WANAOISHI KWENYE HIFADHI YA MSITU WA IPEMBAMPAZI SIKONGE KUPATIWA ARDHI ENEO LINGINE

NA MWANDISHI WETU

SERIKALI imesema kuwa wananchi wa Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora wanaoishi kwenye Hifadhi ya Msitu ya Ipembampazi watapatiwa ardhi kwenye maeneo mengine yaliyotengwa kwa ajili ya kilimo kama vile Scheme ya Ulyanyama, Igigwa na Scheme mpya ya umwagiliaji ya Kalupale.

Hayo yamesemwa leo Aprili 14,2023 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Sikonge, Mhe. Joseph George Kakunda aliyetaka kujua lini Serikali itatekeleza ahadi ya kuwapatia Wananchi wa Sikonge eneo la hekta 33,000 kwenye Mbuga ya Ipembampazi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mhe. Masanya amefafanua kuwa Serikali inatambua mapendekezo yaliyotolewa na Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Sikonge kutaka sehemu ya eneo la msitu huo ligawanywe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji lakini Serikali bado inaona umuhimu wa Msitu wa Ipembampazi kuendelea kuhifadhiwa kutokana na faida za kiikolojia, kijamii na kiuchumi.

“Hifadhi ya Msitu wa Ipembampazi ina umuhimu katika kuimarisha mfumo ikolojia wa Ugalla - Moyowosi unaojumuisha maeneo ya hifadhi yaliyopo katika Mikoa ya Tabora na Kigoma ambapo eneo la msitu huo linatumika kama mtawanyiko na mapito ya wanyamapori hususan tembo na pia eneo hilo lina wanyamapori wa aina mbalimbali na limetengwa kuwa kitalu cha uwindaji wa wenyeji,” Mhe. Masanja amesisitiza.

Wilaya ya Sikonge ina misitu mbalimbali ikiwemo Hifadhi ya Msitu wa Ipembampazi wenye ukubwa wa hekta 133,000 ambao upo chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news