Rais Dkt.Mwinyi awapa majibu wapotoshaji kuhusu Uchumi wa Buluu

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema,wale ambao wanadai kuwa Uchumi wa Buluu haujawafikia wananchi huenda hawafahamu maana ya halisi ya dhana hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Serikali na binafsi katika Ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar leo,ambapo amezungumzia zaidi ile ziara yake nchini Qatar hivi karibuni .(Picha na Ikulu).

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 Ikulu jijini Zanzibar katika vikao vya kawaida vya kila mwezi na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu nchi.

"Kuhusu Uchumi wa Buluu wanasema haujawafikia wananchi, labda hawajui maana ya Uchumi wa Buluu kwa sababu Uchumi wa Buluu ni sekta ambazo tumezitaja, kama ni utalii, utalii umeongezeka hapa Zanzibar, leo ni ndege ngapi zinakuja hapa Zanzibar, madereva wa teksi wote wanapata kazi za kufanya.

"Leo watu wangapi wanaolima mbogamboga wanaouza kwenye mahoteli, ni wavuvi wangapi wanaovua katika nchi hii wanalo soko la kuuza samaki wao, sasa huko si ndiyo kuwafikia wananchi unataka tuwafikie vipi?.

"Huo ndio Uchumi wa Buluu, utalii umeongezeka katika nchi, uvuvi umeongezeka, ninyi ni mashaidi wakati ule tulikuwa tunatoa maboti ya uvuvi na watu wa mwani, si ndio kuwafikia wananchi, tuwafikieje zaidi ya hapo? Kwenye suala la mafuta na gesi ndio hawa tunawatafuta wawekezaji ili kufanya hiyo kazi.

"Kwa ujumla tumeona ongezeko kubwa la masuala yanayohusu masuala ya uchumi wa buluu kutokana na mkazo tuliouweka katika sekta ya uchumi wa buluu na wananchi wananufaika kwa sababu tumetoa sisi maboti kwa wavuvi na wakulima wa mwani.

"Tumewasaidia kujenga mabwawa ili waweze kufuga samaki, tumetoa mikopo kwa ajili ya wale wanaofanya shughuli zao katika uchumi wa buluu, zaidi nini kifanyike ili waone tumewafikia wananchi?.

"Kwa hiyo hizi porojo nyingine za kisiasa tuwaachie wapige ndiyo kazi yao kusimama majukwaani kupiga porojo, lakini ukweli unabaki pale pale ukitazama mambo ambayo yamefanywa na Serikali hii utaona kabisa wananchi tumewafikia,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Rais alipoanzia

Novemba, 2020 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi, kwa uwezo aliopewa na Kifungu namba 41 (2) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 alianzisha rasmi Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar.

Lengo kuu la wizara hiyo ni kusimamia utekelezaji wa kasi na endelevu wa fursa zilizopo na vipaumbele vyake vya uchumi unaotegemea rasilmali za bahari au Uchumi wa Buluu ili kuijenga Zanzibar mpya yenye uchumi wa kisasa.
Wizara inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia matumizi na usimamizi endelevu wa bahari na ukanda wa pwani pamoja na kusimamia, kuratibu na kuimarisha fursa za uwezeshaji na uwekezaji katika sekta za uvuvi, mazao ya baharini, kilimo cha mwani na utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia.

Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 imeiweka Sekta ya Uchumi wa Buluu kuwa sekta kuu ya kukuza uchumi wa Zanzibar ili kuitoa Zanzibar katika umaskini na kuifikisha kuwa nchi yenye kipato cha kati cha hali ya juu.

Aidha, mpango wa uimarishaji wa sekta ya Uchumi wa Buluu unaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025, Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar (ZADEP) wa Mwaka 2021-2026, Sera na Mikakati ya Uchumi wa Buluu, Sera ya Uvuvi na Mazao ya Baharini, Sera ya Mafuta na Gesi, pamoja na mipango jumuishi na shirikishi ya sera nyingine mbalimbali za kitaifa zinazohusiana na usimamizi wa bahari na Uchumi wa Buluu.

Pia, katika utekelezaji wa maazimio na mikataba ya kimataifa, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ina jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa mikataba mbalimbali ya kimataifa inayohusiana na usimamizi wa bahari na Uchumi wa Buluu hususani kwa Zanzibar.

Lengo Namba 14 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 14) la Umoja a Mataifa linalohusiana na Usimamizi na Maendeleo Endelevu ya Bahari, Lengo Nambari 6 la Agenda ya Umoja wa Afrika ya Mwaka 2063 (Agenda 2063), pamoja na mikataba na itifaki mbalimbali za kikanda na kimataifa na kikanda inayoongoza na kuhimiza uimarishaji wa Uchumi wa Buluu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news