Rais Dkt.Mwinyi azidisha tabasamu kwa wazee

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amezitaka mamlaka husika zinazoshughulika na masuala ya pensheni na pensheni jamii kwa wazee, kurekebisha na kuboresha mifumo yao ili zoezi la utoaji wa pensheni kwa mwezi Julai, mwaka huu kuanza bila ya kikwazo chohote.

Pia, amezitaka mamlaka hizo kujitahidi kumaliza zoezi la usajili na uhakiki wa masuala yote muhimu yanayowahusu wazee hao ili yakamike ndani ya mwezi huu wa Juni ili ifikapo Julai, mwaka huu kusiwe na kasoro zozote zitakazowakosesha wazee kupata haki yao ya pensheni.

“Nisingependa hata kidogo kwa nia njema tuliyokuwa nayo ya kuwasaidia wazee, halafu usikie Julai imefika, huyu hajapata, huyu kakosa kitambulisho, itakua hatujawasaidia wazee,”amesisitiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Rais Dkt.Mwinyi ametoa maagizo hayo alipozungumza na Jumuiya ya Wazee na Wastaafu, Zanzibar (JUWAZA), Ikulu jijini Zanzibar waliofika kumpongeza kwa hatua yake ya kuwajali na kuwaongezea pensheni na pensheni jamii.

Akizungumia changamoto ya vitambulisho kwa wazee hao hasa wakati wa kupata haki zao za msingi, Rais Dkt. Mwinyi amezishauri mamlaka husika kurasimisha baadhi ya vitambulisho kwa wazee hao ili wapate haki zao zote kwa wakati yakiwemo masuala ya jamii.

Ameshauri kuwe na utaratibu mzuri kwa wazee hao kupata haki zao kwa wakati kusiwe na urasimu na kuwanyima haki zao za msingi.

“Hakuna ubaya wa kurasimisha vitambulisho, sio lazima vitumike “ZAN ID” au “NIDA” katika kuwapatia wazee haki zao, kama wengine hawana vitambulisho hivyo, kuwe na utaratibu kurasimisha ama kuanzishwe vitambulisho maalumu vya wazee vitakavyowaunganisha na huduma zao zote zikiwemo pensheni, pensheni jamii na masuala ya kijamii ikiwemo usafiri, afya na wepesi wa kupata huduma nyingine,"ameagiza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Mwinyi alizishauri mamlaka zinazosimamia pensheni za wazee kushirikiana na jumuiya hiyo ya wazee ili kubaini wazee wanaozidi ama kupungua kwenye uhakiki wao.

Ameeleza kuna haja ya taasisi za Serikali zinazoshughulikia masuala ya wazee, kukaa pamoja na kuongeza ushirikiano baina yao na JUWAZA ili kupata takwimu sashihi zinazowahusu wazee wote nchini.

Aidha, amewaahidi wazee hao kwamba atatoa maagizo kwa uongozi wa wizara tatu za Serikali zikiwemo Fedha, Ustawi wa Jamii na Afya, ili wakae pamoja na wazee hao kwa lengo la kujadiliana na kuondoka na mipango mizuri ya kuimarisha ustawi wa wazee hao kwa sasa na baadae.

“Niombe na maelekezo nitatoa, kwa wizara tatu za Serikali, mkutane na timu za uongozi wa Wizara ya Fedha, Ustawi wa Jamii na Afya, mjadiliane ili muondoke na mpango mzuri wa kuyafikia haya,"amesisitiza Dkt.Mwinyi.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Katibu wa JUWAZA, Salma Kombo Khamis aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia wazee wa Zanzibar daktari maalum atakayeshughulikia masuala ya wazee kwenye hospitali kuu ya Mnazi Mmoja (Geriatrician) pamoja na wauguzi wa masuala ya wazee tu, ili kuwaondoshea usumbufu wazee wengi wanaotibiwa kwa kuondoshwa njiani tu bila ya uangalizi wa kina kwa mujibu wa hali zao.

Aidha, waliiomba Serikali kupitia vyuo vya afya nchini kuona umuhimu wa kuongezwa kufundishwa kozi maalumu ya kada ya utaalamu wa kuwatibu na kuwashughulikia wazee na iwe endelevu kwa manufaa ya wazee wa sasa na wa baadae.

Pamoja na kuangalia upya kada ya uzazi ambayo alieleza vyuoni inafundishwa kwa kiwango kidogo sana, hivyo aliziomba mamlaka husika kuona haja ya kuongezewa muda ili kuepusha changamoto zinazowakabili mama wajawazito kwa uchache wa wataalamu.

Pia, Katibu huyo aliiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuangalia uwezekano wa wazee kuwekwa kwenye mfumo mpya wa afya ambao utawatambua rasmi wazee, wanawake na watoto ili kuwaepushia kuwakosesha haki zao za msingi ambapo walilaumu kwamba kuna baadhi ya mifumo ya afya haiwatambui wazee hao.

Hata hivyo, wazee hao walimshukuru Rais Dkt.Mwinyi kwa uamuzi wake wa kuwaongezea pensheni na pensheni jamii kutoka kima cha chini hadi asilimia 100 na 150 kwa pensheni jamii na wastaafu.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Wazee na Wastaafu, Zanzibar (JUWAZA) ilianzishwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na mwaka 2016 ilianzishwa pensheni jamii. Wazee wote tangu mwaka 1960 ni 57,000 na wazee wa pensheni ni 28,000 kwa mujibu wa jumuiya hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news