MIAKA 25, HONGERA NMB

NA LWAGA MWAMBANDE

BENKI ya NMB chini ya uongozi thabiti wa mwanama Ruth Zaipuna ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki hiyo tangu Agosti 18,2020 imekuwa ikifanya vema katika sekta ya fedha nchini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan akiwa na viongozi mbalimbali kwenye picha ya pamoja Juni 17, 2023 na wafanyakazi wa Benki ya NMB wanaohudumu tangu kuanzishwa kwake mara baada ya kufunga maadhimisho ya miaka 25 ya mafanikio ya benki hiyo Mlimani City Dar es Salaam. (Picha na Ikulu).

Uthabiti huo ndio unaowafanya kutembea kifua mbele wakati wakisherehekea miaka 25 ya safari ya mafanikio. 
 
Kwa mujibu wa muhtasari wa Mkutano Mkuu wa 22 wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo uliofanyika Juni 3, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ulionesha benki hiyo kupiga hatua kubwa.

Mosi, mwaka 2021, benki hiyo ilifanikiwa kuongeza idadi ya wateja hadi kufikia zaidi ya milioni tano kutoka wateja milioni nne.

Pili, iliongeza idadi ya mashine za kutolea fedha (ATM) kufikia 755 kutoka 753. Tatu, iliongeza idadi ya Mawakala mpaka 10,194 kutoka 8,410 huku idadi ya matawi iliendelea kuwa 226 na hiyo ilichangiwa na benki kuunganisha baadhi ya matawi yaliyopo karibu na kufungua matawi mapya maeneo yenye uhitaji zaidi.

Pia,ilielezwa benki iliendelea kuwekeza kwenye njia mbadala ya utoaji huduma za kibenki kama ATM na wakala ili kufikisha huduma za kibenki kwa urahisi kwa wateja. Aidha, idadi ya wafanyakazi iliongezeka mpaka kufikia 3,482 mwaka 2021 kutoka 3,465 mwaka 2020.

Juni 17, 2023 Benki ya NMB jijini Dar es Salaam imekabidhi gawio la shilingi bilioni 45.5 kwa Serikali, ambapo Serikali inamiliki asilimia 31.8 ya hisa katika benki hiyo huku asilimia zingine zikiwa zinamilikiwa na wadau kutoka sekta binafsi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, katika sekta ya mabenki nchini, NMB wanafanya vema, Endelea;

1.Kwa sekta ya mabenki, kweli mwatuheshimisha,
Mambo yenu yanatiki, wazi mwatufahamisha,
Kwetu nyie marafiki, huduma mwazifikisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB!

2.Mmetoka mbali sana, toka benki kuanzisha,
Mmefanya mengi sana, nchi mwaitambulisha,
Mlivyosambaa sana, wengi mnaturidhisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB!

3.Miaka inavyopita, mwazidi jiimarisha,
Huduma bora twapata, tunayajenga maisha,
Na mikopo tunapata, uchumi twaimarisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB!

4.Tumeliona gawio, kubwa tena linatisha,
Kubwa kutoka mawio, na machweo lafikisha,
Tuwaimbie pambio, shangwe za kuwavumisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

5.Twaona mipango yenu, kweli inaturidhisha,
Hamfanyi yenu yenu, yote mwatushirikisha,
Kesho yetu lengo lenu, muweze kutufikisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

6.Mmejizatiti sana, mzidi tufurahisha,
Kwa huduma bora sana, ngazi zote za maisha,
Wakubwa hata vijana, wote mwawashirikisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

7.Kama nchi Tanzania, uongozi unatisha,
Juu ni mama Samia, nchi anaiendesha,
Zaipuna kakalia, gurudumu aendesha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

8.Viongozi wanawake, vema mnawakilisha,
Bora sana tuwatake, idadi ya kuridhisha,
Mema mengi yatufike, yale ya kutuwandisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

9.Wilaya gani uende, tawi hawajaanzisha,
Mawakala kila pande, kazi waungurumisha,
Jumuishi kila pande, huduma wanafikisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

10.Heri tunawatakia, mzidi jiimarisha,
Faida zidi ingia, ile inayoridhisha,
Na ukubwa shikilia, mzidi tuwakilisha,
Miaka ishina tano, hongera NMB.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news