TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-26:TABORA,NI KITOVU CHA HISTORIA

NA LWAGA MWAMBANDE

MKOA wa Tabora ni miongoni mwa mikoa 31 ya Tanzania. Mji mkuu wa mkoa ni Manispaa ya Tabora ambapo unapatikana katikati ya Magharibi mwa Tanzania.

Tabora umepakana na Shinyanga kwa upande wa Kaskazini, Singida kwa upande wa Mashariki, Mbeya na Songwe kwa upande wa Kusini, Katavi, Kigoma na Geita inapakana na Tabora kwa upande wa Magharibi.

Muonekano wa barabara ya Tabora-Sikonge-Mpanda kwenye mzunguko daraja la Mto Koga ambalo lilikuwa kikwazo kikubwa cha uchumi wa wakazi wa mikoa hiyo miwili ya Tabora na Katavi, barabara hiyo tayari imeanza kuwanufaisha wakazi wa mikoa hiyo miwili baada ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Aidha, Tabora ndio mkoa mkubwa zaidi nchini Tanzania kwa eneo. Idadi kubwa ya wakazi wa mkoa huo wamejikita Kaskazini mwa Wilaya ya Nzega. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anakupitisha kwa kina katika Mkoa wa Tabora. Endelea;


1. Tabora nakumbushia,
TANU lipokutania,
Hamsina nane nia,
Kuondoa ukoloni.

2. Watemi walitimia,
Uhuru kupigania,
TANU wakaitumia,
Mikakati ya mezani.

3. Hili nililoanzia,
Tabora nafagilia,
Uhuru kupigania,
Walifanya bila soni.

4. Mkoa twausifia,
Vile walivyotulia,
Ndiyo mana tasikia,
Huko ni Unyamwezini.

5. Kwa biashara huria,
Tunawaenzi tangia,
Japo waliwatumia,
Kwa visivyo nikidhani.

6. Utumwa ulivamia,
Na wengi wakaishia,
Vile ninafikiria,
Waliteseka jamani.

7. Kwa uchumi wawania,
Kuongoza Tanzania,
Tumbaku wajilimia,
Mauzo hadi Japani.

8. Karanga watuuzia,
Kwa chakula twatumia,
Asali ninasikia,
Ni baba lao nchini.

9. Tabora mwatutambia,
Visura mwajijazia,
Sasa tunawajulia,
Twaingia harusini.

10. Nyerere Mtanzania,
Tabora alifikia,
Shule akajifunzia,
Kisha Makerere ndani.

11.Nenda Tabora tulia,
Huwezi ukakimbia,
Mambo watakufanyia,
Yataingia moyoni.

12. Chifu Mirambo sikia,
Uhuru lipigania,
Wengi walimsifia,
Kamanda alo makini.

13. Ni Mtemi nakwambia,
Yumo kwa historia,
Waliotupigania,
Kulinda hadhi nchini.

14. Tabora nakuambia,
Maarufu Tanzania,
Watu imetupikia,
Maarufu duniani.

15. Mmoja nasimulia,
Huyu ni Mtanzania,
Jina lake nakwambia,
Lajulikana barani.

16. Historia pitia,
Ukombozi nakwambia,
Uhuru kupigania,
Waliingia vitani.

17. Yule alisimamia,
Kibali akitumia,
Alitoka Tanzania,
Tabora ndiko nyumbani.

18. Hashim Mbita sikia,
Mjeshi alotimia,
Mwanadiplomasia,
Na mwingine hafanani.

19. Nchi alitumikia,
Kadha nyingi kutajia,
Kubwa twamkumbukia,
Ni ukombozi kusini.

20. OAU kumbukia,
Ilipojiamulia,
Kamati kujiundia,
Ya ukombozi barani.

21. Mbita lijichagulia,
Aweze kutangulia,
Nchi kuzipigania,
Kusiwepo ukoloni.

22. Kazi alitufanyia,
Ni sifa kwa Tanzania,
Uhuru ukaingia,
Kote Afrika barani.

23. Magumu alipitia,
Kamati kishikilia,
Misaada kupatia,
Kuupinga ukoloni.

24. Vita baridi dunia,
Livyojigawanyikia,
China na Urusi pia,
Kugawanyika vitani.

25. Vikundi kusaidia,
Tofauti nakwambia,
Ni kwa diplomasia,
Kufika vema mwishoni.

26. Jenerali Brigedia,
Kwa kweli alitimia,
Kazi alitufanyia,
Ni maarufu nchini.

27. Msumbiji kumbukia,
Angola nakutajia,
Na Guine Bissau pia,
Alishiriki kazini.

28. Hata Carpe Verde pia,
Uhuru mtawalia,
Kote alipigania,
Yasibaki makoloni.

29. Huyu baba nakwambia,
Alivyotumbania,
Hata na Zimbabwe pia,
Uhuru kamili ndani.

30. Meshajipumzikia,
Umri lipotimia,
Shujaa wa Tanzania,
Amebaki vitabuni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news