MPC yabaini mema zaidi uchumi wa Tanzania

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imeridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei, wakati ikichangia ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta ya fedha. 

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Mei 23, 2023 na Mwenyekiti wa MPC ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba.

Ni baada ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kukutana Mei 22, 2023 kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Machi na Aprili 2023, mwenendo wa uchumi wa dunia na hapa nchini, na kufanya maamuzi ya utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Mei na Juni 2023.

"Utekelezaji huo uliwezesha ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.

"Aidha, utekelezaji huo wa sera ya fedha ulisaidia kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya Extended Credit Facility (ECF) kwa mwezi Machi 2023, na kuweka msingi thabiti wa kufikiwa kwa malengo
ya programu hiyo kwa mwezi Juni 2023,"amefafanua Gavana Tutuba kupitia taarifa hiyo.

Katika kujadili mwenendo wa uchumi,MPC ilibaini kuwa mwaka 2022 ukuaji wa uchumi wa dunia ulipungua, na ukuaji wa uchumi katika mwaka 2023 unatarajiwa kuendelea kupungua kutokana na athari za vita nchini Ukraine, kuongezeka kwa riba kutokana na utekelezaji wa sera za fedha zinazolenga kupunguza kasi ya mfumuko wa bei, na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia,mfumuko wa bei duniani umeendelea kupungua tangu robo ya mwisho ya mwaka 2022,japo umebaki juu ya malengo katika nchi nyingi.

Aidha, bei za bidhaa katika soko la dunia zimeendelea kupungua, ingawa viwango vyake vimebaki juu ya viwango vilivyorekodiwa kabla ya kuibuka kwa vita nchini Ukraine.

"Mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kupungua, kutokana na kuendelea kuongezeka kwa riba ya utekelezaji wa sera ya fedha, pamoja na kuendelea kupungua kwa bei za bidhaa katika soko la dunia,"imefafanua sehemu ya taarifa ya Mwenyekiti wa MPC.

Kuhusu uchumi wa ndani, Kamati ya Sera ya Fedha ilibaini kuwa, mwendendo wa ukuaji wa uchumi nchini umeendelea kuwa wa kuridhisha, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya kibiashara, uwekezaji unaoendelea kufanywa na sekta ya umma na binafsi, kuimarika kwa shughuli za utalii na ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

MPC imebaini kuwa, ukuaji wa uchumi katika robo tatu za mwaka 2022 kwa Tanzania bara ulikuwa wastani wa asilimia 5.2 na unatarajiwa kukua kwa takriban asilimia 5 kwa mwaka mzima wa 2022, na asilimia 5.2 kwa mwaka 2023.

Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2022, ukiwa juu ya ukuaji wa asilimia 5.1 kwa mwaka 2021.

Uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1 kwa mwaka 2023, sambamba na jitihada zinazoendelea za kuimarisha uchumi wa bluu, sera nzuri za kiuchumi na kuendelea kuimarika kwa shughuli za utalii.

Wakati huo huo, mfumuko wa bei kwa Tanzania bara umeendelea kupungua kwa mwezi wa tatu mfululizo na kufikia asilimia 4.3 mwezi Aprili 2023, ukibaki chini ya lengo la asilimia 5.4 kwa mwaka.

Kwa upande wa Zanzibar, MPC imebaini mfumuko wa bei uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.5 mwezi Aprili 2023, kutoka asilimia 7.1 mwezi Machi 2023, ukilinganishwa na lengo la asilimia 5, kutokana na kuongezeka kwa bei za vyakula.

Aidha,kamati inatarajia mfumuko wa bei kuendelea kupungua katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2022/23, kutokana na matarajio ya kupungua kwa bei za vyakula na nishati katika soko la dunia.

Pia, utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ongezeko la ukwasi kwenye uchumi pamoja na ongezeko la chakula nchini vinatarajiwa kuchangia kupunguza mfumuko wa bei.

"Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) uliendana na utekelezaji wa sera ya fedha,ukikua kwa asilimia 17.2 kwa mwaka ulioishia Aprili 2023, ikilinganishwa na lengo la ukuaji wa asilimia 10.3 kwa mwaka 2022/23.
"Mwenendo huu ulichangiwa zaidi na ukuaji wa kasi wa mikopo kwa sekta binafsi wa takriban asilimia 23, juu ya lengo la asilimia 10.7 kwa mwaka 2022/23.

"Katika robo tatu za kwanza za mwaka 2022/23, utekelezaji wa bajeti za Serikali kwa kiasi kikubwa umeendelea kufanyika kuendana na malengo. Mapato ya ndani yalifikia asilimia 95.1 ya lengo kwa Tanzania bara, na asilimia 95.9 ya lengo kwa upande wa Zanzibar.

"Hii ni dalili ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, sanjari na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato, na utayari wa walipa kodi katika kulipa kodi kwa wakati,"imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, matumizi ya Serikali yameendelea kufanyika kulingana na rasilimali fedha zilizopo katika kukidhi vipaumbele vilivyowekwa ndani ya bajeti ya mwaka 2022/23;

MPC imebaini kuwa, sekta ya nje imeendelea kuathiriwa na misukosuko inayotokana na athari za vita inayoendelea nchini Ukraine na janga la UVIKO-19, hali ambayo imechangia bei za bidhaa katika soko la dunia kubakia juu, sanjari na kuvurugika kwa mnyororo wa ugavi.

"Misukosuko hii imesababisha kuongezeka kwa nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nchi za nje, kuongeza mahitaji ya fedha za kigeni, pamoja na kupanda kwa gharama za kukopa katika masoko ya kimataifa.

"Kutokana na changamoto hizi, akiba ya fedha za kigeni ilipungua na kufikia dola za Marekani bilioni 4.9 mwishoni mwa mwezi Aprili 2023, kutoka dola za Marekani bilioni 5.5 mwishoni mwa mwezi Aprili 2022. Kiwango hiki kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi 4.4, kikiwa ndani ya lengo la nchi la miezi minne.

"Sekta ya kibenki iliendelea kuwa imara na thabiti, yenye kiwango cha kutosha cha mitaji, ukwasi na yenye kutengeneza faida. Amana na rasilimali za benki ziliendelea kuongezeka mwezi Aprili 2023, sambamba na kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, pamoja na kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia kidigitali,"amebainisha Mwenyekiti wa MPC kupitia taarifa hiyo.

Aidha, ubora wa rasilimali za mabenki uliendelea kuimarika, ukiakisiwa na kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu na kufikia asilimia 5.45 mwezi Aprili 2023, ikilinganishwa na asilimia 8.25 mwezi Aprili 2022;

Kufuatia mwenendo mzima wa uchumi hapa nchini na wa dunia, Kamati ya Sera ya Fedha imeridhia Benki Kuu kuendelea na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la kiwango cha ukwasi katika uchumi kwa mwezi Mei na Juni 2023.

Utekelezaji huu wa sera ya fedha unalenga kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5.4 katika kipindi kilichosalia cha mwaka 2022/23, na kufanikisha kufikiwa kwa malengo yaliyoainishwa kwenye programu ya IMF chini ya mpango wa ECF kwa mwezi Juni 2023.

"Benki Kuu kwa upande wake itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuchukua hatua stahiki kwa lengo la kukabiliana na athari za mitikisiko yoyote itakayojitokeza,"imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news