ZHC waanza mchakato ujenzi nyumba za makazi Mombasa kwa Mchina mjini Unguja

NA SALMA LUSANGI

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ali Said amesema ZHC imeanza mchakato wa ujenzi wa nyumba 72 za makazi katika eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja ili kuwaletea wananchi wa Zanzibar makaazi bora.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, harakati za ujenzi wa nyumba hizo zimeanza mwezi Machi, mwaka huu ambapo shirika hilo limefunga mkataba wa ujenzi na Mkandarasi Simba Developers Ltd. Hivyo Mkandarasi huyo ameanza kazi rasmi.

Mkurugenzi Mkuu amesema, ujenzi huo utagharimu shilingi za Tanzania bilioni 9.8 hadi kumalizika kwake kati ya fedha hizo shilingi bilioni tatu zitatoka katika mfuko wa ZHC na fedha zingine zimetoka katika mfuko wa Serikali kuu kwa maana ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Dkt, Hussein Ali Mwinyi.

Alifahamisha kwamba, ZHC imekubaliana na Mkandarasi huyo katika kipindi cha muda wa miezi 15 kuanzia Machi, 2023 nyumba hizo ziwe zimekamilika ili shirika liweze kuziuza nyumba hizo kwa wananchi mbalimbali ambao watahitaji kununua.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Mwanaisha Ali Said (katikati) na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Simba Developers Ltd, Nurdin Hussein wakisaini Mkataba wa ujezi wa Nyumba za Makazi zinazojengwa eneo la Mombasa kwa Mchina Unguja.

“Lengo letu ni kuziuza nyumba hizo kwa mwenye kuhitaji, pesa za ujenzi Bilioni tatu tumetoa ZHC na fedha zingine tumepewa na Serikali kuu, nyumba zote zitakua 72 mtu pesa zake tu,”amesema 

Aidha, Mkurugenzi Mwanaisha amesema bei ya kuziuza nyumba hizo zitatofautiana kwa sababu kutakuwa na nyumba za vyumba vitatu na zingine vyumba viwili ila kiwango cha bei itapangwa na Serikali baada ya ujenzi kukamilika. 
Naye Meneja Mkuu wa kampuni ya Simba Developers Ltd, Nurdin Hussein ameishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuiamini kampuni yake na kuipa dhamana ya kujenga nyumba hizo. Hivyo ameahidi kwamba kampuni yake itafanya kazi kwa ufanisi na kwa wakati muwafaka kama walivyokubalina na ZHC.

Kwa upande wa wananchi wa Zanzibar akizungumza, Bi.Asha Ali Kombo (51) mkazi wa Fuoni Uwandani ameishukuru Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa uamuzi wa kujenga nyumba mpya kwani ni wazi kwamba Nyumba za Maendeleo Zanzibar ni chache na kongwe hivyo hatua hiyo itasaidia kuondoa malalamiko kwa Shirika la Nyumba Zanzibar. 

Naye Omar Ali Issa (48) mkazi wa Rahaleo ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuweka mpango wa kuwauzia watu kwa kulipa fedha kidogo kidogo kwa wenye kipato cha chini. Alieleza kwamba kutokana na kipato tofauti baadhi ya watu hawataweza kutoa kiwango kikubwa cha fedha kwa pamoja ila kwa kulipa nusu nusu wataweza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news