Mapato, Sekta ya Fedha yazidi kufanya vema

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan iingie madarakani imerekodi mafanikio mbalimbali nchini.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akionesha Bajeti kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, wakati akiwasilisha Bajeti hiyo, Bungeni jijini Dodoma, Juni 15, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ameyasema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

"Tunakumbuka kuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alishika madaraka ya kuongoza nchi katika kipindi ambacho dunia ilikuwa katika mtikisiko wa kiuchumi kutokana na janga la UVIKO-19 na baadae vita kati ya Urusi na Ukraine ambayo inaendelea hadi sasa.

"Athari za majanga hayo zilionekana katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii duniani ikiwemo kuongezeka kwa vifo,kuzorota kwa shughuli za uzalishaji na kuongezeka kwa gharama za utoaji huduma za jamii, hususan afya na elimu pamoja na kuongezeka kwa gharama za maisha,"ameeleza.

Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, kutokana na athari hizo, ukuaji wa uchumi nchini ulipungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2019 hadi asilimia 4.7 mwaka 2022.

Amebainisha,pamoja na kupokea kijiti cha uongozi katika kipindi cha majanga hayo, uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan umetekeleza sera na mikakati mbalimbali iliyowezesha uchumi wa nchi yetu kuhimili majanga hayo ikiwemo utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti.

"Ni dhahiri kuwa, utekelezaji wa sera na mikakati hiyo umeleta mafanikio makubwa katika kipindi cha uongozi wa Awamu ya Sita. Mafanikio mengi yaliyopatikana katika kipindi cha Awamu ya Sita yamesemwa na Waheshimiwa Mawaziri wakati wakiwasilisha hotuba zao. Naomba nami nitambue baadhi ya mafanikio hayo,"ameeleza Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu.

Mapato

Waziri Dkt.Nchemba amelieleza Bunge kuwa, katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mapato ya ndani yamekuwa yakiongezeka na kufikia shilingi trilioni 24.40 mwaka 2021/22 ikilinganishwa na shilingi trilioni 20.59 mwaka 2020/21.

Aidha, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023, ukusanyaji wa mapato ya ndani umefikia shilingi trilioni 21.67, ambapo mwezi Desemba 2022, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi trilioni 2.63 ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kukusanywa kwa mwezi tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 1996.

"Waheshimiwa wabunge, mwenendo huu mzuri ni ishara kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ipo makini katika kutekeleza mikakati ya kuongeza mapato kwa kuzingatia sheria,miongozo na taratibu pamoja na jitihada za kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini,"amebainisha Waziri wa Fedha na Mipango.

Sekta ya Fedha

Akizungumzia kwa upande wa Sekta ya Fedha amesema,Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Serikali wa Kuboresha Mazingira ya Biashara nchini.

Utekelezaji wa sera hizo, Waziri Dkt.Nchemba amefafanua kuwa, umesababisha kushuka kwa viwango vya riba za mikopo ya benki ambapo katika kipindi cha mwaka kinachoishia Aprili 2023, viwango vya riba za mikopo vilipungua na kufikia wastani wa asilimia 15.91 kutoka wastani wa asilimia 16.58 Aprili 2021.

Kupungua kwa viwango vya riba za mikopo, amesema kumechangia kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi ambapo mikopo hiyo imeongezeka kwa asilimia 22.5 Aprili 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.8 Aprili 2021. Aidha, mikopo chechefu imeendelea kupungua hadi asilimia 5.5 Aprili 2023 ikilinganishwa na asilimia 9.8 Aprili 2021.

Waziri Dkt.Mwigulu amesema, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuimarisha usimamizi wa sekta ndogo ya benki ili kuongeza ufanisi katika eneo hilo.

"Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan,inatambua umuhimu wa kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwemo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Hivyo, Serikali inafanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika ugawaji na urejeshwaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri.

"Utaratibu mpya wa utolewaji na urejeshaji wa mikopo hiyo utakapokamilika, Serikali itatoa taarifa kwa umma na kuendelea kutoa mikopo hiyo.

"Mheshimiwa Spika, napendekeza kuweka shilingi bilioni 1.0 kwenye mfuko wa watu wenye ulemavu kwa ajili ya kusaidia vifaa vinavyohitajika.

"Fedha hizo pia zitatumika kama mfuko wa wabunge wa kundi la watu wenye ulemavu na mchango kwa watoto wanaolelewa katika vituo maalumu.

"Nitoe rai kwa makampuni na watu binafsi kuchangia katika mfuko huo ili kuyasaidia haya makundi maalumu sambamba na programu inayotekelezwa chini ya TASAF. Mama ameanzisha, sote tumuunge mkono,"amesisitiza Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Pia, amesema Serikali inatarajia kufanya marekebisho katika Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha, Sura 342. Marekebisho hayo yataiongezea Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board-DIB) majukumu ya kuweza kuongeza ukwasi kwa njia ya mkopo kwa benki au taasisi ya fedha yenye changamoto ya ukwasi.

"Marekebisho hayo pia yataipatia DIB nguvu na uhalali wa kisheria wa kushiriki kikamilifu, kwa kushirikiana na Benki Kuu, katika kutathmini na kuamua hatua muafaka ambayo inapaswa kuchukuliwa pindi benki au taasisi ya fedha inapokuwa katika hatari ya kufilisika.

"Utaratibu huu utasaidia kuokoa benki au taasisi za fedha kuingia kwenye mchakato wa ufilisi na hivyo kuepusha hasara na adha kubwa kwa wenye amana na wadai wengine,"amesema.

Wakati huo huo, Waziri Dkt.Nchemba amesema, Serikali imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kikosi Kazi cha Kifedha cha Kimataifa (Financial Action Task Force-FATF), ambapo ilifanikiwa yafuatayo.

Mosi, amesema ni kufanya marekebisho ya sheria na kanuni kama sehemu ya kutekeleza viwango vya kiufundi vya FATF.

Pili,kutengeneza Mkakati wa Kitaifa wa Kudhibiti Utakasishaji Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi wa Mwaka 2022/23 hadi 2026/27.

Tatu, amesema ni kufanya mapitio ya vihatarishi vya ufadhili wa ugaidi kwa asasi za kiraia, nne kufanya mafunzo na kampeni mbalimbali za kuongeza uelewa wa masuala ya utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi kwa watoa taarifa na hasa taasisi teule zisizo za kifedha za biashara na taaluma.

Tano, Mheshimiwa Waziri Dkt.Mwigulu amesema ni kuanzisha kituo maalumu cha kushughulikia kesi za utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi na kuandaa miongozo mbalimbali ya kusaidia taasisi zinazosimamia utekelezaji wa sheria katika kuchunguza na kuendesha mashitaka ya utakasishaji fedha haramu na ufadhili wa ugaidi.

"Lengo la hatua hizi ni ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa utakasishaji fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi,"amesema Waaziri Dkt.Nchemba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news