Serikali yatoa rai kwa wananchi kuhusu magonjwa ya mlipuko

NA MWANDISHI WETU

WATANZANIA wametakiwa kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuyaweka mazingira katika hali ya usafi ili kujikinga na Magonjwa ya Mlipuko.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Muleba, Dkt. Kisaka Deo, baada ya kufanya ziara katika visiwa vya Goziba, Kerebe na Nyaburo vilivyopo ndani ya ziwa Victoria kwa ajili ya kujionea namna Elimu ya Afya ilivyozaa matunda katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Marburg mkoani Kagera. 

“Ili kujikinga na Magonjwa yote lazima tuyaweke mazingira yetu katika hali ya usafi, unaponawa mikono haujikingi na ugonjwa wa Marburg pekee bali inasaidia kujikinga na magonjwa kama vile kuhara, Kipindupindu na kuumwa tumbo,"amesema Dkt.Deo.

Aidha, Dkt. Kisaka amewahimiza mama wajawazito kuwa na desturi ya kuwahi kliniki mapema pamoja na kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata chanjo mbalimbali.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Kerebe Kanali Sefu amesema serikali imechukua hatua madhubuti katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

“Maelekezo ya mara kwa mara serikali imekuwa ikiyatoa hawajatuacha nyuma, kwakweli Wizara ya Afya naishukuru licha ya mazingira magumu ya kufikika huku lakini wataalam wamekuwa wakifika na kutoa maelekezo na baada ya elimu kutolewa mpaka sasa hatujapata mhisiwa yeyote na watu wanaendelea kuchapa kazi kama kawaida,”amesema Kanali Sefu.

Naye Diwani wa kata ya Kerebe Bw. Sudy Said amesema, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jambo kubwa la kutuangalia na sisi huku visiwani baada ya ugonjwa huu kujitokeza nashukuru walikuja wataalam wa Afya kutoka Wizarani na Mkoani kwa kweli walifika kwa wakati wametoa semina na vifaa mbalimbali vya kujikinga ikiwemo ndoo na vitakasa mikono.

Nao, baadhi ya wananchi akiwemo mkazi wa kisiwa cha Nyaburo Bi. Mary Josephat ameishukuru Serikali kwa kuondoa hofu na taharuki kwa wananchi kwa utoaji wa Elimu ya Afya hali ambayo imesabibisha kuzingatia kanuni za afya na kuendelea na shughuli za kila siku.

“Tunashuku sana maana kila mtaalam wa afya anapokuja anatuelimisha juu ya kuzingatia usafi wa mwili na mazingira kwakweli somo linatuingia kichwani, tunazingatia usafi ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko,”amesema Bi. Mary.

Ikumbukwe kuwa jumla ya Viongozi Watatu na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) Sita walifikiwa katika kisiwa cha Goziba kwa kupewa elimu ya magonjwa ya mlipuko huku Wananchi 161 na Wanafunzi 124 wa Shule ya Msingi wote kwa pamoja walifikiwa kupatiwa elimu ya kujikinga na magonjwa hayo katika kisiwa cha Kerebe.
Elimu hiyo ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko imetolewa na Elimu ya Afya kwa Umma kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja UNICEF na MV Jubilee Hope Medical Ship Program chini ya Kanisa la AIC Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news