Bunge laidhinisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali 2023/24

NA DIRAMAKINI

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa la Tanzania limeidhinisha kwa kishindo Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 yenye jumla ya shilingi trilioni 44.39.

Kupitia bajeti hiyo,mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38, sawa na asilimia 70.7 ya bajeti yote huku mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi (wizara,idara,taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa yatakuwa shilingi trilioni 4.66.

Akitangaza kura zilizopigwa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Tulia Ackson Mwansasu amesema kuwa,wabunge 374 walikuwepo bungeni na wengine 18 hawakuwepo (Bunge la Tanzania lina wabunge 393, akiwemo Spika).

Alisema kuwa wabunge 354 walipiga kura ya ndiyo, wabunge 20 walikuwa vuguvugu (abstain), na hakuna Mbunge aliyepinga Bajeti Kuu, ambapo matokeo hayo ni sawa na asilimia 95 ya wabunge wote walioikubali na kuipitisha.

Idadi hiyo ya kura za ndio ni sawa na asilimia 95 ambapo miongoni mwa wabunge waliounga mkono bajeti hiyo ni wabunge watatu wa vyama vya upinzani ambao ni wabunge wa viti maalum, Mheshimiwa Nusrat Hanje na Salome Makamba kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Sambamba na Mbunge wa Mtambile, Mheshimiwa Seif Salim Seif wa Chama Cha ACT Wazalendo ambapo imeelezwa fedha zinazokwenda kutekeleza miradi ya maendeleo ni fedha nyingi zaidi kuwahi kutolewa kwa mwaka tangu tupate uhuru.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba akihitimisha hoja Juni 26, 2023 bungeni jijini Dodoma amesema, katika uongozi wa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, fedha zinazokwenda katika wizara,mikoa,wilaya na majimbo ni fedha nyingi ambazo hazijawahi kutokea na kusisitiza kuwa hakuna wizi serikalini.

Pia, katika mjadala wa bajeti hiyo wabunge wengi walihoji kuhusu tozo ya shilingi 100 kwenye mafuta ya petroli na dizeli ambapo Dkt.Mwigulu amesema tozo hiyo ni jambo jema.

Amesema, ni jambo jema kwa sababu linakwenda kutunisha mfuko wa mapato kwa serikali na hivyo kuiwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kijamii.

Katika hatua nyingine, Bunge limepitisha Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2023 ambao pamoja na mambo mengine unalenga kuzifanyia marekebisho sheria zipatazo 18 ili kufanikisha utekelezaj iwa bajeti hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news