesi nane zimeripotiwa, kati yao watano pekee ndio wamefariki.

Mheshimiwa Waziri amesema, mpaka sasa ugonjwa huo hauna tiba mahususi isipokuwa hutibiwa kulingana na dalili.

Hali ilivyo

Hivi karibuni,Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Jamhuri ya Guinea ya Ikweta, Mheshimiwa Diosdado Vicente Nsue Milang alitangaza vifo vya watu tisa ambao walifariki kutokana na ugonjwa wa virusi vya Marburg katika Jimbo la Kie-Ntem.

Pia Serikali ilitangaza kuwa inachunguza visa vinavyoshukiwa vya homa ya kuvuja damu. Ni watu watatu pekee waliokuwa na dalili ndogo za ugonjwa huo ambao waliwekwa karantini kwa wakati huo katika hospitali katika eneo hilo lenye wakazi wachache na vijijini, linalopakana na Gabon na Cameroon.

"Watu watatu waliolazwa hospitalini wana dalili ndogo na wanaendelea kupata matiabu. Equatorial Guinea inatangaza tahadhari ya afya ya homa ya kuvuja damu ya virusi vya Marburg katika jimbo la Kie-Ntem na katika wilaya ya Mongomo,"alieleza Waziri huyo wa Afya.

Aidha, alisema mpango wa kukinga umewekwa kwa ushirikiano wa karibu na Shirika la Afya Duniani la Umoja wa Mataifa (WHO) kukabiliana na janga hilo katika eneo hili lililofunikwa na msitu mnene wa Ikweta Mashariki mwa nchi hii ambayo pia inajumuisha visiwa vikuu viwili.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na kikohozi, maumivu ya viungo, kuhara na kutapika, na mara nyingi hata upungufu wa damu katika mwili.

Marburg ni nini?

Mlipuko huo ulitokana na tumbili wa Kiafrika walioagizwa kutoka Uganda. Lakini virusi hivyo vimehusishwa na wanyama wengine tangu wakati huo.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, virusi vya Marburg, ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 31 kuambukizwa, saba kati yao walikufa, mnamo 1967 huko Marburg na Frankfurt, Ujerumani na Belgrade huko Serbia.

Na miongoni mwa wanadamu, huenezwa zaidi na watu ambao wamekaa kwa muda mrefu katika mapango na migodi yenye popo.

Inaeneaje?

Popo wa matunda aina ya rousette wa Misri mara nyingi huwa na virusi. Nyani wa kijani kibichi na nguruwe wanaweza pia kubeba.

Miongoni mwa wanadamu, huenea kupitia maji ya mwili na malazi yaliyochafuliwa nao.Na hata watu wakipona, damu au shahawa zao, kwa mfano, zinaweza kuwaambukiza wengine kwa miezi mingi baadaye.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news