Rais wa Mahakama ya Afrika aishukuru Tanzania

NA MWANDISHI WETU

RAIS wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud kutoka Tanzania ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa misaada inayoipatia mahakama hiyo ikiwemo ujenzi wa jengo la ofisi ambapo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilikabidhi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi CRJE jijini Arusha tarehe 02 Juni 2023.
Jaji Aboud ametoa shukrani hizo wakati wa kikao na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena L. Tax (Mb) kilichofanyika jijini Dodoma Juni 15, 2023.

Rais wa Mahakama ya Afrika na watumishi wengine, wakiwemo Makamu wa Rais; Majaji na Msajili wapo jijini Dodoma kwa ajili ya kikao (retreat) cha kutathmini utekelezaji wa majukumu ya Mahakama hiyo ili kubaini mafanikio na changamoto kwa ajili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Kwa kutumia fursa ya kikao kufanyika Dodoma, Rais na ujumbe wake wametumia nafasi hiyo kukutana na wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) ili kajadili utekelezaji wa majukumu ya chombo hicho muhimu barani Afrika.
Kwa upande wake, Mhe. Waziri Dkt. Tax alieleza kufurahishwa na uamuzi wa Mahakama hiyo wa kufanya kikao chao jijini Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi. Aidha, aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano unaohitajika ili mahakama hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa jengo la ofisi.

Mhe. Waziri Dkt. Tax alihitimisha mazungumzo yake kwa kumpongeza Jaji Aboud kwa kuchaguliwa tena kwa kipindi cha awamu ya pili na cha mwisho cha miaka miwili kuwa Rais wa Mahakama hiyo. Jaji Aboud alichaguliwa wakati wa ufunguzi wa Baraza la 69 la Pan-Afrika lililofanyika Arusha tarehe 12 Juni 2023.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news