Vikao vya Kamati za Kudumu za Bunge kuanza Machi 11 hadi 31

NA DIRAMAKINI

VIKAO vya Kamati za Kudumu za Bunge vinatarajiwa kuanzia Jumamosi ya Machi 11 hadi 31,2023 jijini Dodoma.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma.

Vikao hivyo vinatangulia kabla ya Mkutano wa 11 wa Bunge ambao utaanza Aprili 4, mwaka huu ukiwa ni mahususi kwa ajili ya Bajeti ya Serikali.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo shughuli zitakazotekelezwa na kamati katika kipindi hicho ni Kamati ya Bajeti pamoja na mambo mengine itachambua mapendekezo ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2023/ 2024.

Pia, kamati 11 za kisekta zitatembelea na kukagua utekelezaji wa miradi iliyotengewa fedha kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itafanya ziara za kufuatilia utekelezaji wa miradi ya uwekezaji wa mitaji ya umma,

Wakati huo huo, taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) itafanya ziara ya kutembelea na kukagua thamani ya fedha za umma zilizotumika katika miradi ya Serikali Kuui, mashirika na taasisi za umma.

Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itafanya ziara za kufuatilia thamani ya fedha za umma zilizotumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya mamlaka za Serikali za mitaa.

Vile vile, taarifa hiyo imefafanua kuwa, Kamati ya Sheria Ndogo itapokea maelezo ya ufafanuzi pamoja na kufanya uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa bungeni wakati wa Mkutano wa 10 wa Bunge.

"Kamati hii itapata mafunzo kuhusu uchambuzi wa Miswada ya Sheria na Sheria Ndogo. Aidha, kamati itapokea taarifa kutoka serikalini kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge yanayotokana na taarifa za shughuli za kamati kwa mwaka 2022/2023,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Machi 13, 2023 kutakuwa na Mkutano wa Wabunge wote kwa ajili ya kupokea mapendekezo ya Serikali ya Mpango na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka kwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news