Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaandika historia Sekta ya Nyumba

NA DIRAMAKINI

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (SMT) imetia saini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar (SMZ) katika ushirikiano kiutendaji na kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi katika sekta za ardhi kwa pande zote mbili. 
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (SMT), Dkt. Angelline Mabula akiongoza hafla ya utiaji saini makubaliano baina ya Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT) na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar (SMZ) Mei 20, 2023 jijini Dodoma.

Makubaliano hayo ya kihistoria yamefikiwa Mei 20, 2023 jijini Dodoma ambapo yataziwezesha wizara hizo zisizokuwa za Muungano kutatua changamoto zinazozikabili katika kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wa SMT, Dkt.Angelline Mabula akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa, sekta ya ardhi na nyumba ni sekta ambayo ni muhimu katika kuwaletea wananchi maisha bora.

"Mheshimiwa Mwenyekiti Mwenza, kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa kuboresha ushirikiano baina ya pande mbili za Muungano, 

"Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania Bara na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Maakazi Zanzibar zimekuwa zikitekeleza maelekezo hayo ili kuimarisha Muungano na kuleta manufaa yenye tija kwa wananchi wa pande zote za Muungano na Taifa letu kwa ujumla. 

"Ushirikiano huo ni muhimu hasa kutokana na changamoto za udhibiti, usimamizi, matumizi ya Ardhi na Makazi kushabihiana kwa pande zote za Muungano. 

"Hivyo,kutokana na umuhimu wa jambo hili, tuliagiza watendaji wetu waweze kukutana ili kuratibu mambo ya msingi yatakayowezesha ushirikiano huu ili kuweka mfumo madhubuti wa kuwezesha ufanisi wa Sekta ya Ardhi na Makazi kwa pande zote za Muungano,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.
Makatibu Wakuu wa Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT), Mhandisi, Anthony Sanga na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar (SMZ), Dkt. Mngereza Mzee Miraji wakitiliana saini makubaliano baina ya wizara mbili hizo.

Waziri Dkt.Mabula amefafanua kuwa,sekta ya ardhi na makazi inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uendelezaji holela wa miji, kukosekana kwa miundombinu ya msingi katika miji, kuwepo kwa migogoro ya ardhi.

Pia upungufu wa vitendea kazi na wataalam na uhaba wa rasilimali fedha kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za sekta ya ardhi na makazi. 

"Kutokana na changamoto hizo naona tumechelewa kuwa na ushirikiano wa pamoja wa kukabiliana na changamoto hizo ili kuwa na miji bora, salama, yenye ufanisi na hivyo kuwaletea wananchi wetu maisha bora ambayo yanasisitizwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

"Sekta ya ardhi, nyumba na makazi ni sekta muhimu sana katika kuwaletea wananchi maisha bora na hivyo tunao wajibu mkubwa pande zote za Muungano kuhakikisha kuwa sekta hii inasimamiwa kikamilifu ili iweze kuwa na tija kwa watanzania wote,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula.

Waziri Dkt.Mabula ameongeza kuwa, "kufuatia maelekezo tuliyoyatoa kwa watendaji wetu, leo (Mei 20,2023) hii tunashuhudia jambo jema sana la utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Tanzania Bara na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar. 

"Vilevile, tunashuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) baina ya Mashirikia yetu ya Nyumba ambao ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ally Said wakipeana mikono baada ya kutiliana saini makubaliano hayo katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

"Mheshimiwa Waziri, pamoja na hafla hii ya leo nayapongeza mashirika haya mawili kwa kuwa na ushirikiano wa muda mrefu wa kubadilishana uzoefu, utaalam na mbinu mbalimbali za uendeshaji wa mashirika haya mawili." 

Amesisitiza kuwa, ustawi wa mashirika hayo yenye dhamana ya kusimamia sekta ya nyumba ni muhimu sana katika kuondoa changamoto za upatikanaji wa nyumba bora na za gharama nafuu kwa wananchi nchini. 

"Kama ulivyosikia kutoka kwa watendaji wetu, maeneo ya ushirikiano yalivyoainishwa katika Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yanaenda kufungua ukurasa mpya wa kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi, nyumba na makazi kwa pande zote mbili za Muungano. 

"Ni matarajio yetu kwamba hati hizi za makubaliano ya ushirikiano zitakazosainiwa leo zitakuwa ni nyenzo muhimu katika kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya sekta ya ardhi na nyumba kwa pande zote mbili za Muungano na hivyo kuwa na mchango chanya katika maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla. 

"Hivyo, nitoe rai kwa pande zote za Muungano kuhakikisha kuwa makubaliano haya yanatekelezwa kwa vitendo na pia ni muhimu kuwa na vikao vya mara kwa mara kwa ajili ya kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa makubaliano yetu. 

"Mheshimiwa Mwenyekiti Mwenza, nitoe shukrani zangu za dhati kwa makatibu wakuu pamoja na watumishi wote waliotekeleza kwa vitendo maelekezo yetu ya kuwa na utaratibu mahsusi wa kushirikiana baina ya wizara zetu kama ilivyoainishwa katika Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoU),"amefafanua waziri Dkt.Mabula.

Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mabula amesema,wizara ina imani kuwa Zanzibar kuna mazuri waliyoyafanya na Zanzibar watajifunza kwa yaliyofanyika Bara yatakayoboresha namna ya kuwahudumia wananchi wa pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Rahma

Naye Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar (SMZ), Mheshimiwa Rahma Kassim Ali amesema kuwa makubaliano waliyoyaingia baina yao ni vyema ukawekwa mpango kazi na kwamba kasoro yoyote ikijitokeza wakae watatue kwa sababu lengo ni kuleta mafanikio.

"Mheshimiwa Mwenyekiti mwenza, leo hii tumeshuhudia utiaji saini Hati za Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) wa pande zote mbili za Muungano katika sekta tulizokabidhiwa kuzisimamia kwa maslahi mapana ya Watanzania. 
"Natumaini hati hizo zitatuwezesha kujifunza mambo mbalimbali kutoka pande zote mbili za Muungano namna bora ya kutekeleza majukumu tuliyokabidhiwa. 

"Hivyo, ni wajibu wetu kuyatekeleza kwa vitendo yote tuliyokubaliana kwa lengo la kuboresha utendaji wa kazi zetu na kuwaletea wananchi wetu maisha bora. Kama ulivyosema hapo awali Mheshimiwa Waziri, makubaliano yetu yanaenda kuondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikikabili sekta zetu za Ardhi, Nyumba na Makaazi kwa pande zote za Muungano,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Rahma.

Aidha, amebainisha kuwa ni matumaini yake taasisi husika zitaendelea kukaa pamoja kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa lengo la kusaidiana katika kutatua changamoto zinazowakabili ambazo zinaleta usumbufu kwa wananchi nchini. 

Mheshimiwa Waziri Rahma amezitaka taasisi husika ziendelee kubadilishana uzoefu na kuangalia mbinu mpya zinazoendelea kutokea duniani ili zitumike kuleta mabadiliko makubwa yatakayoboresha utoaji wa huduma bora kwa Watanzania kupitia sekta wanazozisimamia. 

"Mheshimiwa Mwenyekiti mwenza, napenda kuchukua fursa hii tena kukupongeza wewe binafsi, Katibu Mkuu kutoka SMT, Katibu Mkuu SMZ, Wakurugenzi pamoja na Wataalamu wa pande zote mbili za Muungano kwa ushiriki wao mkubwa uliowezesha kufikiwa kwa makubaliano ambayo yametiwa saini hivi leo. Huu ni moyo wa uzalendo walioufanya na historia ya nchi yetu itaukumbuka mchango wao katika vizazi vingi vijavyo,"ameongeza Mheshimiwa Waziri Rahma. 

Makatibu wakuu

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (SMT),Mhandisi Anthony Sanga alisema katika kutekeleza mwongozo wa Ofisi ya Makamu wa Rais (SMT) na Ofisi ya Makamu wa Pili (SMZ) kuhusu taasisi zisizo za Muungano kukutana na kubadilishana uzoefu wa utendaji wa majukumu yao na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utekekelezaji wa majukumu yao,watendaji wa wizara pande zote mbili SMZ na SMT wamesisitizwa kukutana kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Sambamba na kuendelea kukuza ushirikiano baina ya watendaji wa pande mbili za Muungano katika usimamizi wa masuala ya Sekta ya Ardhi na Makaazi. 

"Waheshimiwa Mawaziri, mnamo Januari 13, 2023, Makatibu Wakuu pamoja na watendaji wa pande zote mbili tulikutana Mjini Zanzibar na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika vikao vya nyuma, kupokea na kujadili taarifa fupi za taasisi zilizo chini ya Wizara za SMT na SMZ. 

"Aidha, tulikubaliana maeneo ya ushirikiano na kuandaa Rasimu ya Hati za Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi (SMT) na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi (SMZ) na kupitia Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya NHC na ZHC hati ambazo zipo tayari kwa ajili ya kusainiwa leo ili taasisi na idara husika zijikite katika utekelezaji,"amefafanua Katibu Mkuu, Mhandisi Sanga.

Mhandisi Sanga ametaja maeneo mbalimbali ya ushirikiano yameanishwa ambayo wizara hizo za SMT na SMZ zinakusudia kwenda kutekeleza kuwa ni kukusanya, kuchakata na kubadilishana taarifa za ardhi baharini.

Pia, kubadilishana uzoefu kwenye maendeleo na matumizi ya mifumo ya habari na teknolojia kwa sekta ya ardhi,kushirikiana kitaalamu na kubadilishana uzoefu katika kuendeleza mfumo wa usimamizi na maendeleo ya sekta ya milki kuu ambayo inajumuisha makazi na nyumba.

Maeneo mengine ni kuweka utaratibu wa mafunzo, kubadilishana mawazo, ujuzi na utendaji mzuri ikiwa ni pamoja na kuwaunganisha wafanyakazi na kubadilishana wataalam wa sekta ya ardhi.

Kubadilishana uzoefu katika kuandaa na kutekeleza Sera, Sheria na miongozo mbalimbali ya Sekta ya Ardhi, kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika utafiti na maendeleo katika sekta ya ardhi,kushirikiana katika utekelezaji wa miradi ya pamoja kwa madhumuni ya kujenga uwezo.

Aidha, maeneo mengine ni kushirikiana na kubadilishana uzoefu juu ya utatuzi wa migogoro ya ardhi, kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika usimamizi na maendeleo ya miji mikongwe na kushirikiana katika nyanja nyingine kama watakavyokubaliana baina yao.

"Waheshimiwa mawaziri,napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa dhati kabisa, Katibu Mkuu kutoka SMZ, Manaibu Makatibu Wakuu, Wakurugenzi pamoja na Wataalamu wa pande zote mbili za SMT na SMZ kwa ushiriki wao mkubwa. 

"Hii inaonesha jinsi ambayo wanavithamini vikao hivi kwani ni kielelezo tosha cha kutambua moyo wao wa uzalendo kwa nchi yao,"ameongeza Mhandis Sanga. 

Dkt.Mngereza

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi (SMZ),Dkt.Mngereza Mzee Miraji amesema,kuna changamoto nyingi katika sekta ya ardhi na nyumba, lakini watapambana kuhakikisha pande zote zinaweza kupata ufumbuzi ili wananchi waweze kupata huduma bora.

NHC

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad amesema, kwa tayari shirika hilo limeshachukua baadhi ya mambo mazuri yanayofanywa na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) kama vile upangishaji wa muda mrefu wa hadi miaka 30 ambayo utekelezaji wake umeaanza kwa kuwekwa katika maandiko tayari kwa utekelezaji.
"Kama alivyosema Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, kuwa tutengeneze Action Plan, ya jinsi gani ya kuweza kutekeleza, tunajifunza sehemu zote mbili,japo kuwa nyie mmeanza juzi, lakini kuna mambo vile vile Bara tunatakiwa tujifunze kutoka kwenu, suala la long term lease, Mchechu (aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemiah Mchechu) aliwaambia tutalichukua.

"Infacts tumeshalichukua sisi. Tunalifanyia kazi, kwa hiyo tulimelichukua tukalieweka kwenye makaratasi huenda utekelezaji nikaanza nao mimi, kwa hiyo kuna mambo ambayo pamoja na kuwa mmeanza juzi, kuna mambo mazuri ambayo mmeyafanya,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

ZHC

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Bi.Mwanaisha Alli Said amesema, makubaliano hayo yana umuhimu mkubwa katika kustawisha sekta ya nyumba nchini kwa maslahi mapana ya Taifa na wananchi wake.

Bi.Said amesema kuwa, katika makubaliano hayo wamekubaliana mambo mengi, lakini kubwa ni kubadilishana wataalamu hasa upande wa Zanzibar hawana baadhi ya wataalamu kwa kuwa NHC lilianza muda mrefu na lina uzoefu mkubwa.

"Katika MoU kuna mambo mengi tumekubaliana, lakini kubwa ni kubadilishana wataalamu,ttunaamini kuna wataalamu upande hasa wa Zanzibar kuna baadhi ya wataalamu ambao hatuna. 

"Kwa sababau, wenzetu (NHC) kihistoria wameanzishwa mwanzo. Sisi tumeanzishwa mwaka 2014, ndiyo sheria imepita, lakini kazi shirika likaanza mwaka 2015. 

"Kwa hiyo wenzetu wako mbali sana...mbali sana, wameanguka wamenyanyuka, wameanguka wamenyanyuka. Kwa hiyo sisi tunajifunza, wenzetu walianguka vipi wakaweza kunyanyuka mpaka wakasimama. 

"Kwa hiyo tumekubaliana kwenye MoU kuweza kubadilishana watalaamu, lakini na wataalamu wenyewe kuweza kuvuka maji, mtaalamu wa Zanzibar akija kufanya kazi SMT isiwe na tatizo lolote kisheria, japo kuwa kihistoria wataalamu na utaalamu wa NHCwameshachukuliwa sana ndiyo maana shirika (ZHC) likaweza kusimama,"amefafanua Bi.Said.

MOU

Aidha,kwa upande wa ngazi ya Wizara Makatibu Wakuu wa Wizara za Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi za Tanzania (SMT), Mhandisi, Anthony Sanga na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar (SMZ), Dkt. Mngereza Mzee Miraji walitiliana saini makubaliano baina ya wizara mbili hizo.

Kwenye ngazi ya mashirika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah Hamad na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC),Mwanaisha Ally Saidi wametiliana saini mkataba huo katika hafla hiyo.
Kuhusu makubaliano hayo mapya ya ushirikiano yatakayodumu kwa miaka 10 kuanzia tarehe yaliyosainiwa yatawezesha taasisi hizo kuweka mipango ya kubadilishana mawazo na ujuzi na kuweza kuwasaidia kwa kiasi kikubwa Watanzania wengi, hususani vijana katika kupata ujuzi wa kuutumia kwenye kuongeza tija kwenye sekta ya ujenzi nchini.

Eneo jingine ambalo ni muhimu katika mustakabali wa taasisi hizi ni rasilimali watu na mbinu bora ili kuwezesha kuhamisha utaalamu, ujuzi na kujengeana uwezo kwa faida ya pande zote mbili hivyo kuwaongezea umahiri pamoja na maarifa zaidi na utamaduni wa mazingira ya kazi husika.

Makubaliano hayo pia yataziwezesha taasisi hizo mbili kuainisha fursa za mafunzo na kushirikiana kupeana nyenzo za mafunzo na kubadilishana taarifa muhimu zinazohusu uendeshaji wa mashirika yao bila kuathiri sera zinazolinda usiri wa taasisi hizo.

Katika makubaliano hayo, wataalamu wa maendeleo ya biashara na utafiti wa Shirika la Nyumba la Zanzibar watafaidika kupatiwa mafunzo kwa mujibu wa taaluma zao kutoka Shirika la Nyumba la Taifa.

Ushirikiano wa Shirika la Nyumba la Taifa na Shirika la Nyumba la Zanzibar upo kwa muda mrefu lakini Mkataba mpya wa ushiririkiano wa sasa utatoa fursa kubwa zaidi kuhakikisha Maendeleo ya pande zote mbili yaliyofikiwa na Mashirika hayo yanawanufaisha wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Mashirika la NHC na ZHC yamesainiana mkataba huo baada ya kutambua mahitaji ya kuongeza mashirikiano kati yao yenye lengo la kustawisha mabadilishano ya ujuzi na welewa mpana kati ya pande mbili hizo na kufikia malengo yao kwa haraka na tija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news