Nabii Dkt.Mjuni asisitiza umuhimu wa Wakristo kuyatuza mazingira Tanzania

NA DIRAMAKINI

MTUMISHI wa Mungu wa Huduma ya Yerusalemu Pomerini Ministry iliyopo mkoani Iringa, Nabii Dkt.Mjuni Kisha amesema, Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla wanalo jukumu kubwa la kuhakikisha wanayatunza mazingira kwa ustawi bora wa vizazi vya sasa na vijavyo.
Dkt.Mjuni licha ya kuwa mstari wa mbele kuwahudumia Watanzania kupitia neno la Mungu na maombezi, pia anashiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za maendeleo huko vijijini ikiwemo kuwawezesha mahitaji wanaoishi mazingira magumu na kutoa elimu ya utunzaji mazingira.

"Sisi kama Wakristo, ikiwa tunataka kuwa watiifu kwa Mungu na kutazama uumbaji wake, hatupaswi kupuuzia kile kinachotokea katika mazingira, hatari iwe inatokana na uchafuzi wa mazingira, mabadiliko ya tabia nchi, uvuvi wa kupita kiasi,uwindaji haramu (ujangili) au sababu nyingine yoyote tunapaswa kusimama imara kuyalinda mazingira,"amesema.

Nabii Dkt.Mjuni amesema, Wakristo wote wanapaswa kuhimizana na kuhimizwa kutunza ipasavyo maeneo yao au bustani zao na kushiriki katika ulinzi wa vyanzo vya maji ikiwemo malisho.

"Wakristo pia wanapaswa kuunga mkono sera na sheria za Kitaifa na Kimataifa ili kudhibiti utunzaji wa mazingira na matumizi ya maliasili, tunapaswa kufanya kazi pamoja, kama alivyofanya mwanamazingira Prof.Wangari ambaye alitunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa sababu ya kazi yake ya kuhifadhi mazingira ya Afrika,"amefafanua Nabii Dkt.Mjuni.
 
Maathai ni nani?

Mwanamazingira, Hayati Prof. Wangarĩ Muta Maathai (1940-2011) kutoka nchini Kenya ni miongoni mwa wana mazingira wakati wa uhai wake waliofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuanzisha vuguvugu la ukanda wa kijani ambalo lilileta matokeo chanya ndani na nje ya Afrika.

Wakati wa uhai wake, Prof.Maathai alianzisha wazo la kuziwezesha jamii kujisimamia katika kupanda miti kwa wingi kuanzia ngazi za chini hadi juu.

Aidha, wazo hilo alilipanua kwa kuanzisha jumuiya aliyolipa jina la Vuguvugu la Ukanda wa Kijani (GBM). Vuguvugu hilo lilianzishwa mwaka 1977, chini ya usaidizi wa Kamati ya Taifa ya Wanawake wa Kenya (NCWK).
 
Hatua hiyo ilikuwa ni njia ya kupambana na mahitaji ya nishati na maji ya wanawake wa vijijini nchini Kenya. Kadri miaka ilivyosonga mbele, jumuiya ya Maathai ya GBM ilifanikiwa kupanda miti milioni 51 nchini Kenya.

Vuguvugu hilo lililofanya kazi katika ngazi ya vitongoji, kitaifa na kimataifa, linalenga kujenga uwezo wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuwawezesha wanawake.
 
Faida

Katika hatua nyingine, Nabii Dkt.Mjuni amefafanua kuwa, kuna faida nyingi za kuyatunza mazingira ambayo ni mambo yote yanayoathiri ukuaji au uwepo wa viumbe hai,mfano hewa,maji na ardhi.

"Mazingira ni kitu muhimu sana katika ustawi wa viumbe hai wowote,katika Taifa letu la Tanzania na Dunia hii tuliyomo.Mazingira ni muhimu kwa ukuwaji ya mimea mbalimbali,viumbe wa baharini,viumbe walioko chini ya ardhi,na viumbe walioko juu ya uso wa dunia, hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunayatunza mazingira ili yaweze kututunza kwa ustawi bora wa vizazi vya sasa na vijavyo,"amefafanua.

Pia amesema, sera mbalimbali za uifadhi wa mazingira na viumbe vyake zimewekwa kwa lengo moja kubwa hususani kutunza mazingira, lakini pili kulinda aina ya viumbe waliomo.

Serikali inasemaje?

Februari 12, 2022 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Isdor Mpango alizindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, uzinduzi uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Siku hiyo, Makamu wa Rais alisema, kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, upandaji miti, kupendezesha miji, kufanya kusafi katika maeneo yote ya makazi na biashara, viwandani na masokoni ni lazima kuanzia sasa kuwa kazi za kudumu.

Aidha, alisema viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wanapaswa kusimamia uhifadhi wa mazingira na suala hilo litakua kipimo cha utekelezaji wa majukumu yao.

Makamu wa Rais alisema, ni muhimu kuondoa nadharia katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwa na mipango isiyotekelezwa bali inahitajika kazi ya ziada itakayotoa matokeo chanya katika kuhifadhi mazingira.

Alisema, sheria ndogondogo za uhifadhi wa mazingira zinapaswa kusimamiwa ikiwemo faini na ikiwezekana kuongeza faini hizo ili kukomesha waharibifu wa mazingira.

Dkt.Mpango alisema, zoezi la kutunza mazingira lazima kuwa shirikishi kwa wadau wote kuanzia mijini na vijijini na kuagiza wizara na taasisi zote za serikali kuhakikisha wanapanda miti na kuitunza katika maeneo yao.

Aliwataka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kutoa elimu kwa wananchi juu ya aina ya miti inayopaswa kupandwa kulingana na maeneo wanayoishi.

Pia, aliwaasa kuhakikisha wanaongeza miche itakayopandwa ikiwemo kuongeza vitalu katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate urahisi wa kupata miche hiyo.

Vile vile, Makamu wa Rais alitoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini kuzingatia misingi ya uzalishaji endelevu pamoja na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira ili kupambana na uchafuzi wa mazingira.

Makamu wa Rais aliagiza Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanashirikiana kushughulikia suala la uharibifu wa mazingira unaofanywa kwenye chanzo cha mto Ruaha katika Bonde la Ihefu kutokana na kuingizwa kwa makundi makubwa ya mifugo pamoja na kuelekezwa maji katika mashamba makubwa bila kurejeshwa mtoni.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo alisema Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 imezingatia masuala mbalimbali ikiwemo mpango wa taifa wa miaka mitano, mpango endelevu, pamoja na mpango wa miaka 15 ulioanza 2011-2012.

Dkt.Jafo alisema, sera hiyo inatarajiwa kuokoa uharibifu wa mazingira katika nchi pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.

Alisema, tayari wizara imefanya zoezi la utoaji elimu ya uhifadhi wa mazingira na kuongeza kuwa, wanatarajia kupanda miti milioni 14.5 nchi nzima kwa kuwashirikisha wanafunzi nchini kote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

4 Comments

  1. HONGERA SANA DOKTA MJUNI KWA UJUMBE HUU, TANZANIA INAHITAJI WATUMISHI WA MUNGU KAMA WEWE ILI KUTOA ELIMU NA HAMASA NJEMA NAMNA HII.KUMBUKA MAZINGIRA BORA YANATUPA MUSTAKABALI MWEMA WA AFYA ZETU.MUNGU WA MBINGUNI AKUZIDISHO HEKIMA

    ReplyDelete
  2. Ujumbe mzuri man of God, songa mbele

    ReplyDelete
  3. Haya ndiyo mambo sasa, unahubiri na kutoa elimu, good job

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news