Sekta ya uzalishaji yazidi kung'ara nchini

NA GODFREY NNKO

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt.Mwigulu Nchemba amesema, tangu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan iingie madarakani Sekta ya Uzalishaji nchini imepiga hatua kubwa.

Mheshimiwa Dkt.Mwigulu ameyasema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

"Kwa kutambua ukweli kuwa asilimia kubwa ya wananchi wetu wanaishi vijijini ambapo kilimo ndiyo msingi wa ustawi wa maisha, Serikali ya CCM chini ya Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea na dhamira yake ya kuboresha maisha ya wananchi kwa kuongeza bajeti ya kilimo.

"Ni kutoka shilingi bilioni 294.0 mwaka wa fedha 2021/22 hadi shilingi bilioni 954.0 mwaka wa fedha 2022/23 na kufikia shilingi bilioni 970.8 mwaka wa fedha 2023/24.

"Kuongezeka kwa bajeti ya kilimo kumewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuanzishwa kwa kilimo cha mashamba makubwa ya pamoja (block farms), kuimarisha tafiti na huduma za ugani.

"Kutolewa kwa ruzuku ya mbolea kwa wakulima, kuanza kwa miradi ya ujenzi na ukarabati wa skimu za umwagiliaji na miundombinu ya uhifadhi wa mazao ya kilimo, kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba.

Pia, amesema Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa maghala 14 na vihenge 20 kwa ajili ya kuhifadhi nafaka.

Hatua hizi, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema zilichangia utoshelevu wa chakula kufikia asilimia 114 mwaka 2022/23.

"Serikali itaendelea kuiwezesha Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) kununua mazao kutoka kwa wakulima,"amesema Waziri wa Fedha na Mipango.

Mbali na hayo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Nchemba amesema, katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya tani 400,000 zinatarajiwa kununuliwa na NFRA. Lengo la Serikali amesema ni kuwa na akiba ya chakula inayokidhi mahitaji yasiyopungua miezi minne.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa ruzuku ya mbolea ili kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa gharama nafuu ambapo hadi Aprili 2023, shilingi bilioni 214.8 zimetolewa ikijumuisha fedha za ndani na nje.

Kutolewa kwa ruzuku hiyo, Waziri Dkt.Nchemba amesema kuliwezesha wakulima kupata mbolea kwa bei ya kati ya shilingi 50,000 hadi 70,000 kwa mfuko wa kilo 50 badala ya bei ya soko ya wastani wa shilingi 140,000.

"Kutokana na jitihada zilizochukuliwa na Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kuimarisha sekta ya kilimo, sote tumeshuhudia maendeleo mazuri ya utekelezaji wa miradi ya kilimo.

"Serikali itaendelea kuongeza fedha kwenye sekta hii kadri ufanisi utakavyoongezeka ikiwa ni motisha kwa utendaji mzuri. Hivyo, ninasisitiza sekta izingatie utaratibu wa Performance for Results (P4R).

"Hatua hii inaweza kuongeza fedha zaidi za utekelezaji wa miradi ya kilimo hata kufikia shilingi trilioni 1.27. Serikali ya Dkt. Samia iko kazini,tunataka kupiga vita umaskini kwa vitendo,tutaelewana tu,"amesisitiza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news