Jeshi la Polisi latoa tahadhari za kiusalama mchezo kati ya Yanga SC na USM Alger kesho

NA GODFREY NNKO

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linatambua kuwa Jumapili ya Mei 28, 2023 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam kutakuwa na mchezo wa soka fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baina ya klabu ya Yanga ya Tanzania na USM Alger ya nchini Algeria utakaochezwa kuanzia saa 10:00 jioni.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,SACP Muliro J.Muliro amesema kuelekea mchezo huo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam tayari linachukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo huo.

"Usalama siku ya mchezo utakuwa wa kiwango cha juu maeneo yote ya kuzunguka uwanja ndani, nje na barabarani. Hairuhisiwa mtu yeyote kwenda uwanjani na silaha ya aina yoyote, isipokuwa baadhi ya vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawatahadharisha baadhi ya mashabiki wenye tabia ya kuwasha fataki au baruti uwanjani, kurusha chupa au kitu chochote. Hayo ni baadhi ya makosa ya mambo ya kiusalama kwenye viwanja vya soka.

"Jeshi la Polisi halitavumilia tabia hizo na zingine ambazo zimepigwa marufuku na vyama vya soka FIFA, CAF na TFF. Watakaokaidi, watakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria. Jeshi la Polisi linawatakia mashabiki wa soka kushangilia kistaarabu,"amefafanua SACP Muliro leo Mei 27, 2023 jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news