Waziri apiga marufuku matumizi ya upinde wa rangi shuleni

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Lela Muhamed Mussa amepiga marufuku matumizi ya upinde wa rangi zinazotuhumiwa kuwa ni alama ya mapenzi ya jinsia moja kwa skuli zote za Serikali na binafsi.

Mheshimiwa Waziri ameyabainisha hayo wakati akitoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na kamati iliyoundwa kuchunguza tuhuma za Skuli ya Seeds of Light inayomilikiwa na Taasisi ya Cr Hope Foundation iliyopo Kizimkazi.

Amesema, kufanya hivyo kunakusudia kuondoa hofu kwa jamii kuhusiana na uwepo wa vitendo hivyo ndani ya jamii, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya Kitanzania.

Pia amesema, wizara imejiridhisha kutokuwepo na vitendo vinavyoashiria tuhuma hizo ndani ya skuli hiyo baada ya kufanya uchunguzi kuanzia umiliki wa skuli, vifaa vinavyotumika, taaluma za walimu pamoja na njia wanazotumia katika kufundishia na kuona hakuna dalili ya tuhuma zilizotolewa.

Aidha, Waziri Lela amesema kuwa, kupitia tume hiyo iliyoshirikisha wadau wa elimu kupitia taasisi mbalimbali iliweza kufanya mahojiano na wanafunzi na wazazi wao ili kupata taarifa sahihi ambapo waligundua kuwepo kwa ukarimu mkubwa kwa wanafunzi na walimu wenye lengo la kuwafanya wanafunzi waweze kusoma vizuri.

Mhe.Lela akizungumzia kuhusiana na vifaa vya kufundishia na vya matumizi mengine vinavyotumika katika skuli hiyo ikiwemo vitabu na dawa amesema dawa hizo zimefanyiwa uchunguzi na kukutwa vipo salama ambapo baadhi ya vitabu vilichukuliwa na taasisi ya elimu kwa uchunguzi zaidi.

Wakati huo huo,Mheshimiwa Waziri amewaomba wazazi kuwa makini na kujiridhisha na skuli wanazowapeleka watoto wao ili kuwalinda na vitendo vitakavyoweza kuwaathiri pamoja na kuwaomba wanajamii kuepuka kuitumia mitandao ya kijamii kwa kutumia habari zinazoweza kuleta taharuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news