TANZANIA,BORA KUISHANGILIA-2:Twapendwa na Maanani

NA LWAGA MWAMBANDE

KATIKA chapisho lililopita tuliangazia kwa kina kuhusu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na namna ambavyo kimeendelea kuwa tegemeo kubwa ndani na nje ya nchi kuzalisha wasomi na kutafiti masuala mbalimbali kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

UDSM ni sehemu au taasisi inayochukua asilimia ndogo sana katika eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini ina umuhimu mkubwa zaidi.
Mawe mawili ya vito ya Tanzanite ambayo yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kupatikana nchini. (Picha na Wizara ya Madini Tanzania/Reuters).

Tanzania ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki ndani ya ukanda wa maziwa makuu ya Afrika. Imepakana na Uganda na Kenya upande wa Kaskazini, Bahari Hindi upande wa Mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda upande wa Magharibi.

Eneo lina kilometa za mraba 947,303.Tanzania ni nchi ya 13 barani Afrika na ya 31 kwa ukubwa duniani, ikiorodheshwa kati ya Misri kubwa na Nigeria ndogo. Maji ya ndani yanachukua asilimia 6.2. Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika, upo Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Idadi ya watu kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2022 ilikuwa 61,741,120 (nchi ya 24 duniani) kutoka 44,928,923 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2012, likiwa ni ongezeko la asilimia 3.2 kwa mwaka.

Aidha, kwa ukubwa huo na upekee wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anaendelea kukupitisha katika mambo na miji tofauti ili uweze kuona namna ambavyo Mungu alivyoiheshimisha nchi hii kupitia rasilimali mbalimbali ambazo zina upekee duniani. Endelea;


1. Nzuri yetu Tanzania,
Bora kuishangilia,
Vitu vyote vya dunia,
Vyapatikana nchini.

2. Bora kuwakubalia,
Wale wanatuambia,
Kwamba sisi Tanzania,
Twapendwa na Maanani.

3. Baridi ikiingia,
Mavuno twajivunia,
Hata kwenye joto pia,
Tunavuna mashambani.

4. Matunda mengi sikia,
Tunakula Tanzania,
Kote utakopitia,
Yamejazia sokoni.

5. Vyakula vya asilia,
Vingi tunavitumia,
Kitaka fuatilia,
Utaona mashambani.

6. Madini ya Tanzania,
Yote utayasikia,
Changamoto kutumia,
Kwa faida yetu ndani.

7. Vile tunajichimbia,
Wageni kuwauzia,
Bila kujichakatia,
Tunapata bei duni.

8. Jitihada fagilia,
Thamani kuyajazia,
Ajira twajipatia,
Tukichakata nchini.

9. Dhahabu tumeanzia,
Tuweze kujitunzia,
Kwingine tukitumia,
Tutafaidi madini.

10. Misitu ya asilia,
Mingi tunajivunia,
Mahitaji yenye nia,
Twajipatia nchini.

11. Mbao twajichakatia,
Bidhaa twajiuzia,
Nje zinapofikia,
Hizo fedha za kigeni.

12. Kiswahili nakwambia,
Zao tunalikalia,
Kwa jinsi kinavutia,
Kote hapa duniani.

13. Hapa kwetu Tanzania,
Kote tunakisikia,
Nchi nyingi nakwambia,
Waswahili washeheni.

14. Ni bora tukatumia,
Utajiri Tanzania,
Tuweze kujipatia,
Fedha nyingi za kigeni.

15. Mengine yakififia,
Yale yasiyovutia,
Hii yetu Tanzania,
Itapaa mawinguni.

16. Mungu twamshangilia,
Makubwa katupatia,
Kutugea Tanzania,
Maziwa asali ndani.

17. Twatamani kufikia,
Maisha ya kuringia,
Ili yetu Tanzania,
Iwe juu kileleni.

18. Ni tajiri Tanzania,
Tukiamua tulia,
Yetu tukajifanyia,
Kwa ustawi nchini.

19. Hapa mwanzo naanzia,
Mengi nitakutajia,
Yale tunajivunia,
Ukitembea nchini.

20. Mikoa taisikia,
Mali zilivyojazia,
Na watu nitagusia,
Ni mashuhuri nchini.

21. Yalivyomengi sikia,
Ninapitiapitia,
Lako usiposikia,
Siniweke kitanzini.

22. Hata watu Tanzania,
Maarufu wazidia,
Nyanja nyingi wajazia,
Waweza fika mbinguni.

23. Wale nitakutajia,
Ni njia nimepitia,
Nawe tanikubalia,
Wana mchango nchini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news