Mashindano ya Netiboli yafana Malya

NA ADELADIUS MAKWEGA
Mwanza

KWA muda wa mwezi mmoja sasa katika viwanja vya ndani vya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kunafanyika Ligi ya Netiboli inayokusanya timu kadhaa za eneo la Malya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambapo sasa yamefikia nusu fainali. 
Ligi hiyo iliyoanza Mei 1, 2023 Malya Queen Walifungua dimba na Malya Sekondari, Malya Queen wakishinda kwa magoli 21 kwa 15 huku Level 4 ambao ni wanachuo wa Astashahada ya Michezo kutoka Malya waliwafunga FDC-Chuo cha Maendeleo ya Jamii kwa kutokupata kitu. 

Michezo hiyo iliendelea tena Mei 5, 2023 ambapo Level 5 ambao ni wanachuo wa pia wa mwaka wa kwanza wa Stashahada ya Michezo Chuo Cha Malya walipambana na ndugu zao wa damu Level 6 ambao ni wanachuo wa mwaka wa pili wa Stashahada ya Michezo Malya mshindi alikuwa Level 5 kwa magoli 52 kwa 19.
Viwanja vya ndani vya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya viliwaka moto tena Mei 6, 2023 ambapo Malya Queen ambao ni wenyeji wa eneo hili wameibuka kuwa tishio kubwa kwa namna wanavyoweza kupiga chenga za mikono kwa wapinzani wao wakitupa mipira hiyo kudunda, kurusha kutokea juu na kurusha kwa pembeni na walionesha umalikia wao kwa kuwafunga Level 6 kwa magoli 35 kwa 26. 

Safari ya mashindano hayo ya kumtafuta mshindi ambaye atajinyakulia mbuzi mkubwa mwenye kilo nyingi yaliendelea Mei 7, 2023 ambapo Level 4 walipambana na Nyabubinza Sekondari ambapo matokeo yalikuwa Level 4 walipata magoli 27 na Nyabubiza waliambulia magoli 14 tu.
Mashindano haya yalipumzika kwa siku chache na yaliendelea Mei 12, 2023 ambapo Level 5 walipambana na Malya Sekondari, matokeo Level 5 walishinda kwa magoli 34 kwa 15, nayo mechi ya pili kwa siku hiyo ilifuata ilikuwa ni baina FDC na Nyabubinza Sekondari ambapo Nyabubinza walipata magoli 20 huku FDC hawakuambulia hata goli moja. 

Mei 14, 2023 mpambano ulikuwa mkali mno baina ya Level 5 na Malya Queens huku Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Richard Mganga akiwa katika viwanja hivyo alishuhudia mmenyano huo wa kufa na kupona ambao wengi wanatabiri ndiyo utakuwa fainali ambapo Level 5 walishinda kwa magoli 30 kwa 20 tu huku jasho likiwatoka kweli kweli. 
Akizungumuza mara baada ya kupoteza mchezo huo kocha wa Malya Queens Mwalimu Jackline Malulu alisema, 

“Japokuwa tumefungwa, sijakata tamaa bado, natambua wenzetu wametuzidi kiasi lakini ninatoa ahadi mechi inayofuata tutashinda na hata tutachukua mbuzi, sisi ndiyo Malkia wa Malya.” 
Akizungumza kwa kujinasibu mchezaji maarufu wa Level 5 ambaye na mwanachuo wa Chuo cha Maandeleo ya Michezo Malya Ndinagu Sungura anayecheza kama GA huku akifunga magoli mengi tangu mshaindano hayo yaanze amesema, 

“Sisi ndiyo timu pekee tunaokibeba chuo hiki, mbuzi atabakia chuoni na mchele vitungu na viungo vya mapishi kumla mbuzi viko tayarijikoni kusibiri siku ifike tu tumalize mambo.”
Mpambano wa pili kwa Mei 14, 2023 ulikuwa baina ya Malya Sekondari na Level 6 ambapo Level 6 walishinda kwa magoli 31 kwa 28, nayo Nusu Fainali inatarajiwa kufanyika Mei 19, 2023, 

Mashindano hayo wakati yakiendelea katika viwanja vya ndani vya Chuo hiki yalipambwa na tambo kadhaa za vitisho, ngoma na nyimbo ambapo tambo hizo ziliwavutia mno watazamaji wa mchezo huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news