Waziri Mkuu azindua huduma ya upandikizaji uloto Benjamin Mkapa

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iliamua kuwekeza shilingi bilioni 2.7 ili kuanzisha huduma ya upandikizaji uloto na kupunguza gharama za matibabu hayo kwa wananchi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Huduma ya Upandikizaji Uloto (Bone Marrow Transplatation) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, Mei 10, 2023. Wengine kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt Grace Maghembe, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandikwa , Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na kulia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Donald Menjiti. Mtoto aliyesimama katikati ni Esther Osena ambaye ametoa Uloto uliopandikizwa kwa kaka yake Elisha Osena. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Kwa lugha nyingine, kuimarika kwa huduma za kibingwa na bobezi nchini kumepunguza gharama kubwa iliyokuwa inatumiwa na Serikali ili kuwezesha Watanzania wenye uhitaji kupata huduma hizo nje ya nchi. Kwa mfano, huduma hii ya upandikizaji uloto ikitolewa katika hospitali hii, itagharimu shilingi milioni 50 hadi 55 kwa mgonjwa mmoja,” amesema.
Amesema hayo leo Mei 10, 2023 wakati akizungumza na wananchi na watumishi wa hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma mara baada ya kuzindua huduma za kibingwa za upandikizaji wa uloto (Bone Marrow Transplant) hasa kwa watu wenye Seli Mundu (Sickle Cell).

Waziri Mkuu amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa inakuwa hospitali ya pili baada ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuzindua huduma hiyo ya upandikizaji wa uloto na hivyo, kuifanya kuwa miongoni mwa hospitali chache zinazotoa huduma hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na mtoto Elisha Osena (kulia) ambaye amepandikizwa Uloto (Bone Marrow Transplantation) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa baada ya kuzindua huduma hiyo kwenye hospitali hiyo jijini Dodoma, Mei 10, 2023. Kushoto ni dada wa mtototo huyo, Esther Osena ambaye ametolewa Uloto uliopandikizwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

“Upandikizaji uloto unatoa nafuu kubwa sana kwa wagonjwa wa seli mundo kwani huwapunguzia kwa kiasi kikubwa maumivu na maambukizi ya mara kwa mara na wakati mwingine huwa sababu ya kupona kabisa kwa ugonjwa huu wa kudumu. Kutokana na nafuu hiyo, mgonjwa huweza kuishi maisha yenye ubora na kushiriki vema katika shughuli mbalimbali ikiwemo masomo”.

Amesema uzinduzi wa huduma hiyo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa ni ushahidi tosha wa namna ambavyo Tanzania inapiga hatua kuboresha huduma za afya. “Huduma za namna hii kuendelea kutolewa katika hospitali zetu si jambo dogo, na hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa huduma kama hizi zinapatikana katika nchi chache sana kwenye bara la Afrika.”
“Nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kutoa rasilimali fedha kwa ajili ya kununulia vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na dawa pamoja na kuwaendeleza kielimu wataalamu wetu katika ngazi za ubingwa na bobezi,” amesema.

Kabla ya kuzungumza na hadhira hiyo, Waziri Mkuu alitembelea wodi za kitengo maalum cha upandikizaji uloto na kuzungumza na watoto na wazazi wenye watoto waliopatiwa tiba hiyo. Wote waliishukuru Serikali kwa kuanzisha huduma hiyo kwani imewasaidia watoto wao kuondokana na maumivu ya mara kwa mara na kutumia muda mwingi kwenda kliniki ya seli mundu kupata matibabu.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washikiri wa uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema kila mwaka duniani kote watoto wapatao 300,000 wanazaliwa na tatizo la Seli Mundu na hapa Tanzania kila mwaka wanazaliwa watoto 11,000 ambapo kati yao watoto 6,000 wanafikiwa na huduma za kliniki.

“Watoto wanaozaliwa na tatizo la seli mundu huwa wanapata maumivu ya mara kwa mara ya viungo, wanakuwa na tatizo la kupungukiwa damu, wanakosa masomo kwa miezi mingi. Kuna mzazi amesema mwanaye alikuwa anahudhuria masomo kwa miezi mitatu tu kati ya 10 anayopaswa kuwepo shuleni,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Ummy amesema wizara hiyo inaangalia uwezekano wa kuipandisha hadhi hospitali hiyo ili iwe hospitali ya Taifa badala ya kuendelea kubakia kuwa ya kanda. “Tumeanza kujenga kituo cha kutoa tiba ya kansa na pia tunataka tujenge kituo cha umahiri cha matibabu ya moyo ili kuimarisha utoaji wa huduma kwenye hospitali yetu.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Alphonce Chandika alimweleza Waziri Mkuu kwamba tangu Januari 19, mwaka huu hadi leo, wamefanikiwa kupandikiza uloto kwa watoto watatu na wote wanaendelea vizuri. “Watoto wawili wanatoka kijiji jirani cha Mapinduzi na mmoja anatoka eneo la Area D hapahapa Dodoma.”

Alisema kufanyika kwa upandikizaji wa uloto kwenye hospitali hiyo, kumeifanya Tanzania iwe miongoni mwa nchi saba zinazotoa huduma hiyo barani Afrika. Alizitaja nchi nyingine zinazotoa huduma hiyo kuwa ni Algeria, Afrika ya Kusini, Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia. “Kwa mantiki hiyo, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuanza kutoa huduma hiyo.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news