MPC:Uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.1 mwaka 2023

NA GODFREY NNKO

UCHUMI wa Zanzibar chini ya Serikali ya Awamu ya Nanne inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi unatarajiwa kukuwa kwa asilimia 7.1 mwaka 2023.

Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa leo Mei 23, 2023 na Mwwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba.

Ni baada ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kukutana Mei 22, 2023 kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Machi na Aprili 2023, mwenendo wa uchumi wa dunia na hapa nchini, na kufanya maamuzi ya utekelezaji wa sera ya fedha kwa mwezi Mei na Juni 2023.

Kamati iliridhishwa na utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi kwenye uchumi ili kudhibiti mfumuko wa bei, wakati ikichangia ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta ya fedha.

Utekelezaji huo uliwezesha ongezeko la ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi, na kusaidia kuweka mazingira mazuri ya kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.

"Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unakadiriwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2022, ukiwa juu ya ukuaji wa asilimia 5.1 kwa mwaka 2021.

Picha na Zanzibarworldtour.

"Uchumi wa Zanzibar unatarajiwa kukua kwa asilimia 7.1 kwa mwaka 2023, sambamba na jitihada zinazoendelea za kuimarisha uchumi wa buluu, sera nzuri za kiuchumi na kuendelea kuimarika kwa shughuli za utalii,"imefafanua sehemu ya taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Gavana Tutuba.

Aidha, kamati imebainisha kuwa, kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.5 mwezi Aprili 2023, kutoka asilimia 7.1 mwezi Machi 2023, ukilinganishwa na lengo la asilimia 5, kutokana na kuongezeka kwa bei za vyakula.

"Kamati inatarajia mfumuko wa bei kuendelea kupungua katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2022/23, kutokana na matarajio ya kupungua kwa bei za vyakula na nishati katika soko la dunia.

"Aidha, utekelezaji wa sera ya fedha inayolenga kupunguza kiwango cha ongezeko la ukwasi kwenye uchumi pamoja na ongezeko la chakula nchini vinatarajiwa kuchangia kupunguza mfumuko wa bei,"imeongeza sehemu ya taarifa ya kamati.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news