Makamu wa Rais ateta na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)

NA MWANDISHI WETU
Sharm El Sheikh

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango tarehe 24 Mei 2023 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt.Akinwumi Adesina kando ya Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri.
Katika mazungumzo hayo wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Benki hiyo katika miradi ya ujenzi wa miundombinu hususani utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Uvinza nchini Tanzania hadi Gitega nchini Burundi.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amefanya mazungumzo na Rais wa Benki ya African Export – Import (Afreximbank) inayojishughulisha na ufadhili wa Biashara za Kimataifa Prof. Benedict Oramah mazungumzo yaliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Sharm El Sheikh nchini Misri.

Katika mazungumzo hayo Benki ya Afrexim imeonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa Kituo cha Ubora cha Matibabu pamoja na ujenzi wa taasisi ya viwango vya ubora wa kimataifa nchini Tanzania.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema serikali inatambua mchango wa Benki hiyo katika ufadhili wa miradi mikubwa ikiwemo ya nishati pamoja na namna inavyotoa mitaji kwa sekta binafsi nchini Tanzania hususani mabenki.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuboresha miundombinu kama vile ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa, barabara na huduma mbalimbali katika Makao Makuu ya nchi Dodoma hivyo ameikaribisha Benki hiyo kuwekeza mkoani humo hususani kituo cha ubora cha matibabu.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu Mwamba, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango – Zanzibar Dkt. Juma Malik Akili, Balozi wa Tanzania nchini Misri Balozi Emmanuel Nchimbi, Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Noel Kaganda pamoja na Mshauri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mabadiliko ya Tabianchi Dkt. Richard Muyungi.

Makamu wa Rais yupo nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) unaofanyika katika mji wa Sharm El Sheikh.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news