Benki Kuu yatoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeukumbusha umma kwamba Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Juni 20, 2023 na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Tutuba imefafanua kuwa, tamko la kwanza lilitolewa mwezi Agosti 2007 na la pili mwezi Desemba 2017.

"Hata hivyo, katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa kama ifuatavyo:

i. Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi; gharama za elimu; huduma za afya,vifaa tiba na vitendanishi; gharama za usafiri, lojistiki na bandari; vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano, n.k.

ii. Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakaazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni.

"Bei hizi zinajumuisha gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.

iii. Viwango vya kubadilisha fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni benki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pekee yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

iv. Mkaazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.

"Benki Kuu inapenda pia kuukumbusha umma kuwa kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 kinaelekeza kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusiwa kutumika nchini, hivyo hakuna mtu au kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa kwa malipo yoyote halali (legal tender). Kitendo cha kukataa malipo kwa shilingi ya Tanzania ni kuvunja Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006,"amefafanua Gavana Tutuba kupitia taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news