Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umepeleka huduma zake moja kwa moja katika Maonesho ya Nane Nane yanayoendelea jijini Dodoma, ukiwalenga kuwafikishia wafanyabiashara, wakulima na wananchi huduma za usajili, utoaji wa leseni pamoja na elimu kuhusu mfumo mpya ulioboreshwa wa usajili wa biashara.
BRELA imesema huduma hizo zinapatikana katika Viwanja vya Nane Nane kuanzia Agosti 1 hadi Agosti 8, 2026, ili kuwawezesha wananchi kupata huduma mbalimbali kwa urahisi bila kulazimika kufika katika ofisi za taasisi hiyo.Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Usajili kutoka BRELA, Yusuf Mwasakafika, amesema wananchi wanaweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo usajili wa majina ya biashara, usajili wa kampuni, utoaji wa leseni za biashara Kundi A pamoja na huduma zinazohusiana na usajili wa alama za biashara na viwanda.Amesema uwepo wa BRELA katika maonesho hayo unalenga pia kuwahamasisha wakulima wanaofanya kilimo cha kibiashara kurasimisha shughuli zao ili waweze kufanya biashara kwa kujiamini zaidi na kunufaika na fursa za masoko.
“Tunawahamasisha wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wanaofanya shughuli mbalimbali za kilimo kufika hapa na kupata huduma ambazo wangeweza kuzitafuta wakiwa ofisini, lakini sasa wanaweza kuzipata hapa,” amesema Mwasakafika.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo






















