Serikali yakoleza kasi mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mheshimiwa Jenista Mhagama amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan imeongeza kasi ya kudhibiti dawa za kulevya nchini.

Mheshimiwa Mhagama ameyasema hayo leo Mei 30, 2023 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelezea kuhusu kuwasilisha taarifa bungeni inayoangazia kuhusu hali ya dawa za kulevya ya mwaka 2022.

"Leo tarehe 30 Mei, 2023, kama ilivyo ada nimewasilisha mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini ya mwaka 2022 nikitekeleza matakwa ya Kifungu cha 60 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015, kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 15 ya mwaka 2017.

"Kifungu hicho kinaielekeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kuandaa na kuiwasilisha Bungeni kila mwaka Taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya Nchini.

Lengo la Taarifa hii ya Hali ya Dawa za Kulevya ni kuwafahamisha wananchi hali ya tatizo la dawa za kulevya
kitaifa na kimataifa pamoja na jitihada zilizotekelezwa na Serikali katika kukabiliana na tatizo hili ikiwemo ushirikiano uliopo kati ya nchi yetu na nchi nyingine katika kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kupambana na tatizo la dawa za kulevya nchini kwa mujibu wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 pamoja na kufuata miongozo ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC),"amefafanua Waziri Mhagama.

Amesema, bangi imeendelea kuwa ni dawa inayotumika zaidi nchini pamoja na juhudi za Serikali za kutaka kutokomeza matumizi ya dawa hiyo ya kulevya.

Mheshimiwa Waziri Mhagama, amesema mwaka 2022, Serikali ilifanikiwa kuteketeza hekari 179 za mashamba ya bangi na tani 20.58 za dawa hiyo ambazo zilikamatwa katika mwaka huo.

"Aidha, hivi karibuni, kumeibuka tabia ya kuchanganya bangi yenye kiasi kikubwa cha kilevi kwenye vyakula kama vile biskuti, asali, juisi, majani ya chai na keki.

"Tukiangalia Taarifa ya Dunia ya Dawa za Kulevya ya mwaka 2022 utaona kuwa asilimia 40 ya nchi zenye matumizi makubwa ya bangi, zilikumbwa na idadi kubwa ya magonjwa ya afya ya akili, uhalifu na uvunjifu wa amani yaliyosababishwa na matumizi ya dawa hizo.

"Operesheni za ukamataji wa dawa za kulevya nchini kwa mwaka 2022, zilifanikisha kukamata tani 15.2 za mirungi, kilo 254.7 za heroin na kilo 1.7 ya cocaine.

"Kumekuwepo na mwendelezo wa ukamataji wa dawa ya kulevya aina ya methamphetamine ambapo kwa mara ya kwanza mwaka 2021 zilikamatwa kilo 430.8 na kufuatiwa na gramu 968.7 ambazo zilikamatwa mwaka 2022,"amefafanua Waziri Mhagama.

Vilevile, Mheshimiwa Waziri Mhagama amesema mwaka 2022, "tumeshuhudia ukamataji wa dawa nyingine ngeni nchini inayojulikana kama mescaline ambapo gramu 56 zilikamatwa.

"Serikali imefanikiwa kuandaa Mwongozo wa Utoaji Elimu Juu ya Tatizo la Dawa za Kulevya Nchini lengo ni kuhakikisha jamii inapata elimu sahihi juu ya tatizo hili.

"Tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya iliendelea kutolewa ambapo kwa mwaka 2022 jumla ya waraibu 871,010 walinufaika na tiba hiyo nchini.

"Aidha, Serikali imeendelea kufadhili mafunzo ya stadi za kazi kwa waraibu wanaopata nafuu ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea,"ameongeza Mheshimiwa Waziri Mhagama.

Pia amesema, katika kipindi cha mwaka 2022,waraibu 245 waliopata nafuu waliunganishwa katika vyuo vya VETA na DonBosco kwa ajili ya kupapata ujuzi wa kujiajiri ili wasirejee kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

"Mafanikio haya ni matunda ya ushirikiano mkubwa baina ya wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na jamii kwa ujumla. Nawapongeza kwa jitihada hizi,"amesema.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news