Faida za ujenzi wa barabara za Outer Ring Road Dodoma zatajwa

NA MWANDISHI WETU

MRADI wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami wa njia nne ya mzunguko (Outer Ring Road) nje ya jiji la Dodoma itakayokuwa na urefu wa kilomita 112.3 unatajwa kuwa na manufaa makubwa ikiwemo katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Dodoma na uchumi wa nchi kwa ujumla.
Faida nyingine za utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katikati ya jiji la Dodoma ambapo magari makubwa ambayo yanakwenda nje ya Dodoma hayatapita mjini bali yatapita katika barabara hiyo huku ajira zaidi ya elfu mmoja zikizalishwa kupitia mradi huo.

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Leonard Chimagu wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa mbele ya waandisha wa habari ambapo amesema mradi huo umegawanywa sehemu mbili na kutekelezwa na wakandarasi wawili tofauti.

Mhandisi Chimagu ameendelea kwa kusema kuwa, kipande cha kwanza kitahusisha ujenzi wa kuanzia Nala-Veyula-Barabara ya Arusha-Mtumba-Ihumwa (bandari kavu) ikiwa na urefu wa kilometa 52.3 ambapo mkandarasi kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na kugharamu kiasi cha shilingi bilioni 100.84.

Ameongeza kuwa ujenzi wa kipande cha pili cha barabara hiyo unaanzia Ihumwa (bandari kavu)-Matumbulu-Nala itakayokuwa na urefu wa kilometa 60 ambao mkandarasi wa kampuni ya AVIC International na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 120.86.

“Hadi kufika sasa mkandarasi amekamilisha kazi kwa asilimia 18.4, mradi huu umekuja na miradi mingine ya kijamii ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya ambapo vitajengwa vituo vya afya vinne vikiwa na gari ya kubebea wagonjwa (ambulance) pamoja na uchimbaji wa visima vinne”, alisema Mhandisi Chimagu.

Akiongelea miradi mingine inayoendelea kutekelezwa jijini humo ni pamoja na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zinazoendelea wilayani Mpwapwa zikiwa na urefu wa zaidi ya kilometa 50 na pia barabara kwa kiwango cha lami ya urefu wa kilometa 23 itakayojengwa kuelekea hospitali ya Mvumi.

Vilevile Mhandisi Chimagu amesema, ndani ya Mkoa wa Dodoma kuna mradi unasanifiwa ambao utahusisha ujenzi wa barabara za lami katikati ya jiji la Dodoma zikiwa na urefu wa kilometa 43.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, Wahandisi Washauri katika mradi huo kutoka kampuni za Inter consultant and Pace na CTC Crown Tech Mhandisi Issa Mjema na Mhandisi Lusekelo Kijalo wamesema watasimamia kazi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kabla ya muda uliopangwa ambao ni mwezi Machi, mwaka 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news