TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-24: SINGIDA, ALIZETI NA FURSA ZAIDI

NA LWAGA MWAMBANDE

MKOA wa Singida upo katikati ya Tanzania Bara. Mji wake Mkuu ni Singida na ni njia panda muhimu kwa usafiri wa barabara kwenda Kaskazini, Magharibi, Kusini na Mashariki.

Singida unapakana na Mkoa wa Manyara kwa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Dodoma upande wa Mashariki, mikoa ya Mbeya na Iringa upande wa Kusini na Mikoa ya Tabora na Simiyu upande wa Magharibi.

Historia inaonesha kuwa, Mkoa wa Singida ulianzishwa rasmi Oktoba 15, 1963 ambapo kabla ya hapo ulikuwa ni Wilaya ya Jimbo la Kati (Central Province) uliojumuisha Mkoa wa Dodoma.

Mkoa wa Singida uko katikati ya Tanzania, kati ya Longitudo 33027’5’’ na 35026’0’’ mashariki ya Greenwich, na kati ya latitudo 3052’ na 7034’ Kusini mwa Ikweta.

Mkoani Singida ndipo kuna eneo eneo rasmi ambalo lilibainishwa na vipimo vya kitaalamu vyenye namba 9305404.35, 698978.015 kuwa ni katikati mwa Tanzania Bara yaani Central point of Tanganyika, ambapo ni katika kitongoji cha Darajani, Kijiji cha Chisingisa kilichopo Kata ya Sasilo Tarafa ya Nkonk’o wilaya ya Manyoni.

Singida una wilaya tano ambazo ni Singida, Iramba, Manyoni, Mkalama na Ikungi; zenye halmashauri saba za Singida, Singida Manispaa, Iramba, Manyoni, Mkalama, Ikungi na Itigi.

Ukubwa wa eneo la Mkoa wa Singida ni kilomita za mraba 49,341 sawa na asilimia 6 ya eneo la Tanzania Bara ambapo kati ya hizo kilomita za mraba 11,340 zinafaa kwa kilimo sawa na asilimia 23 ya eneo lote la mkoa.

Kwa upande wa hali ya hewa ,Mkoa wa Singida hupata mvua kwa kipindi kimoja cha mwaka (mwezi Novemba hadi Aprili) kwa wastani wa milimita 500-800 kwa mwaka na wastani wa hali ya hewa ni nyuzi joto 15-30 kutegemea msimu na mwinuko wa ardhi.

Aidha, kutokana na hali ya hewa, Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa iliyopo kwenye ukanda wa unaopata mvua kidogo.

Kwa miaka ya karibuni wastani wa mvua umekuwa ukipungua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kote duniani.

Shughuli za kiuchumi mkoani Singida ni pamoja na kilimo ambacho huajiri wastani wa asilimia 86 ya wakazi wote. Mazao ya kipaumbele kwa upande wa chakula ni uwele, mtama, mihogo na viazi vitamu na kwa upande wa mazao ya biashara ni alizeti, vitunguu, pamba na ufuta. Pia,shughuli nyingine za uzalishaji mali ni ufugaji, uchimbaji mdogo wa madini, viwanda vidogo na biashara.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, ukifika mkoani Singida utabaini fursa nyingi za kiuchumi. Endelea;


1.Singida nikichangia,
Mwishoni sitafikia,
Moyoni yaniingia,
Hata sijui kwa nini.

2.Huko tunajipatia,
Mafuta ya kupikia,
Huko kama wapitia,
Mwenyewe utabaini.

3.Alizeti nakwambia,
Ya kwetu ya asilia,
Wenyewe wajilimia,
Tunapikia jikoni.

4.Ningependa kuchangia,
Jema tukiwafanyia,
Tule vyetu Tanzania,
Siyo vya ughaibuni.

5.Mafuta ya kupikia,
Ya kwetu tukitumia,
Watu hawatasinzia,
Wakiingia kondeni.

6.Mafuta kuagizia,
Wakulima wafifia,
Bei wanazouzia,
Si ubora kwetu jamani.

7.Uwele, mtama pia,
Singida watulimia,
Kuku watusambazia,
Morogoro hadi Pwani.

8. Karibu tutasikia,
Umeme wakichangia,
Wanatuhakikishia,
Usambae hadi Pwani.

9.Ni wa upepo sikia,
Hiyo kawi tatumia,
Ni utajiri sikia,
Wapatikana nchini.

10.Madini ni mengi pia,
Singida ninakwambia,
Watu wanajichimbia,
Fedha zenda kibindoni.

11.Dhahabu shaba sikia,
Huko meingundulia,
Utajiri Tanzania,
Kaujaza Maanani.

12.Wapi utanitajia,
Hapa kwetu Tanzania,
Bila kunihesabia,
Utajiri wa madini?

13.Ndiyo yetu Tanzania,
Hilo tunafurahia,
Maendeleo sawia,
Yatuletea madini.

14.Tundu Lissu mesikia,
Maarufu nakwambia,
Singida alianzia,
Kuja hapa duniani.

15.Msomi mwanasheria,
Nchi ametumikia,
Visa alivyopitia,
Ni vya ajabu jamani.

16.Mwanasiasa sikia,
Bungeni aliingia,
Hoja alivyochangia,
Ziliingia kichwani.

17.Kidogo nasimulia,
Yale aliyopitia,
Yale hapa Tanzania,
Vichwa vilikuwa chini.

18.Nyumbani akiingia,
Watu walimvamia,
Risasi zikaingia,
Ni nyingi sana mwilini.

19.Lengo aweze jifia,
Tusiweze msikia,
Kile aliwafanyia,
Siri yao mioyoni.

20.Kumi na sita sikia,
Risasi ziliingia,
Zingine zimebakia,
Bado yupo duniani.

21.Ni muujiza sikia,
Twashangaa Tanzania,
Wale walimfanyia,
Ni bado tuko gizani.

22.Fundisho linaingia,
Fitina si nzuri pia,
Hii ya Mungu dunia,
Uhai tuuthamini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news