Walimu Kasulu kwenda kujionea maajabu ya Hifadhi ya Taifa Gombe

NA RESPICE SWETU

JUMLA ya walimu wakuu 72 wa shule za msingi za umma na za watu binafsi zilizopo katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma wanatarajia kufanya ziara ya siku mbili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Gombe na Makumbusho ya Dr. Livingstone.

Akizungumzia ziara hiyo, mratibu wa safari ya walimu wakuu kwenda Gombe, Mwalimu Wenseslaus Lugaya amesema, pamoja na kujifunza, ziara hiyo inakusudia kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuutangaza utalii na vivutio vya ndani.

Amesema, kupitia ziara hiyo, jumla ya walimu wakuu 72 wa shule za Msingi za Umma na za watu binafsi zilizopo kwenye halmashauri ya Mji wa Kasulu, watapata fursa ya kutembelea na kujionea mambo mbalimbali kwenye maeneo hayo.

Lugaya anayejulikana zaidi kwa jina la Ghadafi amesema, kufanikiwa kwa ziara hiyo ni matokeo ya juhudi zilizofanyika za kuwahusisha wadau na wahisani mbalimbali kufadhili ziara hiyo.

"Tulipata wazo la kufanya ziara hiyo tukamhusisha mkurugenzi na wadau wengine wakaitika vizuri, nichukue nafasi hii kumshukuru sana mkurugenzi wetu kwa mchango wake na wadau wengine," amesema.

Pamoja na mkurugenzi wa Mji wa Kasulu, Ghadafi amewataja wadau wengine waliowezesha safari hiyo kuwa ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Kasulu Mjini, Prof.Joyce Ndalichako na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Wilaya ya Kasulu.

Wadau wengine kwa mujibu wa Ghadafi ni wafanyabiashara wa Mjini Kasulu, Chama cha Walimu (CWT) Wilaya ya Kasulu, wamiliki wa shule binafsi na idara ya elimu msingi ya halmashauri hiyo.

Ghadafi amefafanua pia kuwa kutokana na michango hiyo, gharama ya kufanyika kwa ziara hiyo kwa kila mmoja imepungua.

"Nauli ya kwenda Kigoma na kurudi mmelipiwa, nauli ya kwenda Gombe na kurudi Kigoma mmelipiwa, gharama ya matembezi hifadhini mmelipiwa, gharama za chumba cha kulala mmelipiwa, kiingilio cha Livingstone mmelipiwa; mnatakiwa kulipa elfu 32 tu za chakula na vinywaji kwa kila mmoja," amesema Ghadafi alipokuwa akiwahamasisha walimu kuchangamkia fursa hiyo.

Kufuatia hamasa hiyo, kundi la kwanza litakalokuwa na walimu 50 litaondoka Jumamosi ya wiki hii huku safari ya kundi la pili itakayokuwa na walimu 22 ikipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao.

Kuondoka kwa makundi kumetokana na maelekezo yaliyotolewa na uongozi wa hifadhi ya wanyama ya Gombe kwamba hawana uwezo wa kupokea "watalii" zaidi ya 50 kwa wakati mmoja.

Pamoja na kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Gombe na makumbusho ya Dr. Livingstone yaliyopo Ujiji Manispaa ya Kigoma, ziara hiyo pia itawafikisha walimu hao katika bandari ya Kigoma na kwenye uwanja wa ndege.

Miongoni mwa vivutio vikubwa katika Hifadhi ya Taifa Gombe. (Picha na Mtandao).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news