TAMWA Zanzibar yatoa angalizo kwa wazazi

NA DIRAMAKINI

WAKATI jamii ikielekea katika sherehe za Sikukuu ya Eid-El-Fitri, Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) kimewasihi wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa kuhakikisha kwamba watoto hawatoki peke yao kwenda kusherehekea.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Dkt.Mzuri Issa ambaye ni Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake, Zanzibar (TAMWA Zanzibar).

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,kila mwaka wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid Hajj au Eid El Fitri huripotiwa matukio ya udhalilishaji kwa watoto katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, ikiwemo kupotea kwa watoto, kubakwa, kulawitiwa, kutoroshwa na matukio ya aina hiyo.

"Hivyo ni vyema wazazi na walezi kuwakinga watoto wasikumbwe na vitendo vya udhalilishaji katika sehemu mbalimbali za viwanja vilivyotengwa kwa ajili ya sherehe hizo,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo imeongeza kuwa, kwa vile watendaji wa vitendo vya udhalilishaji,wanabadilisha mbinu mpya kila siku, na kukua kwa teknolojia hasa mawasiliano ya simu na kimtandao, TAMWA Zanzibar inatoa wito kwa wazazi kutoa taarifa mapema pale wanapogundua hali isiyokuwa ya kawaida ya Watoto wao au watu wanaowatuhumu kufanya vitendo hivyo.

"TAMWA Zanzibar inaiomba jamii kuacha tabia ya kumpa dhamana mtoto kuwa ndio kiongozi wa kundi la watoto wengine wadogo, kwani kufanya hivyo kunapelekea udhibiti mdogo wa watoto katika viwanja vya starehe,"imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Takwimu zilizotolewa mapema mwaka huu na Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinaonesha kuwa, jumla ya watoto 1,173 waliathirika na vitendo vya udhalilishaji na ukatili mwaka 2022.

Pia, kwa mujibu wa taarifa hiyo jumla ya matukio 883 sawa na asilimia 75 ambayo yaliripotiwa ni kwa watoto wenye umri kati ya miaka 11 hadi 17, hivyo watoto wapo katika hatari zaidi ya kukumbwa na vitendo vya udhalilishaji na ukatili. "TAMWA Zanzibar tunawatakia wananchi wote nchini Eid El Fitri njema."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news