SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-22

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...haiwezekani mtu umweke ndani halafu apotee kiaina aina ndani ya mahabusu, mkuu huyo wa kituo alikosa la kujitetea mbele ya mabosi wake.

Endelea

Baada ya mtoto huyo kuingizwa mahabusu aliwakuta watuhumiwa kumi na tano. Watuhumiwa hao walikuwa wameshapata taarifa za miujiza aliyokuwa akiifanya mtoto huyo, walimkaribisha kwa upendo ndani ya mahabusu hiyo.

Kila mmoja alieleza tuhuma zilizosababisha kuwekwa mahabusu humo, asilimia kubwa tuhuma zao ilikuwa uuzaji wa bangi na ukwapuaji wa fedha.

Wapo pia waliotuhumiwa kwa utekaji wa magari pamoja na kujihusisha na ujambazi, wengine walikuwa na tuhuma za wizi wa kuku, kudhulumiana fedha pamoja na kupigana.

Katika kundi hilo mtoto huyo alivutiwa na watuhumiwa watano. Mtuhumiwa wa kwanza aliitwa Shing'weng'we, yeye alikuwa na tuhuma ya ujambazi wa kutumia silaha.

Mtuhumiwa wa pili aliitwa Malale, yeye alituhumiwa kwa ukataji mapanga vikongwe kwa imani za kishirikina. Mtuhumiwa wa tatu aliitwa Masangu, yeye alituhumiwa kwa utekaji wa magari na kuwanyang'anya watu mali zao kwa nguvu.

Mtuhumiwa wa nne aliitwa Makoye, huyu alikuwa nduguye Masangu na wote walishirikiana katika utekaji wa magari. Mtuhumiwa wa tano aliitwa Ndama, yeye alituhumiwa kwa uuzaji wa bangi na dawa za kulevya.

Mtoto THE BOMBOM alivutiwa kwa kiasi kikubwa na watu hao, aliwateua kuwa walinzi wake kila alipokuwa akienda walipaswa kuambatana naye.

Mahali pekee ambapo hawakupaswa kufuatana naye ni katika shughuli zake za uchawi, bahati nzuri walinzi hao hawakumfahamu kiundani mtoto huyo.

Watuhumiwa wengine kumi waliosalia aliwabadili maumbo yao na kuwa sisimizi, waliutumia muda huo kutoka mahabusu kisha wakapita kwenye kundi la watu waliokuwa nje pasipo kuonekana na kutokomea mbali.

Wakiwa mbali na mazingira hayo kila mmoja alianza kurudia umbo lake halisi, muujiza huo uliwavutia watu hao kumi na kulitukuza jina la mungu wa mtoto huyo. Akautumia muda huo kutoroka na wale walinzi watano, wakati huo wote walikuwa wameshasilimu na kuachana na imani zao.

Aliwabadili katika umbo la upepo kisha wakautumia muda huo kutoka mahabusu, kule nje walikutana na gari la mkuu wa wilaya, mkurugenzi na kamanda wa polisi wilaya wakipaki gari lao.

Mtoto huyo akiambatana na walinzi wake walipita katikati yao na kutokomea mlimani pasipo kuonekana.Kule mlimani walikaa siku tano akiwafundisha miiko mbalimbali katika imani yake, aliwafundisha pia namna ya kuzungumza na watu na mambo mbalimbali.

Jambo jingine alilowafanyia ilikuwa na kuwanywesha madawa mbalimbali ya kuwafanya kuwa waaminifu kwake siku zote. Siku zote tano walinzi walikula chakula kizuri pasipo kukipika mlimani hapo.

Kila mlinzi aliletewa chakula alichokuwa akitamani kula siku hiyo pasipo hata kumueleza mtoto huyo, jambo hilo liliwaongezea imani juu yake na kumuona kuwa mtoto huyo alikuwa ni nabii wa kweli.

Kila siku wakati wa usiku mtoto huyo aliwatoroka na kwenda kambini kwao kuendelea na shughuli za kichawi. Kwa kuwa hakutaka wajue shughuli zake, kabla ya kuondoka alihakikisha walinzi hao wameghubikwa na lindi la usingizi mzito mpaka atakaporudi.

Ndugu msomaji unapaswa kutambua kuwa, kila alichokuwa akikifanya mtoto huyo kilikuwa ni mpango mzima wa kambi yao ya kichawi.

Hakuna jambo lililofanyika pasipo mpango maalum, haya yalikuwa ni maandalizi ya KANISA LA KICHAWI ambalo walikubaliana liitwe SURVIVE FROM THE DEATH.

Kulingana na uwezo wa madawa aliyokuwa nayo mtoto huyo, kambi nzima ilikuwa ikimuunga mkono juu ya ujenzi wa kanisa hilo.

Hata hivyo, kutabiriwa kwa mtoto huyo miaka mingi iliyopita kuliwaongezea imani wachawi hao juu ya mtoto huyo. Tayari walikuwa wameshaonja faida za mtoto huyo, huyu ndiye aliyechangia kufanikisha kukamatwa kwa hasimu wao Mkuu Padri Samson.

Siku tano za mafunzo ya kanuni za imani ya kanisa la mtoto huyo zilitamatika haraka, walinzi hao walikuwa wamevutiwa sana na imani hiyo.

Miujiza mingi aliyoionesha mtoto huyo wangali mlimani ilikuwa ni ushahidi tosha wa unabii wa mtoto huyo.Alibadili mawe kuwa vitanda vya kisasa, alibadili majani yakawa godoro. Alibadili upepo kuwa maji, pia alibadili pilipili zikawa kalimati au bagia.

Katika mafundisho yake walihudhuria wanyama wa kila aina, hata viumbe wa ajabu walihudhuria pia. Viumbe wa kutisha kama mazimwi yalikuwepo pamoja na majini walikaa pamoja na kumsikiliza mtoto huyo akifundisha habari njema.

Itoshe kusema tu kuwa, mtoto huyo alikuwa na nguvu za ajabu alizozipata toka kwa muumba wake. Nguvu hizo ndizo ziliwatisha wazungu hivyo kuanza mipango ya kumpoteza haraka.

Kwa kuwa mafunzo hayo yalikuwa ni ya siku tano ilipofika siku ya tano waliondoka. Siku zote imani za kiafrika huzingatia mzunguko yaani mduara, kwa kuwa walikuwa watano hivyo siku za mafunzo zilipaswa kuwa tano ili kukamilisha mduara.

Ndugu msomaji unadhani kwa nini nyumba halisi za kiafrika ni za duara? Viti vya vya kiafrika ni vya duara? Uso wa duara? Ungo wa duara? Makalio ya duara? Matiti ya duara? Kwa nini walizika watu kwa kaburi la duara? Ipo nguvu kubwa sana katika mzunguko huu wa duara, hii nitaisimulia katika kisa kingine.

Basi tuendelee na kisa chetu, mtoto huyo alishuka mlimani akiambatana na walinzi wake, walipofika kijijini walianza kufuatwa na kundi la watu.

Watu hao walikuwa wameshasikia miujiza aliyokuwa akiifanya mtoto huyo, kila walipopita watu walimfuata huku wakiwa na imani kuu juu yake.

Kila mmoja alimfuata mtoto huyo akiwa na shida zake, wapo waliotaka kushuhudia miujiza, wengine walitaka kuponywa magonjwa, baadhi walitaka utajiri.

Wakiwa njiani wakielekea Jineli ya Ilongo, walikutana na bibi kizee aliyekuwa akimsukuma mjukuu wake kwa baiskel ya maalumu aliyekuwa kapooza.

Bibi yule alijitahidi kumsogelea mtoto huyo, lakini hakufanikiwa kulingana na idadi kubwa ya watu. Hata hivyo hakukata tamaa, mbali ya kutokuwa na nguvu za kuisukuma baiskeli hiyo aliendelea kujaribu tena na tena.

Katika harakati za kutaka kumsogelea nabii mtoto THE BOMBOM, hatimaye akawa amefanikiwa. Ghafla mtoto huyo nabii alisimama na kumfuata bibi huyo na mgonjwa wake. Watu walikuwa wengi kama mchanga wa baharini, hakukuwa na sehemu hata ya kutemea mate.

Mtoto huyo aliyekuwa kapooza alikuwa wa kike, nabii mtoto THE BOMBOM alipomkaribia mgonjwa huyo alimshika paji la uso kisha akazungumza kitu.

Ghafla mtoto huyo alisimama na kurukaruka, watu wakashuhudia miujiza mingine ya kwanza baada ya siku tano za kutoonekana kwa nabii huyo.

Bibi kizee huyo na mjukuu wake walichukua kiti mwendo chao na kuondoka wakiwa wanatembea kwa miguu yao. Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji si watu wote waliopooza majumbani ni binadamu. Wengine siyo binadamu wa kweli, yamkini ni nyani, msukule au mbwa katika umbile na picha ya binadamu halisi.

Kuna muda wachawi huwachukua watu halisi na kuwabadilishia viumbe vya ajabu, ndugu yako anaweza kuchukuliwa kichawi kisha ukawekwa nyani aliye na picha ya ndugu yako.

Kinachofanyika hapa huwa ni hiki, kama wamepanga kumchukua mwanaume ndani ya familia huwa wanaleta mzozo ndani ya familia husika.

Mzozo huo huchochewa na dawa ambazo wanakuwa wamemwaga kwenye mji huo. Kelele za mara kwa mara na ugomvi usioisha katika familia hiyo hufanyika, majirani lazima watatambua kisha makosa huelekezwa kwa yule asiyetakiwa na wachawi.

Wachawi hutumia muda huo kumchukua mlengwa na kuwawekea kiumbe yeyote anayeonekana kupooza. Majirani watatangaza kuwa chanzo cha kupooza kwa mtu huyo ni kelele zilizosababishwa nyumbani kwake, wengi huamini hivyo kumbe aliyepo siyo binadamu halisi.

Pia ipo njia nyingine ambayo hutumiwa na wachawi kumchukua mtu na kuwawekea kiumbe kingine kilichopooza. Njia hiyo ni kupitia ajali, ndani ya ajari hiyo wanamchukua mlengwa kisha wanaweka kiumbe kilichopooza.

Ndugu na jamaa huamini ndugu yao amepooza kutokana na ajari , kumbe wanahangaika na nyani aliyewekwa kwa malengo fulani.

Zipo njia nyingi sana zinazotumiwa na wachawi katika kuweka kiumbe kilichopooza. Jambo la msingi kuweza kuwatofautisha kati ya mtu halisi aliyepooza na kiumbe aliyewekwa na wachawi kwa lengo la kuwazubaisha.

Mosi, kiumbe aliyewekwa na wachawi badala ya mtu halisi huwa hana kumbukumbu, ukienda kumtembelea hawezi kukukumbuka hata kidogo.

Kiumbe aliyewekwa yeye muda wote huwa ameinama huku mdomo wake ukiwa umepinda, hapendi mawasiliano ya mara kwa mara kuhofia kubainika.

Kuna kipindi huwa anaugua sana magonjwa mbalimbali ili familia mtumie fedha nyingi kumhudumia. Muda mwingi hutokwa na ukonda mdomoni, hupendelea sana kulala muda mwingi huku akiwa hapendi kukaa na watu.

Ukiona dalili hizo chungumza kwa makini yamkini mgonjwa wako hajapooza bali unahangaika na kiumbe kingine. Baada ya miujiza hiyo mtoto THE BOMBOM aliendelea na safari yake, walinzi wake walikuwa wamemuweka katikati hivyo hakuna mtu aliyemsogelea.

Hatimaye walifika kwenye kwenye eneo la wazi la Jineri hiyo, ndugu msomaji ninaposema Jineri ni kiwanda kidogo cha kubangua pamba na mbegu zake.

Pia kiwanda hicho hutumika kufunga marobota ya pamba na kukamua mafuta ya kula yanayotokana na mbegu za pamba.

Katika kiwanda hicho kulikuwa na eneo la wazi, eneo hilo lilikuwa na uwezo wa kuchukua watu zaidi ya elfu kumi. Watu walikuwa wakitiririka eneo hilo mithili ya chemichemi za bahari, wakati huo ilikuwa ni muda wa saa tano asubuhi.

Watu waliofika walielekezwa eneo la kukaa, eneo la katikati la kiwanja hicho walizuiwa kuingia. Pia kila pembe ya kiwanja hicho iliachwa njia ya kuwaruhusu watu kuingia, kwa namna hiyo kulikuwa na njia nne za kuingia uwanjani paliozuiliwa watu kuingia.

Mtoto THE BOMBOM, alikwenda kusimama katikati ya kiwanja kisha akapiga makofi matatu, baada ya muda mchana ukamezwa na giza.

Pakawa na giza totoro kiasi kwamba hakuna mtu aliyeweza kumuona mwenzie, fisi walianza kuunguruma mapangoni. Bundi na wadudu wengine walitoka sehemu za maficho na kuendelea na shughuli zao.

Hali hii iliendelea kwa muda wa dakika ishirini kisha ukarudia mwanga. Watu wote walipigwa na butwaa kwa maajabu hayo aliyokuwa akiyaonesha mtoto huyo.

Baada ya hapo alipiga miruzi mitatu tena, ghafla walionekana wachawi wakiwa kwenye fisi wakija eneo hilo.Kulikuwa na idadi kubwa ya wachawi waliokuja eneo hilo, baadhi walikuwa kwenye nyungo huku wengine wakiwa kwa miguu.

Waliendelea kumiminika uwanjani hapo wakiwa katika mavazi ya kichawi, mluzi ule alikuwa amewaita wachawi wote wa eneo hilo.Ndugu msomaji kumbuka wachawi hao hawakuhusiana na kambi ya kichawi ya mtoto THE BOMBOM.

Hawa ni wale masalia ya wafuasi wa Ng'wana Michembe pamoja na Padri Samson, hawa ndiyo walioleta kimbunga kipindi mtoto huyo alipotaka kumfufua Mchungaji wa Shika Maneno Tenda Maneno.

Kwa kuwa walikuwa wenyeji wa kijiji hicho na maeneo ya jirani walifahamika kwa urahisi, waliendelea kumiminika kila baada ya muda.

Hali ilitisha sana eneo hilo, nguvu za mtoto huyo ambaye alijiita nabii ilikuwa ikitamalaki eneo hilo. Makutano walibaki wakishangaa miujiza hiyo iliyofanywa na nabii wa mungu, wachawi waliendelea kumiminika, kumiminika, kumiminika.

Ndugu msomaji mambo yanaendelea kutakata, tayari mtoto THE BOMBOM amefanya miujiza mingine siku ya kwanza baada ya kurejea kijijini toka mlimani. Unadhani nini kitampata mtoto huyo? Hebu ungana nami sehemu inayofuata.

MIDIMU!!!

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news