Vijiji vinavyozunguka hifadhi kunufaika na miradi ya ujirani mwema

NA FRESHA KINASA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaanza kutoa miradi mbalimbali ya ujirani mwema kwa vijiji ambavyo vinazunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na hifadhi mbalimbali ambavyo wananchi wake wanashiriki vyema katika kupambana na vitendo vya ujangili, na uwindaji haramu wa wanyama mapori.
Hatua hiyo inalenga kuwafanya wananchi wanaopakana na maeneo ya hifadhi wawe mstari wa mbele kuhakikisha wanashiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za serikali katika kutokomeza vitendo vya ujangili ambavyo ni kinyume cha sheria. 

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Mary Masanja wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa vijiji saba vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.
Mkutano huo umefanyika katika Kijiji cha Bisarara Kata ya Sedeco na kuhudhuriwa pia na ananchi kutoka vijiji vya Bonchugu, Nyamburi, Bisarara, machochwe, Merenga Nyamakendo mbalibali. 

Mkutano huo, ulihusisha mawaziri watatu wa Kisekta akiwemo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mheshimiwa, Dkt. Angeline Mabula, Waziri wa OR-TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mary Masanja pamoja na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee. 
Mawaziri hao,wamefanya ziara ya kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili Wananchi wanaopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kutoa ufafanuzi wa changamoto mbalimbali kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa aliyoyatoa hivi karibuni Bungeni jijini Dodoma.

Mheshimiwa Masanja amesema kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona hifadhi zinatunzwa na kulindwa kwa manufaa endelevu ya vizazi vijavyo. Hivyo wananchi wawe sehemu ya kuunga mkono juhudi hizo kwa kutokiuka sheria ikiwemo kuingiza mifugo katika maeneo hayo na kufanya uwindaji haramu. 

Kuhusiana na mifugo ambayo hukamatwa na kutaifishwa na Serikali inapoingia maeneo ya Hifadhi, Mheshimiwa Masanja amesema mifugo hiyo hukamatwa na kupelekwa mahakamani kwenye chombo ambacho hutafsiri sheria na hivyo wananchi wanapaswa kutoilalamikia TANAPA kuhusika na kutaifisha mifugo na njia pekee ni kuheshimu sheria kwani imeweka katazo. 
Naye Marwa Ryoba Chacha aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mkoani Mara, ameiomba Serikali kuangalia upya sheria ya kutaifisha mifugo kwani imekuwa ikiwafanya Wananchi kuwa maskini kutokana na mifugo yao kukamatwa na kutaifishwa. 

"Naiomba serikali, kubadilisha hii sheria ya kukamata mifugo na kuitaifisha imewafanya Wananchi wengi kuwa maskini kabisa hata kusomesha wanashindwa. Kwani gharama pia zinazotozwa Kama faini pindi mfugo unapoingia hifadhini ni kubwa,"amesema Marwa Ryoba Chacha.
Pia, ameiomba Serikali kujenga fensi katika maeneo yanayopakana na hifadhi kudhibiti wanyama wasitoke katika maeneo yao kuvamia mashamba na kuharibu mazao yao na pia kuhatarisha usalama wa wananchi wanaopakana na hifadhi. Ombalo ambalo Naibu Waziri Masanja amesema amelichukua. 

Naye Mbunge wa Jimbo la Serengeti Mlimi Amsabi amesema kuwa hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapaswa kuendelea kuongeza manufaa kwa Wananchi ikiwemo kuwapa ajira vijana waliomaliza mafunzo ya jeshi la akina sambamba na serikali kuongeza kifuta jasho ambacho hupewa Wananchi kufuatia uharibifu ambao hufanywa na wanyama pori hasa tembo wanapoharibu mazao. 
Kwa upande wake Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amesema serikali inatarajia kutengeneza Mpango wa Matumizi bora ya Ardhi kwa Vijiji saba vya Wilaya ya Serengeti ambavyo vinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mara baada ya suala lililoko Mahakamani kuisha.

“Serikali inasubiri suala lililoko Mahakamani dhidi ya vijiji na Tanapa likiisha tutatekeleza mpango huo kupitia Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata hati za kimila ambazo zina hadhi ya kuwawezesha kunufaika kiuchumi kupitia ardhi yao na wakati ukifika wananchi mjitokeze kutoa ushirikiano kwa wataalam, "amesema Waziri Dkt.Mabula.
Kwa upande wake Waziri wa OR-TAMISEMI, Angellah Kairuki amewataka wananchi na Watanzania kwa ujumla kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanya na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na pia akawahimiza kufuata sheria za nchi kuepuka migogoro ambayo inarudisha nyuma maendeleo.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amesema kuwa, maendeleo ya Mkoa wa Mara yanategemea sana ushirikiano mzuri baina ya viongozi pamoja na wananchi na hivyo amesistiza uwajibikaji wenye tija kwa kila mmoja kwa nafasi aliyonayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news