Kijiji cha wakulima, wafugaji stadi Musoma Vijijini chaunganishwa kwenye barabara kuu

NA FRESHA KINASA

ZAIDI ya wakazi 4,000 katika Kijiji cha Kinyang'erere kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara wameondoka na changamoto ya kukosa huduma mbalimbali muhimu za jamii baada ya kuunganishwa na miundombinu muhimu.
Ni kufuatia Serikali kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 11 yenye madaraja mawili, kwenye mito miwili ukiwemo Mto Sijati na Nyamagusi kwa ajili ya kukiunganisha kijiji hicho cha Kinyang'erere kwenye barabara kuu ya Murangi (Musoma Vijijini-Bugwema-Masinono-Manyamanyama katika Wilaya ya Bunda. 

Kijiji cha Kinyang'erere ni moja ya vijiji vinne (Bugwema, Kinyang'erere, Masinono, Muhoji) vya Kata ya Bugwema Jimbo la Musoma Vijijini. Vijiji vyote vinne vipo ndani ya Bonde la Bungwema ambalo Serikali imepanga kujenga miundombimu ya kilimo cha umwagiliaji.

Hayo yamebainishwa Mei 11, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini. 

"TARURA inafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kujenga barabara (kilomita 11), yenye madaraja mawili, kwenye mito miwili (Sijati na Nyamagusu) kwa ajili ya kukiunganisha Kijiji cha Kinyang'erere kwenye barabara kuu ya Murangi (Musoma Vijijini)-Bugwema-Masinono-Manyamanyama (Bunda).

"Mazao makuu yanayolimwa kijijini Kinyang'erere ni mpunga, dengu, choroko, mahindi, maharage na alizeti. Huku mifugo muhimu ya kijiji hiki ni ng'ombe, kondoo na mbuzi.
"Barabara hiyo ya kilomita 11 inaunganisha Wilaya za Musoma na Bunda kupitia Kijiji cha mpakani kiitwacho Karukekere (Mwibara, Bunda),"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji hicho wakizungumza na DIRAMAKINI, wameishukuru Serikali kwa kujenga barabara hiyo ambapo wamesema itakuwa muhimu kwa kuwawezesha kwenda kupata huduma za kijamii kuimarisha shughuli za kiuchumi ikiwemo kusafirisha mazao yao. 

"Wakati wa mvua kina mama walipata tabu sana walipotaka kwenda kujifungua kijiji jirani,wakati mwingine kubebwa kwenye mkokoteni na wakati mwingine walijifungulia njiani kutokana na kukosa barabara. 

"Lakini tunamshukuru Rais Samia (Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan) kuendelea kugusa maisha yetu wana Musoma Vijijini kwa kujenga barabara hii.

"Pia,itasaidia wanafunzi kwenda masomoni wakati wote baada ya kujengwa madaraja ambayo awali wanafunzi walishindwa kuhudhuria masomo hasa wakati wa masika,"amesema Esta Peter. 
"Barabara hii itasaidia wananchi kusafirisha mazao yao kwani awali wakati wa masika ilikuwa kero kubwa ilibidi wasafirishe wakati wa kiangazi kutokana na njia kutopitia. Nimshukuru Mbunge Prof. Muhongo kwa kufuatilia hatimaye barabara hii imejengwa na Rais Samia pia kutoa fedha ambazo zimefanikisha jambo hili,"amesema Juma Ndilana Mwenyekiti wa wa kijiji hicho. 

Mhandisi Mrisho Shomari kutoka Ofisi ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Musoma amesema,"barabara hii inaitwa Masinono-Kinyang'erere ina urefu wa kilomita 11 napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea fedha nyingi za ujenzi wa barabara hasa Wilaya ya Musoma. Mwanzoni kulikuwa na changamoto ya bajeti ambayo tulikuwa nayo ilikuwa ndogo,"amesema na kuongeza kuwa.
"Bajeti haikukidhi ufunguaji wa barabra hata ujenzi wa madaraja makubwa. Kipekee nimshukuru tena Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuongeza fedha upande wa TARURA ambazo zinafanikisha miradi kama hii ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi,"amesema Mhandisi Shomari. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news