TAZAMA ANGA LA MWANZA, NITARUDI TENA MWANZA

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mji wa Mwanza ulianzishwa mwaka 1892 kama Kituo cha Utawala na Kituo cha Biashara ili kudhibiti uzalishaji hasa wa maeneo ya pamba katika eneo la Ziwa Victoria.

Picha na MITU.

Mwaka 1978 Mwanza ilipata hadhi ya Manispaa kulingana na muundo wa Serikali za Mitaa ulioanzishwa mwaka 1972. 
 
Mwaka 2000, Mwanza iliendelezwa zaidi kuwa na hadhi ya Jiji. Majiji mengine mbali na Mwanza kwa Tanzania Bara ni Dar es Salaam,Dodoma,Arusha,Tanga, Mbeya na Jiji la Zanzibar kwa upande wa Tanzania Visiwani.

Aidha, mbali na hayo, Mji wa Mwanza upo katika mwambao wa Kusini mwa Ziwa Victoria Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Jiji la Mwanza ni la pili kwa ukubwa nchini Tanzania baada ya jiji la Dar es Salaam, na kituo kikuu cha biashara kwa mikoa inayozunguka Ziwa Victoria na nchi jirani za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda. Jiji limezungukwa na vilima vya mawe vilivyo na mawe makubwa ya kuvutia.

Pia, jiji hilo lina joto kati ya 25.7OC na 30.2OC katika msimu wa joto na 15.4oC na 18.6OC katika miezi ya baridi huku mvua kwa mwaka ikiwa ni kati ya 700 na 1000mm. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, ukiwa jijini Mwanza hautajutia kukaa huko kamwe. Endelea.

1.Tazama anga la Mwanza, la Ziwa Victoria,
Asubuhi unaanza, mawimbi yanakwambia,
Siku ndiyo inaanza, nawe sasa karibia,
Mwanza nitarudi Mwanza, niweze ifurahia.

2.Tamaa kweli yaponza, ni supu ya Tilapia,
Asubuhi ukianza, lazima kumalizia,
Ladha yake yakufunza, utajiri Tanzania,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

3.Hao dagaa wa Mwanza, ni samaki nakwambia,
Mwili wanavyoutunza, afya yazidi ingia,
Hamu yaweza kuponza, ule kupitilizia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

4.Kumbukumbu njema Mwanza, miaka ilotimia,
Kuna kwaya kule Mwanza, kweli tulishangilia,
Na kwao tulijifunza, Mungu kumtumikia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

5.Town Kwaya ya Mwanza, nani hakuisikia,
Kwaya zilipamba Mwanza, kwa kurudiarudia,
Nyimbo wakiimba Mwanza, kiroho zilijazia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

6.Usiku wa manane anza, wimbo kujishushia,
Ni Makongoro ya Mwanza, ndiyo walitupatia,
Sauti kwenye stanza, na vyombo vilijazia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

7.Ninakumbukia Mwanza, soka nitawasifia,
Naisema ile Mwanza, walitamba Tanzania,
Nini kilichowaponza, kiasi wamefifia?
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

8.TP Lindanda ya Mwanza, timu ninakutajia,
Ilivyochomoza Mwanza, makubwa kutufanyia,
Ubingwa kuenda Mwanza, wengi wakiangalia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

9.Timu ya Pamba ya Mwanza, ndiyo ninakutajia,
Soka ilivyotufunza, kileleni kufikia,
Nini kilichowaponza, sasa wanainukia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

10.Umekosa nini Mwanza, Mungu asokujalia,
Ukarimu uko Mwanza, watu ukiwafikia,
Uwazi mvuto Mwanza, lao watakuambia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

11.Ndiyo jiji kubwa Mwanza, kanda hiyo nakwambia,
Wengine ndiyo waanza, wazidi kuinukia,
Hawatafikia Mwanza, ngazi inajipandia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

12.Ukerewe nako Mwanza, huko tumeshazamia,
Wenyewe wanatutunza, maisha twafurahia,
Kama hujapita anza, nawe utafurahia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

13.Pamba inalimwa Mwanza, fedha inatupatia,
Viwanda ni vingi Mwanza, uchumi vinachangia,
Madini yachimbwa Mwanza, na kuchenjuliwa pia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

14.Jiji lapendeza Mwanza, barabara zavutia,
Na ilivyokaa Mwanza, makubwa twasubiria,
Kanda Mashariki Mwanza, rahisi kupafikia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

15.Toka Kenya kuja Mwanza, rahisi kupafikia,
Uganda kufika Mwanza, marathoni wafikia,
Rwanda Burundi za kwanza, vyote zitajipatia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

16.Hongera wakazi Mwanza, kazi mnajifanyia,
Ndivyo mwaikuza Mwanza, kuijenga Tanzania,
Mtafika mbali Mwanza, tuzidi washangilia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

17.Saanane iko Mwanza, rahisi kuifikia,
Nenda katalii Mwanza, mawe kuyashangilia,
Srengeti toka Mwanza, si mbali nakuambia,
Mwanza nitarudi Mwanza, nizidi ifurahia.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news