Prof.Muhongo aelezea umuhimu wa Sekta ya Madini nchini

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof. Sospeter Muhongo ameelezea umuhimu wa Sekta ya Madini katika kuongeza mchango wake kwenye ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Prof. Muhongo ameelezea umuhimu wa sekta hiyo Aprili 28,2023 wakati akitoa mchango wake bungeni jijini Dodoma ambapo pia amesema suala la umakini kwenye madini mapya tunayoanza kuchimba aina ya (PGM) na (REE.) ni muhimu likazingatiwa.

Mbali na hilo, pia Prof. Muhongo amebainisha kwamba Serikali iwe na migodi inayoimiliki yenyewe kwa asilimia 100 bila ubia ili sekta ya madini iwe na tija na iwezeshe kuinua na kuleta mabadiliko chanya katika maendeleo.

"Ni matumaini kwamba wizara inaenda kubadilika, ukweli ni kwamba ukisikiliza fedha unaelezwa mabilioni kama huna uzoefu na hii sekta utaona ni fedha nyingi sana. Lakini niwaeleze ukweli ni kwamba sekta ya madini haijachangia ipasavyo.

"Na sababu ni hizi, sekta ya madini ingechangia ipasavyo ukuaji wetu wa uchumi unaopaswa kuondoa umaskini lazima ukue kwa asilimia 8 mpaka 10, ukiwa chini ya hapo hata ukifanyaje hautatoa umaskini. Umaskini wetu lazima upungue utoke asilimia ishirini mpaka 15 na inayoweza kutupeleka huko ni sekta ya madini gesi na vingine.

"Sasa toka mwaka 1961 miaka 60 iliyofuata hadi 2021 ukitaka kukubaliana na ninayosema ni kwamba, Tume ya Madini muda mwingi imejishughulisha na utawala wa sekta ya madini Administration of the Mineral Sector na ndio maana madini yanayochimbwa ni hayo hayo.

"Yaani dhahabu, almasi na vito hasa Tanzanite na ndio maana ya Liganga na Mchuchuma nitayaongea siku nyingine. Wasingeshughulika na mambo ya utawala sana chuma ya liganga toka miaka ya 1960 tungeshachimba.

"Uchumi wa Dunia ya leo msemaji mmoja ameongea vizuri sana, sijui kama mmemuelewa Prof. Mkumbo ameongea vizuri sana uchumi wa leo wa Dunia haijalishi wewe ni m-socialist kwanza ni vitu vimepitwa na wakati haujadiliwi.

"Sasa hivi uchumi wa Dunia ya sasa unaongoza ni wa aina mbili, Private Wealth Capitalism ya ubinafsi ambayo ni ya nchi za Magharibi na uchumi mwingine umekuja kuibuka kwa nguvu sana ni State Capitalism na hii inafanywa China, imefanikiwa India, Brazil Norway...

"Sekta hii ya madini ni lazima itupeleke huko ni lazima iwepo migodi inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 la sivyo hatutatoka. Mtakuwa mnadhani hizo bilioni ni hela nyingi, lakini ni ndogo sana, Sasa kuanzia 2023 kuendelea ndio maana nimesema naunga mkono nadhani tutakuja na hybrid tuchanganye hizi kampuni binafsi, lakini hizi za serikali lazima ziwepo."

ATOA USHAURI

"Sasa inamaanisha kwamba, sekta ya madini kuanzia sasa ijihusishe na uwekezaji na kufanya haya tunahitaji taasisi mbili muhimu sana ya kwanza ni Geological Survey ni ajabu kwamba Tume ya Madini inapewa umuhimu bado ni makosa yale yale ya kushughulika na utawala wa madini badala ya kukuza Geological Survey.

"Sasa Geological Survey ni lazima tuwekeze ndio utatueleza tuna madini ya aina gani, kiasi gani tunataka kuendelea na utawala wa madini, lakini Geological Survey haijawekezwa.

"Vile vile Wizara ya Madini sio lazima ione kwamba hii ni Wizara ya Elimu, huko zamani tulipokuwa chuo kikuu sisi tulikuwa tunafanya kazi na Geological Survey.Kwa sababu ukitaka wataalam wengi wako UDOM, UDSM, maabara zile lazima ziwezeshwe."


MADINI MAPYA

"Haya madini mapya tunayoyaingia haya ninavyoelewa mimi hatuna maabara zinazoweza kutusaidia hapa nchini. Kwa hiyo mtaendelea kupokea ripoti kutoka nje ambazo nyie hamuwezi kuthibitisha, Sasa kuna mapungufu makubwa sana, lakini mtu anaweza kushangilia akaifurahia hii mpya ninayosema tunapata hisa asilimia 16.

"Waheshimiwa Wabunge na Watanzania hili ni kosa kubwa tunalolifanya asilimia 16 hiyo tunaweza tusipate kitu kwa sababu moja hatuko kwenye bodi inayofanya maamuzi...kwenye Management ya juu haupo haujui unazalisha kiasi gani, haujui unauza kiasi gani wewe unakaa pembeni unasubiri tu uletewe fedha asilimia 16.

"Maana ya kuwa mwana hisa ni kwamba lazima ushirikiane na mwenzako kuwekeza kwenye hasara, na kwenye faida sasa cha kujifunza Watanzania ninaomba hili wizara iende pale Mwadui ichukue ripoti ya mgodi iliyofanywa na marehemu Kassam alikuwa anafanya kazi nchi za nje akaomba nafasi akapata cheo UN (Umoja wa Mataifa)."

"Lakini, Mwalimu Nyerere akamrudisha mwaka 1969 akampeleka pale Mwadui musomi mzuri tu wa Uingereza akamwambia tunataka kutaifisha hebu angalia Mwadui inavyokwenda. Alitoa ripoti ambayo kwa ufupi nasema hawaelewi nini kilikuwa kinaendelea pale Mwadui, watu hawaelewi.

"Kwa hiyo Mwadui tulianza na shares 50 kwa 50... tumekwenda wakasema wajenge plant mpya nzuri ya kisasa Tanzania mwenzetu changia hela sisi hatuna tutaelewana huko huko wewe leta tu plant wakaleta plant share zetu zikashuka kutoka 50 zikabaki 25 sijui Mwadui kama bado tunashare.

"Kwa hiyo, hii asilimia 16 ndugu zangu waheshimiwa nawaambia ni kosa ambalo lazima tulirekebishe sababu hatuna control huenda hata tusipitate kitu au tukapata inakuwa kidogo sana.

"Kingine ambacho Wizara inahitaji umakini mkubwa ni madini mapya na leseni wanazotoa nitawatolea mfano hapa leseni zimeshatolewa za (PGM) Platinum Group Metals je, tunajua huko wanaenda kuchimba nini?.

"Maana yake (PGM) hii group ina madini kama saba...mengine ya thamani sana, unakuta kwenye Layer Earth Element wanasema madini ya mkakati kwako au upande wa wawekezaji? Sasa hii kama mtu haelewi anaweza kuwa anaongea tu kwa mzaha mzaha.

"Ni madini element 17 ziko kwenye hii group na zote za thamani. Ndio hayo Marekani ya kimkakati, Ujerumani na Japan sasa katika haya madini yapo matatu makubwa kabisa Latetium, Lanthanum na Scandium nichukue moja Latetium inatumika kwenye X- ray hata treatment ya Cancer ukiwa na haya madini ambayo yanaitwa '177 P S M A' kozi kozi moja ni dola 10,000 na treatment inatakiwa kozi tatu mpaka nne.

"Haya madini ukitaka kuyanunua unaweza ukaingia kwenye mabilioni ya dola. Je, leseni tunazozitoa za Earth Layer Elements tunajua ni madini gani tumewambia wachimbe?, ndio maana badala ya kuwekeza hela nyingi kwenye tume, mimi ningewekeza kwenye taasisi zetu za Geology.

"Kuna madini mengine mfano Scandium, hii yenyewe kilo moja ni dola 3,912 na duniani kwa mwaka zinahitajika tani kati ya 15 na 20 mwaka mzima na haya yako kwenye Layer Earth Elements Je, tunajua leseni tunazozitoa je tunajua hii ya asilimia 16 tuliyopewa ya bure je tunajua...?.

ASISITIZA UMUHIMU WA KUWA NA GOLD RESERVE

"Nije kwenye mada ya kuwa na Gold Reserve, kwa taarifa kwa wale ambao bado wanasita sita. Nimeenda kwa wale wanaotukopesha World Bank nikajulia hisa za World Bank ambazo zinadaiwa unavyozidi kuwa na hisa nyingi ndivyo ambavyo kura yako inazidi kuwa nzito.

"Kwa hiyo, World Bank nimechukua tatu voting power za Marekani ni kati ya 17 percent, Japan ni kati ya 8.55 percent, China 2.25 percent sasa angalia Marekani mwenye voting power kubwa kwenye World Bank ana dhahabu reserve tani elfu 8,133. tani gold reserve.

"Japan anayevot kwenye International Development Association ( IDA) World Bank ina mikopo ya aina mbili hii (IDA) ndio ya kwetu sisi maskini huko huyo Japan yeye voting power zake ni 8.5 percent ana reserve kwenye benki yake ya taifa tani 884, China ana voting power ya 2.5 percent ana reserve ya dhahabu tani 1,948 wewe Tanzania kwa nini bado unasita?...Wizara ya Madini na Benki Kuu kwa nini bado mnasita?.

"Lazima tuwe na hiyo, na kuwa na hiyo lazima refinery zetu mbili zifanye kazi. Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba refinery mbili za dhahabu tulizonazo ya Geita inaanza ku-process kilo 600 kwa siku ya Mwanza 480 kwa siku, lakini waheshimiwa wabunge hizo refinery hazina dhahabu na huenda zikafungwa,"amesema Prof. Muhongo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news