Serikali kugharamia matibabu ya majeruhi na mazishi ya wananfunzi ajali ya Bahi

NA MWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule amesema Serikali itagharamia mazishi ya wanafunzi wawili wa shule ya Sekondari Mpalanga wilayani Bahi waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea Mei 11, 2023 majira ya saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Chidilo wilayani humo.
Aidha, Mhe. Senyamule ameahidi kuwa, Serikali itagharamia matibabu ya wanafunzi wote majeruhi 31 walioumia katika ajali hiyo ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Ajali hiyo imehusisha gari yenye namba za usajili T 519 BSY aina ya Mitsubishi Canter mali ya Bw. Abdul Rashid mkazi wa Dar es Salaam.

Gari hiyo ilikuwa imebeba wanafunzi 51, walimu wawili na dereva mmoja ambao walikuwa wakielekea Shule ya Sekondari Magaga kushiriki mashindano ya michezo ya UMISETA.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Bahi, ASP Bakari Ramadhani amesema kuwa, chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo lililobeba wanafunzi, uliosababisha gari kumshinda dereva, kuacha njia na kupinduka na hadi sasa dereva wa gari hiyo anashikiliwa na jeshi la polisi.

Akitoa salamu za Serikali Mhe. Senyamule amewataka wafiwa kuwa na moyo wa subra na kuelekeza Jeshi la Polisi kuchukua hatua haraka kwa wote watakaothibitika kuhusika na uzembe kwa namna yoyote ile.

"Ndugu zangu nawapa pole kwa niaba ya Mhe. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tumeguswa sana na misiba hii ya kupoteza nguvu kazi ya Taifa la leo na kesho. Serikali iko pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu, tutaendelea kushirikia katika wakati huu wa msiba kwa kusimamia mazishi ya marehemu na matibabu ya majeruhi wetu. Viongozi wote wakuu pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa ana Serikali za Mitaa (TAMISEMI) mwenye dhamana ya kusimamia Shule na Michezo mashuleni wanatoa pole sana,”amesisitiza Mhe. Senyamule.

Awali Mhe. Senyamule amepata fursa ya kuwatembelea majeruhi 31 wanaoendelea na matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma huku Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo Dkt. Ernest Ibenzi akithibitisha kuendelea kuimarika kwa afya za majeruhi hao.

Pia, Mkuu wa Mkoa amepata fursa ya kutembelea familia zilizopatwa na misiba hiyo katika Kijiji cha Nholi na Chidilo. Waliofariki duniani ni Magreth Juma Shimba (18) mwanafunzi wa Kidato cha Nne ambaye anatarajiwa kusafirishwa kesho kuelekea Wilaya ya Kishapu, Shinyanga na Neema Yohana Hoya (16) mwanafunzi wa kidato cha pili atakayezikwa kesho Kijiji cha Chidilo, Wilayani Bahi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news