John Kayombo aomba ushirikiano Dodoma Jiji

NA DENNIS GONDWE

MKURUGENZI wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, John Kayombo ameomba ushirikiano kwa Baraza la Madiwani na Timu ya Menejimenti ya jiji hilo katika kutekeleza majukumu yake ili kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuwaletea maendeleo watanzania.

Joseph Mafuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi (kulia) akimkabidhi nyaraka za ofisi John Kayombo, Mkurgenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kauli hiyo aliitoa baada ya kukabidhiwa rasmi nyaraka za Ofisi ya Mkurugenzi kutoka kwa aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Joseph Mafuru katika ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Kayombo alisema kuwa kikubwa anachoomba kutoka timu ya menejimenti ni ushirikiano. “Ndugu zangu ushirikiano wenu ndiyo utakaofanya twende mbele alipoishia ndugu yangu Joseph Mafuru. Ushirikiano kutoka Kamati ya Usalama ya Wilaya kwa sababu kuna maeneo ambayo utakwenda na wataalam na hutaweza kuingia utalazimika kuomba msaada upande wa pili ili mambo yaende. Mstahiki Meya na Baraza lako la Madiwani niombe sana ushirikiano wenu. 
 
"Tuelekezane ili mambo yaweze kwenda, lengo la serikali ni kufanya kazi ili wananchi waweze kupata zile huduma mahususi. Nitaomba ushirikiano kutoka Ofisi ya Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma. Mimi ninaamini kabisa tukiunganisha ‘timework’ alipopaacha Joseph Mafuru, sisi tutakwenda mbele zaidi” alisema Kayombo.

Mkurugenzi huyo aliwataja wakuu wa divisheni na vitengo wa Halmasaghuri ya Jiji la Dodoma kuwa watofauti.

“Wakuu wa divisheni na vitengo ukishapata bahati ya kuwa mkuu wa divisheni na kitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wewe ni tofauti na mkuu wa divisheni na vitengo wa maeneo mengine.

"Lazima uwe na kitu cha ziada usijilinganishe na wale wengine. Kuna maelekezo ya serikali, Mheshimiwa Rais ana maelekezo yake maalum ambayo anataka yatekelezwe, naomba tujikite kwenye hayo maelekezo, ile ndoto ya wenye ilani tuhakikishe inafikiwa. Kwa upande wangu mtegemee ushirikiano mkubwa sana ili Mheshimiwa Rais tusimuangushe na tuanze mwaka mpya wa fedha vizuri,” alisema Kayombo.

Kwa upande wa mkurugenzi aliyehama, Joseph Mafuru alivitaja vitu ambavyo vipo katika nyaraka za makabidhiano kuwa akaunti za halmashauri zinazotaja kiasi cha fedha kilichopo.

“Nakukabidhi na ‘token’ ya mkurugenzi ambayo nilikuwa naitumia. Na mali nyingine unajua Jiji la Dodoma lina mali nyingi kuanzia mitambo na magari. Kuna majengo, viwanja ukipata muda maafisa wapo kwa ajili ya kukupitisha kwenye mali za halmashauri.

"Nakukabidhi na watumishi 4,740. Mkurugenzi Kayombo, upatapo changamoto yoyote nipo ‘frexible’ nitumie ujumbe, nipigie niulize nitakusaidia kwa sababu naamini tunajenga nchi moja hatupaswi kuacha vitu vya watu ‘unattended’. Aidha, niwashukuru wote kwa ushirikiano na upendo wenu mlionipa kwa kipindi chote nilichofanya kazi katika Jiji la Dodoma,”alisema Mafuru.

Nae Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Godwin Gondwe alisema kuwa utendaji kazi wa Halmashauri ya Jiji unatakiwa kujikita katika utoaji huduma kwa wananchi. “Mheshimiwa Rais ametutuma wote kutoa huduma bora kwa wananchi na mimi sina shaka nawe Kayombo katika eneo hilo.

"Mheshimiwa Rais siku zote anatuelekeza kusikizia kero za wananchi na kutatua changamoto zao. Jambo la pili ni mapato nalo amekuwa akilisisitiza sana. Halmashauri ya Jiji la Dodoma lazima tujikite katika ukusanyaji mapato ili yasaidie katika kutoa huduma bora kwa wananchi,”alisema Gondwe.

Ikumbukwe kuwa mapema mwezi huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alifanya mabadiliko ya wakurugenzi wa mamlaka za serikali ya mitaa nchini yaliyomuhamisha Joseph Mafuru kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenda Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na John Kayombo kuhamia Halmashauri ya Jiji la Dodoma akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news