Prof.Muhongo amlilia waziri mstaafu Herman Kirigini

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara,Prof.Sospeter Muhongo amewakumbusha viongozi mbalimbali waliopo katika ofisi za serikali na binafsi kuwa kielelezo bora katika utumishi wao kwa kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati na uadilifu kama alivyofanya marehemu Herman Kirigini wakati akihudumu serikalini. 
Ameyasema hayo Mei 26, 2023 katika Kata ya Kamunyonge Manispaa ya Musoma wakati akitoa salamu za rambirambi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Waziri wa kwanza wa mifugo na baadaye Waziri wa Kilimo na Mifugo, Herman Kirigini ambaye alifariki dunia Mei 23, 2023 kutokana na ugonjwa wa kisukari. 

Prof.Muhongo amesema, Herman Kirigini alikuwa kiongozi mahiri na makini aliyejipambanua kusaidia Wananchi kwa moyo wa dhati katika kutatua kero zao na kwamba viongozi mbalimbali waliweza kupita Katika mikono yake ambao kwa Sasa wanahudumu Ofisi za serikali na binafsi hivyo wafuate nyayo zake. 

Ameongeza kuwa, ni viongozi wachache ambao wanaweza kusimama na kusaidia jamii kama ambavyo alifanya kiongozi huyo wakati akihudumu katika nyazifa alizopita kwani alijali wananchi na kutanguliza mbele uadilifu. 
Amebainisha kwamba, yeye pia aliweza kusaidiwa na Herman Kirigini kutoa gari bandarini wakati akiwa kiongozi na pia alisimamia maslahi ya wananchi katika utumishi wake jambo ambalo viongozi wanapaswa kulionesha katika utumishi wao ili kuacha alama njema kwa vizazi vijavyo 

Akisoma wasifu wa marehemu, Peter Kirigini amesema, Herman Kirigini alizaliwa Desemba 22, 1945 na katika kipindi cha uhai wake alishika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo Waziri wa Kwanza wa Mifugo,na baadaye Waziri wa Kilimo na Mifugo na akiwa Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini.

Pia, amewashukuru madaktari waliokuwa wakimhudumia Herman Kirigini kipindi cha ugonjwa uliokuwa ukimsumbua wa kisukari kwa muda mrefu. 

Marehemu Herman Kirigini anatarajiwa kuzikwa leo Mei 27, 2023 kijijini Muliaza wilayani Butiama mkoani Mara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news