TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-22: NI MKOANI SHINYANGA, KARIBUNI

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Shinyanga ulikuwa ni sehemu ya Mkoa wa Ziwa (Lake Province) mpaka mwaka 1963 ulipoanzishwa rasmi ukiwa na wilaya tatu. Wilaya hizo zilikuwa ni Maswa, Shinyanga na Kahama iliyomegwa kutoka Mkoa wa Tabora.

Aidha, kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 1982 Serikali ya mkoa ilikuwa katika mfumo wa madaraka mikoani ambapo vyama vya ushirika, utemi na Serikali za mitaa zilifutwa.

Mkoa uliongozwa na mkuu wa mkoa, akifuatiwa na Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa (Regional Development Director) ambaye alisimamia wakuu wa idara mbalimbali.

Muundo huo wa utawala ulitumika hadi mwaka 1997 ambapo ulibadilishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tawala za Mikoa (Regional Administration Act No. 19 of 1997).

Sheria hiyo ilifuta cheo cha Mkurugenzi wa Maendeleo wa Mkoa na kuanzisha cheo cha Katibu Tawala Mkoa. Katibu Tawala Mkoa ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za Serikali katika mkoa.

Mkoa wa Shinyanga uliendelea kukua ambapo maeneo mapya ya utawala yalianzishwa na kufikia wilaya saba ambazo ni Kahama, Bukombe, Maswa, Kishapu, Bariadi, Meatu na Shinyanga.

Kuanzia mwaka 2012 kutokana na mkoa kukidhi vigezo muhimu vya kitaifa vya uanzishaji maeneo mapya ya utawala, Serikali ilifanya uamuzi wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala ambapo mikoa mipya ya Simiyu na Geita ilianzishwa ikiwa imemega baadhi ya wilaya za Mkoa wa Shinyanga.

Wilaya za Bariadi, Maswa na Meatu zilimegwa kuanzisha Mkoa wa Simiyu na Wilaya ya Bukombe ilipelekwa Mkoa mpya wa Geita.

Mkoa wa Shinyanga uliongeza maeneo ya kiutawala kwa kuanzisha halmashauri mpya za Kahama mji mwaka 2012, Msalala na Ushetu mwaka 2013 ambazo zilitokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Kahama.

Uamuzi huo wa Serikali ulilenga kuboresha huduma za kiutawala na maendeleo ili wananchi waweze kuzipata kwa karibu zaidi.

Mkoa wa Shinyanga uko Kaskazini Magharibi mwa Tanzania na Kusini mwa Ziwa Victoria. Mkoa unapakana na Mikoa ya Mwanza, Simiyu na Geita kwa upande wa Kaskazini, upande wa Mashariki Mkoa wa Simiyu.

Upande wa Magharibi Mkoa wa Geita upande wa Kusini Mkoa wa Tabora. Mkoa uko kati ya nyuzi za Latitudo 30 12’ - 40 27’ Kusini mwa Ikweta na nyuzi za Longitudo 310 29’ - 340 18’ Mashariki ya Greenwich.

Mkoa wa Shinyanga una eneo la kilometa za mraba 18,555. Leo, katika mwendelezo huu wa kuifikia mikoa yote nchini, mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema ni zamu ya Mkoa wa Shinyanga kupitia ushairi huu. Endelea;

1. Shinyanga nakutajia,
Mkoa umetulia,
Utajiri wanukia,
Kwa kilimo na madini.

2. Huko Wasukuma pia,
Uchumi wanachangia,
Mengi wanatufanyia,
Maendeleo nchini.

3. Madini ninaanzia,
Yale wanatupatia,
Kama kutajirikia,
Huko ninapatamani.

4. Almasi wasikia,
Ya vioo kukatia,
Mwadui inatambia,
Yasikika duniani.

5. Japo wanatuchimbia,
Kazi tunajipatia,
Fedha tunajikimia,
Maisha bora nchini.

6. Mungu tunashangilia,
Vile ametujalia,
Mengi ametupatia,
Neema zimesheheni.

7. Dhahabu twajichimbia,
Kwingi kwingi Tanzania,
Buzwagi nataja pia,
Twaivuna kama nini.

8. Fedha tunajipatia,
Za kigeni nakwambia,
Hakika zasaidia,
Maendeleo nchini.

9. Shinyanga mpunga pia,
Mchele watupatia,
Malori yanapakia,
Asubuhi na jioni.

10. Pamba nitakutajia,
Na tumbaku wachangia,
Hawa nikiwakamia,
Yani hawawezekani.

11.Mifugo mia kwa mia,
Shinyanga imejazia,
Nyama tunazojilia,
Watuletea mijini.

12. Watu ukiangalia,
Kazi wanajifanyia,
Lengo lao kufikia,
Juu wala siyo chini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news