Namibia yaguswa na huduma za matibabu ya moyo JKCI

NA MWANDISHI WETU 

WABUNGE wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia wameipongeza Serikali kwa kuimarisha huduma za matibabu ya moyo jambo ambalo limewafanya watanzania na mataifa mengine kutibiwa moyo hapa nchini.
Msimamizi wa kliniki maalumu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Afisa Uuguzi Odilia Njau akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia jinsi wanavyowahudumia wagonjwa wanaotibiwa katika kliniki hiyo wakati wabunge hao walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Pongezi hizo zimetolewa na wabunge hao jijini Dar es Salaam wakati walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwaajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa pamoja na kujifunza jinsi ambavyo Tanzania imefanikiwa katika kutoa huduma za matibabu hayo. 

Kiongozi wa msafara wa wabunge hao Julieta Kavetuna alisema kufika kwao katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wamejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuona mitambo na vifaa tiba vya kisasa vya kutoa huduma za matibabu ya moyo.

“Nchini Namibia hatuna Taasisi ya Moyo kama hii sisi tuna idara ya magonjwa ya moyo ambayo iko katika Hospitali ya Taifa, lakini kama Serikali ikiamua tunaweza kuwa na Hospitali ya moyo inajitegemea ambayo itakuwa inatoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wagonjwa,”amesema.
Daktari bingwa wa wagonjwa wa dharura na mahututi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Vivienne Mlawi akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia jinsi wanavyowahudumia watoto waliolazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji wanaohitaji uangalizi maalum wakati wabunge hao walipotembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

“Vitu tulivyojifunza hapa ikiwa ni pamoja na kusomesha wataalamu, kufanya kazi kwa pamoja, kutoa huduma bora kwa wagonjwa na kununua vifaa tiba vya kisasa tutakwenda kuvifanyia kazi Namibia, ninaamini miaka michache ijayo nasi tutakuwa na Hospitali ya moyo”, alisema Julieta.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Anjela Muhozya alisema tangu kuanzishwa kwa Taasisi hiyo mwaka 2015 idadi ya wagonjwa wa ndani na nje ya nchi imekuwa ikiongezeka hii ni kutokana na kuwa na wataalamu wa kutosha pamoja na vifaa tiba vya kisasa.

Dkt. Angela alisema ili kuongeza ujuzi wataalamu wa Taasisi hiyo wamekuwa wakifanya kambi maalumu za matibabu na upasuaji wa moyo kwa kushirikiana washirika wao kutoka mataifa mbalimbali yaliyoko katika Bara la Ulaya, Marekani, Australia na Asia.
Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt.Anjela Muhozya akiwaeleza wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia aina ya upasuaji wa moyo unaofanyika katika Taasisi hiyo wakati wabunge hao walipotembelea JKCI kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. 

“Tunaishukuru Serikali ambayo imekuwa ikituunga mkono kwa mambo yote tunayoyafanya kwani imesomesha wataalamu,kutujengea majengo na kutununulia vifaa tiba nasi kama wataalamu tunahakikisha watu wenye matatizo ya moyo wanapata huduma bora na kwa wakati,”amesema.

“Taasisi yetu inatoa huduma ya tiba mkoba ya kuwafuata wananchi mahali walipo tunatoa huduma hii kwa kushirikiana na wenzetu wa hospitali husika. Wakati tunatoa huduma hii tunafanya mafunzo ya kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili waweze kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo kwa kufanya hivi wagonjwa wanatambuliwa mapema na kupata huduma kwa wakati.
Viongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Masuala ya Usawa wa Jinsia, Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Familia kutoka Bunge la Namibia wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya wabunge hao kumaliza ziara yao ya kutembelea Taasisi hiyo kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Dkt. Angela alisema Taasisi hiyo pia imekuwa ikipokea wagonjwa kutoka nchi inazopakana nazo mipaka zikiwemo za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Somalia, Sudani, Zambia, Congo, Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na Visiwa vya Comoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news