Waziri Dkt.Mabula ataka madalali wenye weledi, staha

NA MUNIR SHEMWETA
WANMM 

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula ameitaka Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kuhakikisha madalali wanaoteuliwa wanapata mafunzo na wenye weledi wanaoweza kufanya kazi kwa staha. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya (hawapo pichani) Mei 16, 2023 ilipomtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga.

Dkt.Mabula ameyasema hayo Mei 16,2023 alipokutana na Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi, Nyumba na Wilaya ilipokwenda kumtembelea ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma. 

Kamati hiyo ambayo iko chini ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliundwa Desemba 27, 2021 kwa mujibu wa wa kifungu cha 2&3 cha sheria ya Mahakama za migogoro ya ardhi sura 216. 

"Ni vizuri madalali mtakaowateua waonekane ni wale waliopata mafunzo na wenye weledi na wanaoweza kufanya kazi kwa staha, hilo nalo ni zuri zaidi," amesema Dkt. Mabula. 
Baadhi ya Wakuu wa idara wa wizara ya ardhi wakiwa pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya wakiwa katika kikao na Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula jijini Dodoma.

"Unaenda kutekeleza amri ya mahakama halafu unachukua vitu unarusha huko hiyo hapana, tunatambua ni amri ya mahakama lakini basi ifanyike kwa staha siyo kujivurugia kwa sababu ni dalali, tusingependa kuingia kwenye historia ya kuanza na madalali walioteuliwa kwa kanuni mpya na kupigiwa kelele,"amesema Dkt.Mabula. 

Aidha, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ametaka madalali walio na leseni za utekelezaji kutoenda moja kwa moja kwenye tukio bila kupita ofisi za utawala wa eneo husika na kutaka madalali wakati wa utekelezaji kupita kwa Mkuu wa Mkoa, Wilaya au Afisa Tarafa kutegemeana na utaratibu utakaowekwa ili kazi ifanyike na baraka za utawala. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akifuatilia mchango wa mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na nyumba ya wilaya (hayupo pichani) alipokutana nao jijini Dodoma. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga.

"Kumekuwa na changamoto hiyo mara nyingi sana, dalali anapata kazi anaamkia site anaenda kuvunja nyumba mimi nisingependa yatokee kwa style hiyo ni vizuri kupita kwa DC akaona hukumu yenyewe au amri ya mahakama na kujiridhisha ingawa hana namna ya kubadilisha lakini akawa na taarifa nini kinaenda kufanyika,"amesema Dkt. Mabula.

Akigeukia suala la wito wa mahakama, Waziri Mabula ametaka kujua sheria inasemaje kwa mtu anayepelekewa wito na kukosekana mara moja au mbili nyumbani kwake. 

"Nisingependa malalamiko yatokane na madali walioteuliwa halafu mtu akose haki kutokana na kutopata wito au nyaraka iliyotoka mahakamani na taratibu nyingine zikaendelea ni vizuri kuangalia utaratibu mzuri wa kuhakikisha mhusika amefikiwa na kama hakufikiwa utaratibu upi unatumika ili walau afahamishwe kile kinachoendelea vinginevyo tunatumia madalali badala ya kupunguza changamoto zinakuwa zinaendelea,"amesema Mabula. 
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya. Wa pili kulia ni Katibu Mkuu, Mhandisi Anthony Sanga. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI).
.
Majukumu makuu ya Kamati ya Uteuzi na Nidhamu ya Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya ardhi ni kufanya uteuzi wa Madalali na Wasambaza Nyaraka wa Mabaraza ya ardhi, Kusikiliza na kuamua madai ya utovu wa nidhamu dhidi ya madalali na wasambaza nyaraka wa mabaraza ya ardhi pamoja na kuunda na kusimamia kamati ndogo za kusimamia Madalali na Wasambaza Nyaraka katika ngazi za mikoa. 

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news