Askofu amuombea msamaha Cyprian Musiba kwa Mheshimiwa Membe kuhusu fidia ya mabilioni ya fedha

Mpendwa Mheshimiwa Bernard Membe!

Ninakusalimu katika Jina la Bwana wetu Yesu Kristo! Ninaandika waraka huu kwako muda huu usiku ikiwa bado dakika chache kuingia Dominika ya Kwanza baada ya Pasaka!

Miezi michache iliyopita nilikutafuta sana na kijana wako akiuona waraka huu atakuwa shahidi kuwa nilitaka tuongee ana kwa ana. Kwa kuwa jambo hili ni la kuponya nchi nilisukumwa liwe hadharani ili nguvu ya uponyaji ilete ishara kwa taifa ambalo tunataka liingie katika maridhiano.

Imani yangu kwako haijaanza mwaka 2020, ingawa kipindi hicho ndicho kilichotuweka karibu zaidi.

Imani yangu kwako pia haitokani na matukio yako ya kisiasa ya mwaka 2020 ingawa hayo yalisaidia kutuweka karibu.

Imani yangu kwako ilianza zaidi ya miaka 14 iliyopita mwaka 2009. 

Wakati huo, nilipokuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kujisomea Biblia (Scripture Union of Tanzania) nilimtuma katika mikoa ya Lindi na Mtwara kijana aliyeitwa Laban Boaz Nzaganya kusambaza vitabu vya Wasomaji wa Biblia.

Alifikia katika Cathedral ya Kanisa Kuu la Anglikana Dayosisi ya Masasi ni kwa sababu tulifahamiana na Mhashamu Baba Askofu Patrick Mwachiko wakati wa mchakato wa Kanisa Anglikana lilipoomba kurudishiwa Hospitali ya Mkomaindo ambapo vikao kati ya Serikali na Kanisa vilifanyikia Scripture Union.

Katika taarifa yake, Laban alitueleza alifika hata katika Ofisi yako ya Mbunge na alipoonana na wewe ulionyesha kumtia moyo. Tangu wakati huo tulianza kukuombea kama huduma yetu na mimi binafsi niliendelea kukuombea pia.

Mheshimiwa Membe! Wewe ulikwishabarikiwa na Mungu na ili kuthibitisha hayo rejea matukio mazito ambayo nusura upoteze uhai wako ila Mungu alikulinda.

Haukulindwa kwa sababu ya ujuzi wako katika masuala ya mbinu na medani kwani ingelikuwa hivyo, basi Jenerali Kombe angeendelea kuishi.

Bali wewe ulilindwa kwa kuwa Mungu alikupa kibali na alitaka uendelee kuwepo kwa sababu ya kusudi maalum.

Mheshimiwa Membe! Mimi kama Askofu ninaandika waraka huu kwako ambao kwa hakika utakufikirisha wewe na pia utakunyima amani hadi pale utakapoweza kuchukua hatua ya ujasiri na imani ya kuishinda dhamira yako ambayo inataka kulipa kisasi. 

Wewe sio dhaifu kiasi hicho cha kuendelea kupambana na mtu ambaye hana sifa ya kuingia darasani kwako.

Mheshimiwa Membe! Nimesukumwa sana mimi kama Askofu asimamaye katika zamu yake ili kukuomba kuwa umsamehe Cyprian Musiba na usiendelee kushinikiza ili akulipe mabilioni ya shilingi kama fidia ya kukuchafua.

Cyprian Musiba hana fedha hizo na hata akiuza kijiji kizima hana fedha hizo. Mungu amekujalia wewe afya na mali na hivyo kumsamehe mtu ambaye hawezi kulipa fadhila ndio jambo la ibada ambalo unaweza kufanya.

Hii ni nafsi ya kipekee iliyokuja kwako nikiamini utakuwa na ujasiri wa imani ya kufanya jambo hili ukiwa na imani kuwa Roho Mtakatifu yupo katika hili.

Ki-Biblia, Cyprian Musiba ni askari aliyesalimu amri asiye na silaha na Wakristo tunakatazwa kutumia silaha nzito kwa ajili ya kupambana na mtu aliyesalimu amri asiyekuwa hata na silaha.

Mfalme Daudi alimkaripia Jenerali Jobu kwa kumuua Jenerali Abner wakati wa amani huku Abner akiwa sio tishio. Huyu Cyprian Musiba sio tishio tena kwako na kwa mtu yeyote yule.

Ni kwa sababu hiyo, ninakuomba mimi niliye Askofu uchukue hatua ya kumsamehe Musiba mbele ya kamera na kuutangazia ulimwengu kuwa wewe hauna haja ya kuendelea kumdai.

Ni imani yangu kuwa wanasheria watalitunza jambo hilo ili mazungumzo ya kimahakama yaweze kufanyika ili kuhitimisha jambo hilo.

Ninamuomba Mungu auangaze moyo wako ili kusudi uweze kuona mapenzi na dhamiri yake Mungu kupitia andiko hili kupitia kwa mtumishi aliye mdogo miongoni mwa watumishi wake.

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!


Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula

Askofu Mkuu Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki na Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Makanisa ya Moravian ya Uamsho Duniani (World Fellowship of Moravian Revival Churches - WFMRC).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news