Rais Dkt.Mwinyi: Serikali itaendelea kuboresha mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inajitahidi kuboresha mazingira wezeshi kwa watu wenye ulemavu kwenye sekta zote za jamii zikiwemo usafiri wa umma, elimu na afya kwa kuzingatia na kurahisisha mahitaji yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na ujumbe kutoka Shirika la Kimataifa la Christian Blind Mission (CBM) waliofika kumtembelea.

Ameeleza kufurahishwa kwake na ushirikiano uliopo baina ya Serikali na shirika hilo kupitia Wizara ya Afya Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesema, Serikali ikiwa kwenye mchakato wa kutoa huduma za Bima ya afya kwa wananchi wa Unguja na Pemba, kipaumbele zaidi kimezingatiwa kwa watu wenye ulemavu  Zanzibar.

Akizungumzia sera ya watu wenye ulemavu ya Zanzibar, Rais Dkt. Mwinyi alieleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza sera hiyo kwa vitendo kwa kuzingatia matakwa na mahitaji ya jamii hiyo hata kwenye majengo yote ya umma inaweka mkazo zaidi kwa mahitaji yao ikiwemo kuboresha miundombinu ya majengo na ofisi za Serikali kufikiwa na watu wajamii zote ikiwemo huduma za ngazi na vyoo kuwa na mazingira rafiki kwa watu wote.

Alisema Serikali kwa kuzingatia mpango mpya wa huduma ya usafiri wa Umma imeadhimia kuboresha huduma hiyo kwa jamii, kwa kuwazingatia watu wenyeulemavu na kuangalia uwezekano wa kuwafikia kwa huduma wezeshi huku akieleza wadau zaidi wanahitajika kuunga mkono kwenye sekta ya afya kwa watu wenyeulemavu.

Aidha, aliiomba taasisi ya CBM, kuangalia uwezekano wa kuungamkono suala la ujenzi wa makaazi kwa ajili ya watu wenyeulemavu, kwani Serikali ina nia ya kuboresha huduma hiyo, pamoja na kuwakaribisha wadau wengine wa maendeleo kuunga mkono huduma hiyo kwa Serikali.

Nesia Satoki Mahenge, Mkurugenzi Mkaazi wa CBM amesema, wanashirikana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia hospitali ya Mnazi Mmoja ambapo wametoa kiasi cha shilingi bilioni moja kwaajili ya kutekeleza mradi wa matibabu kwa watu wenyeulemavu. 

Naye, Mkurugenzi Maendeleo Jumuishi CBM, Dominique Schlupkothen alimueleza Dkt. Mwinyi kwamba taasisi hiyo inafanyakazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali, taasisi binafsi pamoja na wadau wengine wa maendeleo, mbali na kujikita kwenye kutoa huduma za afya ya macho pia wamejikita na miradi inayoshughulikia maradhi yasiyopewa kipaumbele duniani yakiwemo mabusha, minyoo na maradhi mengine.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news