Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wadhamiria mambo makubwa kwa ustawi bora wa elimu ya juu

NA DIRAMAKINI

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mh. Songoro Mnyonge, amelitaka baraza la Wafanyakazi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kujadilliana na kuja na mipango ya kuona ni namna gani taifa linajiandaa na kukabiliana na ongezeko la wanafunzi linatokana na ongezeko la idadi ya watu nchini.
Mheshimiwa Mnyonge, ametoa wito huo wakati akifungua mkutano wa Tisa wa Baraza la wafanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania lililofanyika Aprili 5, 2023, mkao makuu ya OUT Kinondoni jijini Dar Es Salaam.

“Idadi ya wanafunzi inaendelea kuongezeka kila uchao, ardhi itakwisha sababu idadi ya watu inaongezeka ila ardhi ni ile ile. Miundombinu ya kufundishia nayo itafika kipindi itaelemewa (itatuacha), lazima tutafute mbinu mbadala ya kufikisha elimu kwa raia wetu.Nayo si nyingine bali ni hii inayotolewa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,”amesema Mheshimiwa Mnyonge.
Ameendelea kusema kuwa, kwa mwaka huu wa 2023, Manispaa ya Kinondoni imefanikiwa kuwapeleka shule wanafunzi wote waliochaguliwa kidato cha kwanza kutokana na kujengwa madarasa mapya kupitia mpango wa fedha za UVIKO zilizotolewa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia Mkutano wa Baraza la tisa la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mh. Mnyonge amesema, mabaraza ya wafanyakazi ni takwa la kisheria ambayo pamoja na mambo mengine husaidia kuzuia migogoro mahali pa kazi. Pia, mabaraza hutoa fursa nzuri kwa wafanyakazi kuwa pamoja na kujadiliana kuhusu maswala mbalimbali yanayohusu utumishi wao na taasisi kwa ujumla.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Prof. Elifas Bisanda, akizungumzia ongezeko la wanafunzi, amesema tangu serikali ilipoanza mpango wa kutoa elimu bure, kumekuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ambapo uwezo wa vyuo vikuu nchini hautoweza kubeba wanafunzi hao katika kipindi kifupi kichacho.

“Mwaka huu wanafunzi watakaofanya mtihani wa darasa la saba kwa mujibu wa takwimu za udahili ni 1,387,448 na uwezo wa vyuo vikuu Tanzania kupokea wanafunzi kwa mujibu wa takwimu ni wastani wa 150,000, kwa hili wimbi linalokuja ni kubwa sana, kimbilio pekee litakaloweza kuwapokea wote hawa ni Chuo Kikuu Huria cha Tanzania,” amesema Prof. Bisanda.
Akifafanua zaidi, Prof. Bisanda amesema, ili kujiandaa kukabiliana na wimbi hilo la wingi wa wanafunzi linalotarajiwa ndani ya miaka michache ijayo, serikali ingeweza kukiingiza Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika mpango wa miaka mitano ili kukiimarisha na kukiwezesha kwa sababu ndiyo chuo pekee kinachoweza kupokea wanafunzi wengi kwa wakati mmoja hata kufikia zaidi ya milioni moja.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Maadili Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ndugu Ally Ngowo, amesema watumishi wanapaswa kuutumia muda wa kazi ipasavyo na kuepuka kuutumia muda huo kwa mambo mengine hususani kuperuzi mitandaoni kupitia simu zao.

Ndg. Ngowo, amewataka watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, kuleta tija kazini kwa kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza udhahili na kuongeza mapato ya chuo badala ya kupoteza muda mwingi kuchati mambo yasiyokuwa na tija muda wa kazi.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Utawala, Fedha na Mipango Prof. George Sylivanus Oreku amewataka watumishi wote wa OUT kufanya kazi zao kwa kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma.
"Nawakumbusha watumishi wote kuzingatia maadili katika utumishi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kinidhamu pale itakapobainika kuna maadili yamekiukwa. Uzingatiaji wa maadili ya utumishi ni msingi wa kutoa huduma bora, kukuza ufanisi na kuleta tija katika taasisi,"amesema Prof. Oreku.

Baraza la Watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, leo Aprili 5, 2023 limefanya mkutano wa Tisa na kufanikiwa kujadili mambo muhimu yahusuyo watumishi, bajeti ya chuo, mpango mkakati, masuala mtambuka na mwisho kuushauri uongozi wa Chuo katika masuala mbalimbali ya kukuza na kuendeleza OUT.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news