Viongozi ALAT wapongeza utekelezaji miradi Manispaa ya Iringa

NA PETER JOSEPH

UONGOZI wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) umepongeza ubora wa miradi ya kijamii ambayo imetekelezwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salim Abri Asas katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Akizungumza kwa niaba ya viongozi na watendaji wa ALAT kabla ya kumtunukia tuzo ya cheti MNEC huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya ASAS Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa Mhe.Sima Constantine Sima amesema ALAT imempatia tuzo hiyo kutokana na kuthamini kazi kubwa ya kujitolea aliyoifanya ya kufadhili miradi mbalimbali katika halmashauri za mkoa wa Iringa.

Miongoni mwa miradi iliyofadhiliwa na ASAS ni pamoja na ile ya elimu, afya na ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo wadogo katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa,

Mbali na kutoa fedha za ufadhili wa miradi Makamu Mwenyekiti huyo amesema wao kama wasimamizi wa halmashauri zote 184 nchini kuna kitu wamejifunza baada ya kuitembelea miradi hiyo na kujionea ubora wa miradi hiyo.

Amesema utekelezwaji mzuri wa miradi hiyo uliofanywa na ASAS umewapa somo Viongozi wa ALAT kuhusu usimamizi wa fedha za miradi ya halmashauri wanazoziongoza.

“Mbali na msaada unaotolewa lakini ‘standard’ ya miradi inayotekelezwa, kuna kitu kikubwa cha kujifunza sisi kama wasimamizi wa halmashauri,” amesisitiza Mhe. Sima na kuongeza:

“Mradi unatekelezwa lakini katika kiwango chenye ‘standard’ kubwa ambacho hata sisi (wasimamizi wa halmashauri) tungepewa ufanywe chini ya usimamizi wetu wenyewe tusingeweza kufanya kitu kama kile,” amesema.

Makamu Mwenyekiti huyo wa ALAT Taifa ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza amesema kuwa anapoona miradi ikitekelezwa na mdau kama ASAS katika utimilifu kuliko kama ingesimamiwa na halmashauri, anaamini kuwa ipo haja kwa viongozi wa halmashauri kuongeza uwajibikaji ili kuleta ufanisi katika miradi inayosimamiwa.

Mojawapo ya mradi uliomvutia Makamu Mwenyekiti huyo wa ALAT ni mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama ‘wamachinga’ ambapo amekiri kuwa kukosekana kwa miundombinu muhimu inayotumiwa na wafanyabiashara hao kama kuwepo kwa vibanda kwa ajili ya vivuli na vyoo ni changamoto kubwa kwa majiji sita nchini.

“Agizo la Mhe Rais (Samia Suluhu) lilikuwa twende tukawapange lakini swali muhimu tunapaswa kujiuliza sisi viongozi wa halmashauri ni wapi tukawapange wamachinga,” amesema Mstahiki Sima na kuongeza:

“Sisi pale Mwanza kuna sehemu tulikuwa na dampo pale tuliwapeleka wafanyabiashara hao kule lakini kesho yake walirudi mjini, kwa sababu tulikosa mtu wa kutusaidia kufanya reconciliation (upatanisho) kama alivyofanya ASAS hapa Iringa.”

Amesema kuwapatia miundombinu wanayoyahitaji wamachinga ndiyo jambo kuu la msingi kabla ya kuwapeleka wafanyabiashara wadogo wadogo kwenye maeneo yaliyotengwa na halmashauri.

Amesema haina maana kwa viongozi wa halmashauri kupanga kutumia mathalani shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuweka mafuta kwenye magari na kuwatumia Mgambo na Maaskari ili kuwatoa wamachinga katikati ya miji wakati halmashauri zinashindwa kutumia walau shilingi laki tano kujenga vibanda na vyoo kwa ajili ya kuwawezesha Wamachinga hao kuendesha shughuli zao katika mazingira rafiki.

Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Mhe. Ibrahim Ngwada aliitaja baadhi ya miradi iliyofadhiliwa na ASAS katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwa ni pamoja na ukarabati wa jengo la ofisi ya Mstahiki Meya kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 150, na Jengo la ustawi wa jamii lililogharimu zaidi ya milioni 60.

Miradi mingine ni mradi wa soko la wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama wamachinga ambalo liligharimu zaidi ya shilingi milioni 220 kwa ajili ya ujenzi wa vibanda, vyoo na eneo la soko la matunda.

Kwa upande wake Mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya Taifa aliwashukuru viongozi wa ALAT kwa kuthamini juhudi alizozifanya katika halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Viongozi wa Jumuiya hiyo katika kusukuma gurudumu la maendeleo la Manispaa ya Iringa.

Amesema ziara ya viongozi wa ALAT imempa hamasa ya kuendelea kujitolea na imemuongezea wadau na kuahidi kushirikiana na ALAT katika shughuli zao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news