Serikali kuanzisha vituo vya huduma vya utengamao kwa waraibu wa dawa za kulevya

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imejipanga kuanzisha vituo vya utengamao ambavyo pia vitakuwa vikitoa mafunzo ya ufundi stadi kwa waraibu wa dawa za kulevya ili kuwasaidia waweze kujikwamua kiuchumi.

Hayo yamebainishwa leo Mei 11, 2023 na Kamishna Jenerali Msaidizi wa Kinga na Huduma za Utangamano kutoka DCEA, Dkt.Cassian Nyandindi wakati akizungumza katika kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Redio jijini Dar es Salaam.

Dkt.Nyandindi amesema, katika vituo hivyo walengwa watakuwa wanapatiwa huduma na mafunzo ambayo yatawapa ufahamu wa kutosha ili waweze kujitegemea.

"Ni maeneo ambayo waraibu wa dawa za kulevya watakuwa wanapatiwa huduma, na kufundishwa masuala ya ujasiriamali,Serikali ilikwishaliona na katika bajeti yetu ya mwaka 2023/2024 tupo kwenye mkakati wa kutengeneza maeneo hayo mawili nchini.

"Kwa hiyo ni suala ambalo Serikali imeliona, Ofisi ya Waziri Mkuu na sisi kama mamlaka tumeliona, na kitu ambacho tayari tumeanza kukifanyia kazi. Kwa hiyo tumuombe tu Mungu bajeti inavyokwenda ili hicho kitu kianze na ninafikiri tunaweza kuanza na mikoa ya Mwanza na Dodoma, kwa hiyo ni kitu ambacho kipo tayari,"amefafanua.

Kamishna Jenerali Msaidizi wa Kinga na Huduma za Utangamano ameendelea kufafanua kuwa, "Na katika mafunzo hayo ni kwamba watafundishwa pia masuala ya ujasiriamali ili waweze kukaa na kujitegemea.".

Wakati huo huo, Dkt.Nyandindi ameendelea kusisitiza kuwa, huduma za tiba ya uraibu wa dawa za kulevya zinapatikana katika hospitali zote za mikoa na wilaya nchini kupitia vitengo vya afya ya akili.

"Lakini suala la pili ni kwamba kama nilivyozungumza awali, huduma za tiba ya uraibu wa dawa za kulevya zinapatikana katika hospitali zote za mikoa na hospitali za wilaya kupitia vitengo vya afya ya akili.

"Huduma hii mara nyingi inapatikana bure, haina gharama, sasa mtu anatakiwa amchukue muhusika ampeleke pale, ila changamoto nyingine ambayo ningependa kuiweka wazi ambayo watu awanapswa kuifahamu mtu anapokuwa ni mrahibu wa dawa za kulevya mara nyingi anakuwa hana tatizo tu la dawa za kulevya.

"Anaweza akawa na tatizo la uraibu wa dawa za kulevya, lakini pia anaweza akawa na matatizo ya magonjwa mengine ambayo yanaambatana na matumizi ya dawa za kulevya, kama vile labda kifua kikuu, muda mwingine, homa ya ini na muda mwingine vidonda.

"Kwa hiyo atakapokuwa anakwenda hospitali wataalamu wa afya mara nyingi hawaangalii tu urahibu wa dawa za kulevya, wataangalia uraibu wa dawa za kulevya, lakini pia wataangalia matatizo mengine ambayo mtu atakuwa nayo, kwa hiyo ushauri ni kwamba wawachukue hao watu wawapeleke vituo vya afya.

"Kama tulivyosema madaktari wawaone waweze kuhudumiwa,lakini pia waweze kujiandaa iwapo kuna matatizo mengine yatajitokeza kwa sababu daktari atamuangalia mgonjwa kila kitu na atatakiwa atibiwe kila kitu na daktari pia ataweza kumpa ushauri.

"Kama ni ushauri wa tiba, kama ni ushauri wa dawa au kama ni rufaa ya kwenda sehemu nyingine kwa ajili ya kutibiwa huo uraibu wake wa dawa za kulevya. Kwa hiyo wananchi wasiogope wazitumie hospitali zetu,na waende ili waweze kupata hizo huduma ambazo zipo tayari,"amefafanua Dkt.Nyandindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news