SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-24

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia... alizungumza maneno machache kisha akaviweka chini vyakakula hivyo. Ghafla boksi hilo lilianza kuongezeka ukubwa wa umbo na vyakula vikaongezeka.

Endelea

Vyakula hivyo vilianza kusambazwa kwa makutano wote waliokuwa eneo hilo, kila mtu alichukua chakula na kinywaji cha kutosha.

Jambo lililoshangaza, kila chakula kilivyokuwa kikichukuliwa kwenye boksi hilo kiliendelea kuongezeka. Watu elfu kumi na mbili walikula chakula hicho na kusaza.

Jambo jingine lililoshangaza ilikuwa ni utamu wa mikate, biskuti na soda hizo. Ilikuwa mitamu kuliko maelezo. Chakula hicho kilikuwa kinaletwa na majini waliokuwa wakikichukua eneo fulani kwenye mabohari makubwa huko India, yasemekana majini hao walikiiba bara Hindi na kuileta eneo hilo.

Kwa asili majini wana uwezo wa kusafiri kwa kasi zaidi duniani, wana uwezo wa kutumia sekunde chache kufika eneo lolote la dunia.

Majini hao walimtii mtoto huyo kama nabii wao. Kwa kuwa ni vigumu kuwaona kwa macho ya kawaida, mara nyingi katika safari za mtoto huyo aliambatana nao.

Baada ya chakula mtoto huyo alianza kuwafundisha makutano mambo mbalimbali. Alianza kwa kuwaelimisha juu ya umuhimu wa majina ya asili, alieleza kuwa watu wameacha majina ya babu zao na kufuata majina ya kigeni.

Hakuna mawasiliano mema kati ya wahenga na watu walio hai wenye majina ya watu weupe. Alisema kuwa mtu anapokufa kabisa roho yake huendelea kuwa hai, kuna muda huja kuwatembelea watu wa ukoo wake na kuwabariki.
Roho hiyo inapokuta mtu huyo ana jina la watu weupe waliowatendea vibaya mababu zetu, huwa haitoi msaada kwa mtu huyo maana ameikataa asili yake.

Mtoto huyo pia alielezea kwa kina namna huko mwanzo mababu zetu walivyolazimishwa kubadili majina yao na kupokea majina ya kitumwa ya watu weupe.

Alieleza unyama waliofanyiwa mababu na mabibi zetu na watu weupe kipindi cha majilio yao Afrika. Alieleza namna mababu zetu walivyoingiliwa kinyume cha maumbile na watu weupe kipindi cha majilio yao Afrika.

Alifafanua kwa kina namna bibi zetu walivyobakwa na kulawitiwa na washenzi hao. Makutano walikuwa kimya huku wengine wakitokwa na machozi, wakiendelea kumsikiliza mtoto huyo nabii.

Alielezea namna dini za watu weupe zilivyohusika katika kuwafanya watumwa watu weusi. Alifafanua biashara ya binadamu iliyofanywa na watu weupe walipokuwa wakieneza dini zao Afrika.

Alifafanua namna walivyowindwa mithili ya wanyama majumbani kwao na kuuzwa kama bidhaa. Alieleza namna watu hao walivyotumia dini zao kuisambaratisha Kemet nchi ya ahadi ya Mwafrika.

Aliwaeleza makutano kuwa kuendelea kutumia majina ya watu waliowalawiti babu na kuwabaka mabibi zetu ni kuunga mkono unyama waliofanyiwa.

Kila mmoja katika makutano hayo alijawa na hasira juu ya unyama huo, wengi walibadili majina yao na kufuata majina ya asili.

Mafundisho hayo yalitamatika muda wa saa tano usiku, kila mmoja aliamua kujipumzisha ili kusubiri siku inayofuata. Wakati makutano hao wamelala mtoto huyo aliondoka eneo hilo na kwenda kambini kwake.

Kule kambini alipokelewa kwa shangwe kuu na kundi lake la wachawi, siku hiyo kulikuwa na kundi la wachawi kutoka Kongo waliokuja kumuona nabii mtoto THE BOMBOM.

Kundi hilo ni miongoni mwa makundi yaliyokuwa yakisubiria kutimizwa kwa unabii, unabii uliodumu kwa muda wa miaka dahari.

Mara baada ya kufika kambini hapo, wachawi hao walimuendea na kusujudu mbele yake. Baada ya hapo alizungumza nao mambo mbalimbali juu ya shughuli za kichawi, aliwapa njia mbalimbali za kutatua changamoto walizokuwa wakipitia.

Baada ya hapo alichukua kibuyu kisha akatemea mate ndani yake, akachukua kibuyu kingine na kumimina mchanga aliokuwa ameukanyaga.

Aliwapa maagizo ya kuchanganya dawa zao na mchanga huo pamoja na mate yake. Baada ya hapo majadiliano yalikuwa mengi, wachawi hao wakaomba angalau kushirikiana naye siku mbili kwenye shughuli alizokuwa akifanya wakakubaliwa.

Usiku wa manane mtoto huyo alirudi na kundi la wachawi wa Kikongomani, aliwakuta makutano wakiwa kwenye lepe la usingizi.

Wale wachawi walijumuika na makutano, ilikuwa vigumu kwa makutano kutambuana kila mmoja eneo hilo hata kama wangeliwakuta macho.

Asubuhi yake waliendelea na safari yao, njiani aliendelea kufanya miujiza mingi. Aliwaponya wagonjwa kwa nguvu ya giza japo watu walikubali ni kwa nguvu za mungu.

Walivuka mji wa Bundilya, Lugeya na Nyanguge ilipofika saa tano asubuhi walikuwa mji wa Ihayaboyaga kata ya Bukandwe. Walipofika mji mdogo wa Njicha waliamua kupumzika,watu walikuwa wengi mithili ya mbegu za ufuta kwenye kitalu.

Kwenye msafara wa mamba hata kenge hawakosekani, usemi huu una ukweli ndani yake. Ndugu msomaji katika makutano hao watu wengine walikuwa na shughuli zao.

Wapo waliokuwa wakifanya biashara ya mchanga alipokanyaga nabii mtoto THE BOMBOM, mchanga huo walikuwa wakiwauzia watu wa kada mbalimbali.

Kwa upande wa wafanyabiashara waliuweka mchanga huo mahali pa biashara zao, yasemekana biashara zao ziliongezeka mara dufu.

Kwa upande wa wafanyakazi, wao waliusaga mchanga huo na kuwa vumbi ambayo walijipaka mwilini kipindi walipokuwa wakienda kazini.

Kwa wafugaji na wakulima mchanga huo waliuweka zizini au shambani, jambo lililopelekea mifugo au mazao yao kustawi vizuri zaidi.

Kama ilivyo kawaida kwa wanasiasa kutopitwa na jambo, wao waliutumia mchanga huo katika siasa zao ili kukubalika zaidi. Katika msafara huo pia kulikuwa na wezi na watu wa karba mbalimbali kama vile wachawi , wagonjwa, wenye matatizo binafsi nk.

Baada ya mapumziko ya kutosha mtoto THE BOMBOM aliendelea na safari yake. Ilipotimia saa kumi na mbili jioni walikuwa wamefika eneo husika yaani mji wa Kanyama.

Eneo lenyewe lilikuwa zuri hakuna mfano, kwa upande wa Magharibi mji huo ulipakana na mji wa Kisesa, kwa upande wa Mashariki ulipakana na mji wa Nyamhongolo.

Kwa upande wa Kusini ulipakana na mji wa Kishiri na kwa upande wa Kaskazini mji huo ulipakana na mji wa Busekwa.

Mji huo ulikuwa na kijimlima cha wastani chanye mandhari ya kuvutia, kijimlima hicho hakikuwa na miti bali nyasi fupi za ukoka zilizosambaa eneo zima mithili ya nywele za mwanamwali wa Kiafrika.

Kijiupepo baridi chenye mchanganyika wa harufu ya maua safi kilitamalaki eneo zima, hakika mandhari yalikuwa mazuri zaidi ya yale ya mji wa Kapilanaumu au Gethaman.

Eneo la chini ya kijimlima hicho upande wa Kusini kulikuwa na mto uliokuwa ukitiririsha maji yake safi Ziwa Nyanza, japo wengi huliita kwa jina la kitumwa yaani Victoria.

Mto huo ulivutia kuutazama kwa namna ulivyokuwa umejikunjakunja mfano wa mito ya mbinguni, maji yake ya buluu yalimfanya mtu kuhisi yupo mawinguni au peponi kadri alivyoutazama mto huo.

Hakika ulikuwa mto mzuri wenye kumvutia mtu yeyote ambaye angelipita eneo hilo, ni uhuni wa watu weupe kutouweka kwenye maajabu saba ya ulimwengu.

Ndege jamii ya solodi,punze, jiji nkwemba na balwe walionekana kwa wingi katika mto huo, wataalamu wa maliasili wanasema kuwa ndege wa jamii hiyo wanapatikana Tanzania ni eneo hilo tu duniani.

Wenyeji wa eneo hilo husema mara moja moja nyakati za usiku hasa saa saba, mlima huo huzingirwa na watu wenye mabawa waliovaa nguo nyeupe.

Huonekana wakiomba kwa utukufu huku wakilisifu jina la mungu, yamkini mlima huo uliandaliwa maalumu kutimiza unabii wa mtoto THE BOMBOM.

Kwa upande wa Mgaharibi wa kijimlima hicho, kulikuwa na miti ya matunda iliyokuwa imepandwa kwa ustadi wa hali ya juu.

Kulikuwa na miti ya mihama, sungwi, miso ga nh'olo, mikoma, makamelwa nk , wengine husema yamkini bustani ya kwanza ilikuwa ni eneo hilo.

Mawingu yaliyopita karibu na kijimlima hicho yaliongeza uzuri wa eneo , yalilipamba eneo hilo na kuonekana kama paradiso

Ndugu msomaji mambo yanaanza kuiva,makutano wamefika kwenye mji wa ahadi wa nabii mtoto THE BOMBOM. Unadhani nini kitaendelea kwenye simulizi hii sehemu inayofuata? Ungana nami sehemu inayofuata.

KINEHEYI MAMI?

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news