WATU WASHIKE ADABU: Museveni amejibu, tuwakatae kwa mambo ya aibu

NA LWAGA MWAMBANDE

SERIKALI ya Jamhuri ya Uganda chini ya Rais Yoweri Kaguta Museveni inatayarishwa mswada kwa lengo la kuharamisha kabisa mapenzi ya jinsia moja, ukiwa na adhabu ya hadi miaka 10 gerezani na faini ya hadi shilingi milioni 10 za Uganda.

Kwa mujibu wa VOA, mswada huo unawalenga watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja, wamiliki wa nyumba na hoteli, wamiliki wa vyumba vya burudani, mashirika yanaoyoeneza ushoga, waandishi wa habari, watengenezaji filamu miongoni mwa wengine.

Aidha,Uganda inajaribu kutunga sheria kali dhidi ya ushoga, mara hii mswada unalenga kila mtu anayechangia kwa namna yoyote kueneza mapenzi ya jinsia moja nchini humo.

Mbunge wa Manispaa ya Bugiri huko Mashariki mwa Uganda, Mheshimiwa Asuman Basalirwa ambaye ameandaa mswada huo, ameambia VOA kwamba mswada wake unalenga kuweka mazingira magumu kabisa kwa ushoga kufanyika Uganda.

Pia unawalenga wafadhini wa ushoga, wanaoeneza, wamiliki wa hoteli, vyumba vya burudani na wenye nyumba za kawaida za kukodisha.

Sambamba na wanaoneza ushoga kwa kuchapisha vitabu, na wafadhili, watatozwa faini ya shilingi milioni 100 za Uganda.

Na wanaomiliki vyumba vya kufanyia ushoga watahukumiwa miaka saba gerezani huku wamiliki wa nyumba watakaokodisha kwa watu walio katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja watahukumiwa mwaka mmoja gerezani.

Mtu yeyote atakayejaribu kushawishi mwingine kufanya mapenzi ya jinsia moja atafungwa miaka mitano gerezani na atakayepatikana na makosa ya kusimamia au kubariki ndoa hizo atafungwa miaka 10 gerezani.

Katika hatua nyingine, waandishi wa habari, wahariri, watengenezaji filamu watakaofichua waathiriwa wa ushoga bila idhini yao watatozwa faini ya shilingi milioni tano za Uganda.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Uganda kukabiliana na vitendo hivyo vichafu, ambavyo vinakwenda kinyume na tamaduni, maadili na mila za Waafrika zinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja kwa sababu huo ni zaidi ya ushetani. Endelea;

1.Ya kale kweli dhahabu,
Watu washike adabu,
Wasilete ya aibu,
Kama wapo wawe bubu.

2.Misaada si sababu,
Maovu yawe karibu,
Kama tabu iwe tabu,
Kwetu wabakie bubu.

3.Amekwishasema babu,
Na wala hajaharibu,
Anafwata ya vitabu,
Kwetu wabakie bubu.

4.Wenyewe waliharibu,
Wakavileta vitabu,
Twashika bila aibu,
Kwetu wabakie bubu.

5.Yale yanayowasibu,
Nchi wabaki wababu,
Sababu wajiharibu,
Kwetu wabakie bubu.

6.Msimamo unatibu,
Na Mungu wamjaribu,
Hakuna la kutusibu,
Kwetu wabakie bubu.

7.Wamalizana aibu,
Wanabebana aibu,
Kwao wazidi haribu,
Kwetu wabakie bubu.

8.Museveni kawajibu,
Wache wabaki na gubu,
Hakuna kutughilibu,
Kwetu wabakie bubu.

9.Qatari walijaribu,
Waende wakaharibu,
Vizuri waliwajibu,
Kwetu wabakie bubu.

10.Mpira siyo sababu,
Ya Mungu tukaharibu,
Donda kubwa walitibu,
Kwetu wabakie bubu.

11.Misaada ya aibu,
Hiyo tusiijaribu,
Mungu wetu yu karibu,
Kwetu wabakie bubu.

12.Hakuna yote sababu,
Uumbaji tuharibu,
Maagizo tusijibu,
Kwetu wabakie bubu.

13.Mungu alivyoratibu,
Adamu limjaribu,
Viumbe wote na dubu,
Hakuwepo wa karibu.

14.Hakutaka kuharibu,
Upweke umghilibu,
Uzuri alimtibu,
Kumleta wa karibu,

15.Hawa ni bibi si babu,
Wawili kuwa karibu,
Agizo wakalijibu,
Ongezeko wakatibu.

16.Jaza dunia jaribu,
Na huo wenu ububu,
Watabakia mababu,
Upweke utawasibu.

17.Kwenu mmeshaharibu,
Mnafanya ya taabu,
Tamaa mnazitibu,
Kumfwata mjaribu.

18.Yeye azidi haribu,
Awe na watu karibu,
Yale yatayomsibu,
Ajaze chake kitabu.

19.Amka msiwe bubu,
Ugonjwa wenu utibu,
Na kwa Mungu mkatubu,
Asijekuwaharibu.

20.Museveni amejibu,
Tunapenda lake jibu,
Na wengine taratibu,
Ee Mungu uwaratibu.

21.Tamaa zisiwasibu,
Wakaogopa kujibu,
Mabaya yakatusibu,
Dunia ukaharibu.

22.Sababu ya walojibu,
Mungu usituharibu,
Wala tusipate tabu,
Na maisha ya ajabu.

23.Mungu wagonjwa watibu,
Wasizidi jiharibu,
Wala kusiwe sababu,
Kuendekeza aibu.

24.Wale wamewaghilibu,
Na ushoga kuwasibu,
Waponye hiyo aibu,
Watoto wako twatubu.

25.Dunia usiharibu,
Tunaomba tunatubu,
Maombi yetu yajibu,
Tusizidi jiharibu.

26.Mungu wewe unatibu,
Wasamehe tukitubu,
Uwezo wako ajabu,
Tunaomba utujibu.

(Warumi 1:17-32, Mathayo 19:4-6)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news