ZANZIBAR NI TANZANIA-32: VIONGOZI WAKUU ZANZIBAR

NA LWAGA MWAMBANDE

ZANZIBAR ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na visiwa vidogo vidogo vilivyoizunguka na bahari yake ambayo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iliitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Kwa ujumla visiwa hivyo vipo baina ya Latitude na Digrii 6 Kusini mwa mstari wa Ikweta na Longitudi 39.55 na Digrii 40 Mashariki, Zainzibar ni miongoni mwa nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Zanzibar ina miongo minne ya majira ya hali ya hewa katika mwaka wa Kalenda inayoanzia mwezi wa Januari hadi Disemba ambayo inahusisha majira ya Kaskazi (Disemba hadi Febuari), Masika (Machi hadi Mei), Kipupwe (Juni hadi Septemba) na Vuli (Oktoba hadi Novemba). 
Awamu ya Kwanza ya Uongozi wa Kitaifa Zanzibar ilikuwa chini ya Chama cha Afro-Shirazi kilichoongozwa na marehemu Mzee Abeid Amani Karume ambaye alikuwa ni Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Ni kati ya Januari 12, 1964 hadi Aprili 7, 1972. Awamu hii inatajwa kuwa muhimu sana katika historia ya nchi ya Zanzibar. 

Kwani, ndiyo awamu iliyoweka dira ya mwelekeo wa Zanzibar katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ili kufikia malengo yaliyowekwa na Chama cha Afro Shirazi Party (ASP). 

Ni dhahiri kwamba awamu hii ililazimika kuchukua hatua madhubuti na kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha kuwa lengo la Mapinduzi linafikiwa na kuwanufaisha Wazanzibari wote. 

Uongozi ulifuata misingi ya kuongozi kwa kuonesha njia ambapo viongozi wa Serikali walikuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa kila shughuli ya maendeleo iliyofanywa na wananchi. 

Hiki ni kipindi ambacho dhana ya kujitolea katika ujenzi wa Taifa ilikuwa ndio dira ya utekelezaji wa shughuli za Serikali. Katika hali hiyo Serikali ya ASP ilianza kutekeleza ahadi zake zilizoorodheshwa katika Manifesto ya ASP. 

Aidha, historia inaonesha kuwa,baada ya kifo cha Mzee Abeid Amani Karume mwaka 1972, Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alipendekezwa na hatimaye kuthibitishwa na Baraza la Mapinduzi (BLM) katika kikao kilichofanyika Aprili 11, 1972 Makao Makuu ya Afro Shirazi Party (ASP) Kisiwandui Zanzibar.

Kwa dhamira ya kuimarisha Muungano na kuzingatia mafanikio yaliyopatikana tangu nchi mbili hizi kuungana, vyama vilivyoongoza Zanzibar (ASP) na Tanganyika Association National Unity (TANU) viliunganishwa Februari 5, 1977 na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Kwa mujibu wa mfumo wa kisiasa wa wakati huo, Chama Cha Mapinduzi kilishika hatamu ya kusimamia Dola ya Serikali zote mbili. Awamu hii itakumbukwa zaidi kwa kuasisi na kuimarisha misingi ya demokrasia na utawala chini ya mfumo wa chama kimoja.

Baada ya kujiuzulu Rais wa Awamu ya Pili, kiongozi aliyeteuliwa kushika nafasi ya Urais wa Zanzibar ni Mzee Ali Hassan Mwinyi. 

Nafasi ambayo alidumu nayo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu (Januari 31, 1984 hadi Oktoba 17,1985) kabla ya kuteuliwa na kuchaguliwa kushika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Rais Ali Hassan Mwinyi alimteua Mheshimiwa Seif Sharif Hamad kushika nafasi ya Waziri Kiongozi ambaye, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, alikuwa ni msaidizi wa Rais na Mkuu wa shughuli za Serikali katika Baraza la Wawakilishi.

Halmashauri Kuu ya CCM ilipitisha jina la Mheshimiwa Idris Abdulwakil kwa ajili ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 13, 1985. 

Mzee Idris Abdulwakil (17 Oktoba 1985 - 25 Oktoba, 1990) naye aliendeleza mfumo ule ule wa Serikali wenye kuzingatia mihimili mitatu ya Dola ambapo pia alimteua Mhe. Seif Sharif Hamad kuendelea na wadhifa wa Waziri Kiongozi. 

Hata hivyo, katika kuimarisha utendaji wa Serikali, tarehe 26 Januari 1988, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alilivunja Baraza la Mapinduzi na baadae kumteua Mheshimiwa Dkt.Omar Ali Juma kushika nafasi ya Waziri Kiongozi badala ya Mhe. Seif Sharif Hamad. Uongozi wa Mheshimiwa Idris Abdulwakil ulimalizika baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka 1990.

Wakati huo huo, Oktoba 25, 1990 hadi Novemba 8, 2000 Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Tano iliongozwa na Dkt. Salmin Amour Juma na ilifuata mfumo wa uongozi sawa na wa awamu zilizotangulia. 

Hata hivyo, Awamu hii ilikuwa na mabadiliko makubwa katika safu za siasa na uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Awamu ya tano ilikuwa ni ya vipindi viwili kisiasa. Kipindi cha kwanza cha uongozi kilianza mwaka 1990 hadi 1995 na muendelezo wa mfumo wa utawala wa chama kimoja cha siasa hadi mwaka 1992 ambapo mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa tena. 

Katika uongozi wa miaka 10 wa Rais Dkt. Salmin Amour Juma, Serikali ilitilia mkazo kuimarisha uchumi na mawasiliano ya kisiasa.

Katika kipindi cha kwanza cha uongozi Dkt.Omar Ali Juma aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi na katika kipindi cha pili alimteuwa Dkt.Mohamed Gharib Bilali kuwa Waziri Kiongozi. 

Aidha katika kipindi hicho ilianzishwa nafasi ya Naibu Waziri Kiongozi ambapo Mhe. Omar Ramadhan Mapuri aliteuliwa kuwa Naibu Waziri Kiongozi. 

Kipindi hicho cha uongozi baada ya Uchaguzi Mkuu chini ya mfumo wa vyama vingi kilikuwa kigumu kutokana na kususiwa misaada na wafadhili wa nje, hasa kutoka nchi za Magharibi kutokana na sababu za kisiasa.

Novemba 8, 2000 hadi Novemba 3, 2010, Serikali ya Awamu ya Sita iliongozwa na Mhe.Dkt. Amani Abeid Karume baada ya kuchaguliwa na wananchi wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2000 na 2005. 

Awamu ya Sita ya uongozi ilikuwa na vipindi viwili (2000-2005) na (2005-2010). Kama awamu zilizopita Serikali ya awamu hiyo iliendelea kulinda na kuendeleza misingi iliyowekwa. 

Katika vipindi vyote hivyo Mhe.Dkt.Amani Abeid Karume alimteuwa Mhe.Shamsi Vuai Nahodha kuwa Waziri Kiongozi. Na katika kipindi cha pili alimteuwa Mhe.Ali Juma Shamuhuna kuwa Naibu Waziri Kiongozi.

Mabadiliko hayo ya Katiba yalitokana na maamuzi ya viongozi wa vyama vya siasa (Mhe.Dkt.Amani Abeid Karume ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar na Mhe.Seif Sharif Hamad ambaye ni Katibu Mkuu Civil United Front (CUF) Taifa ya kukubali kuanzisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. 

Maamuzi ya viongozi hao yaliungwa mkono na wananchi wa Zanzibar katika kura ya maoni iliyopigwa Julai 31, 2010. Uongozi wa Dkt. Amani Abeid Karume ulimazika baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Pia, Novemba 3, 2010 hadi Novemba 3, 2020 katika Awamu ya Saba ya Urais wa Zanzibar chini ya Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulibadilika kutoka mfumo wa Serikali inayoongozwa na chama kilichoshinda peke yake kwenda katika mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambapo chama kilichoshinda kinashirikiana na chama kilichoshika nafasi ya pili katika kuunda Serikali.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaongozwa na Rais ambaye anasaidiwa na Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais na kufuta nafasi ya Waziri Kiongozi iliyokuwepo kabla ya marekebisho hayo ya Katiba. 

Kwa mujibu wa marekebisho hayo, Rais anatoka chama kilichoongoza katika Uchaguzi Mkuu, Makamu wa Kwanza wa Rais anateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichoshinda nafasi ya pili katika matokeo ya uchaguzi wa Rais na Makamu wa Pili wa Rais anateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka chama anachotoka Rais na ndiye atakayekuwa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali. 

Marekebisho hayo pia yamemuweka Katibu wa Baraza la Mapinduzi kuwa ni Katibu Mkuu Kiongozi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Zanzibar.

Aidha, muundo huu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye Mfumo wa Umoja wa Kitaifa umeendelea kuendesha shughuli zake kupitia Baraza la Wawakilishi ambacho ndicho chombo kikuu cha kutunga Sheria Zanzibar, Baraza la Mapinduzi pamoja na Mahakama. 

Mihimili yoye mitatu inafanya kazi kwa uhuru na kujitegemea. Serikali ya Umoja wa Kitaifa inaendelea kulinda na kutetea malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka1964 kwa kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar kuwa kitu kimoja na kusahau tafauti zao za kisiasa.

Novemba 3, 2020 mpaka sasa,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane ambayo iliingia madarakani Oktoba 2020 inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi.

Serikali kupitia uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi imedhamiria kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasimali zake ili kujenga uchumi imara kwa kufanya mapinduzi ya kiuchumi kwa kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuweka mkazo katika kuziimarisha sekta za huduma ikiwemo sekta ya utalii ambayo ni Muhimili Mkuu wa Uchumi wa Zanzibar.

Vipaumbele zaidi ni kuimarisha sekta mbalimbali za maendeleo na kukuza uchumi wa nchi kwa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali,kuwa na ubunifu katika kutekeleza majukumu ya taasisi za Serikali.

Pia,kuimarisha utawala bora kwa kupiga vita rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma,kuwa na utamaduni wa kuwasikiliza wananchi,uwajibikaji,kuondoa urasimu na usumbufu katika kutoa huduma kwa wananchi. 

Kusimamia masalahi ya watumishi wa umma, kutoa taarifa kwa jamii kuhusu shughuli zinazotekelezwa na taasisi za Serikali ikiwemo kuimarisha usafi wa mazingira katika miji na vijiji pamoja na majengo ya tasisi za umma. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, mara zote Muungano wetu tunauthamini. Endelea;

1.Zanzibar ni Tanzania,
Ninakuthibitishia,
Mengi twajifaidia,
Muungano twathamini.

2.Muungano kisikia,
Udongo walichangia,
Nyerere alipania,
Karume akasaini.

3.Baba Karume sikia,
Makubwa litufanyia,
Hivi tunavyotambia,
Ni kwa wake umakini.

4.Baba alifikiria,
Bila hata kukawia,
Umoja kiaminia,
Nchi iwe na amani.

5.Mapinduzi twasifia,
Aliongoza sawia,
Uhuru kujipatia,
Kutoka kwa Sultani.

6.Myezi hakusubiria,
Urais kutambia,
Muafaka kafikia,
Muungano wa amani.

7.Alofanya yabakia,
Milele twasimulia,
Taifa katuundia,
Tanzania yashaini.

8.Unguja ukifikia,
Mitaa kuzungukia,
Majumba katuachia,
Ni alama duniani.

9.Ni mfano nawambia,
Nyumba wajimilikia,
Ni hawa hawa raia,
Kazione Michenzani.

10.Alichopandikizia,
Watu kujiaminia,
Wazenji kiwafikia,
Yataingia moyoni.

11.Zenj imewaingia,
Hiyo waiaminia,
Mapinduzi kisikia,
Wayaenzi maishani.

12.Kamwe hawataachia,
Bwanyenye akaingia,
Hilo wameshikilia,
Kwao ni kama imani.

13.Zanzibar ni Tanzania,
Marais kutajia,
Na wasaidizi pia,
Karume yu kileleni.

14.Vibaya aliishia,
Risasi mmiminia,
Lakini amesalia,
Muasisi Visiwani.

15.Abdul Jumbe sikia,
Urais lishikia,
Ni wa pili nakwambia,
Zanzibar madarakani.

16.Pia alishikilia,
Umakamu Tanzania,
Hadi alipoishia,
Hali ya hewa nchini.

17.Jumbe naye liichangia,
Zanzibar kutumikia,
Uchumi tuinulia,
Kwa ubora maishani.

18. Mengi alitufanyia,
Yale aliyowazia,
Japo lijitibulia,
Nakuishia njiani.

19.Siasa ziliingia,
Hewa katuchafulia,
Kitini hakusalia,
Kaishia Kigamboni.

20.Undani kiutakia,
Yale yaliyotukia,
Vitabu tajipatia,
Yaingie akilini.

21.Pale alipoishia,
Mji Mwema jikalia,
Ali Mwinyi kaingia,
Urais Visiwani.

22.Huyu twamkumbukia,
Muda alitumikia,
Mwaka moja nakwambia,
Akapaa kileleni.

23.Alipojing’atukia,
Nyerere wa Tanzania,
Ni Mwinyi aliingia,
Muungano kileleni.

24.Muungano takwambia,
Mwinyi alotufanyia,
Vile alivyosalia,
Miaka kumi nchini.

25.Lipokuja Tanzania,
Rais kushikilia,
Wakil akaingia,
Rais wa Visiwani.

26.Baba alitumikia,
Mitano akaishia,
Huo mwaka nakwambia,
Moja tisa na tisini.

27.Magumu alipitia,
Vyama vingi kuingia,
Nguvu alivyojitia,
Akafikia mwishoni.

28.Vyama vingi kuingia,
Changamoto nakwambia,
Mambo mengi litukia,
Kama vile tu vitani.

29.Kama si kusimamia,
Kwa nguvu ninakwambia,
Yale yangelitukia,
Tungekuwa msambweni.

30.Wakil kumalizia,
Salmin kaingia,
Huyu alijitwalia,
Sifa nyingi Visiwani.

31.Mkali ninakwambia,
Mapinduzi tulindia,
Hadi akajipatia,
Lile jina la vitani.

32.Komandoo lisikia,
Jina lilompatia,
Wale walimsikia,
Wanakumbuka moyoni.

33.Kama ukimbishia,
Yeye alikutishia,
Na usipoangalia,
Ungekuwa msambweni.

34.Komandoo kisikia,
Kiti alishikilia,
Maalim litishia,
Akaishia jelani.

35.Nafasi alitumia,
Wapinzani kupigia,
Vibaya liwafanyia,
Watu huko Visiwani.

36.Wengi liwafungulia,
Kesi kuwamalizia,
Vile liwatuhumia,
Kwa kesi ya uhaini.

37.Kile tunafurahia,
Nchi yetu Tanzania,
Korti lituamulia,
Kesi ikapigwa chini.

38.Kwamba nchi Tanzania,
Jamhuri yasalia,
Hiyo kama wajitia,
Ni kesi ya uhaini.

39.Visiwani kasikia,
Haiwezekani nia,
Kutaka jipindulia,
Kuuita uhaini.

40.Somo lilipoingia,
Wale wakawaachia,
Na nchi ikatulia,
Tukaenda kwa Amani.

41.Dokta twamsifia,
Nchi livyosimamia,
Nguvu asingetumia,
Angelikuwa shidani.

42.Komandoo asalia,
Mbabe kihistoria,
Zanzibar kutumikia,
Akiwa madarakani.

43.Hapa nikikutajia,
Kiongozi tavutia,
Ambaye alichangia,
Akiwa serikalini.

44.Kwanza limsaidia,
Abdul Wakil pia,
Na huko hakusalia,
Kawa Makamu nchini.

45.Ni mwiba ninakwambia,
Vile twamkumbukia,
Komando limshukia,
Sibaki madarakani.

46.Pia alisaidia,
Muungano Tanzania,
Sasa ninakutajia,
Sikiza masikioni.

47.Omar Juma sikia,
Daktari lotimia,
Umakamu Tanzania,
Liongoza kwa makini.

48.Baba alisimamia,
Ofisi twakumbukia,
Mazingira kupitia,
Muungano ushaini.

49.Kwa msimamo sikia,
Alikuwa katimia,
Uwazi alitumia,
Mambo yawe hadharani.

50.Mmoja nakumbukia,
Muda ulipowadia,
Rais kumalizia,
Apishe mtu kitini.

51.Akataka kusalia,
Kiti aking’ang’ania,
Omar limshukia,
Kwa maneno si mwilini.

52.Busara alitumia,
Ujumbe mfikishia,
Ng’atuka ninakwambia,
Bado wapendwa moyoni.

53.Usije ukasalia,
Kiti uking’ang’ania,
Washindwe kuvumilia,
Upigwe mawe mwilini.

54.Komandoo kaishia,
Kiti akaachilia,
Amani Karume njia,
Kufika madarakani.

55.Vyama vingi nakwambia,
Ilikuwa ngumu njia,
Kiti walishindania,
Hasa kule Visiwani.

56.Maalim Seif pia,
Kura alijipatia,
Japo hazikufikia,
Yeye kuwa kileleni.

57.Mengi tuliyasikia,
Lawama zinasalia,
Lile tunashikilia,
Yalowekwa hadharani.

58.Amani livyoingia,
Uchaguzi nakwambia,
Vurugu ziliingia,
Hilo ni doa nchini.

59.Damu kutumwagikia,
Hasa Pemba nakwambia,
Dunia ilisikia,
Hali yetu kawa duni.

60.Busara walitumia,
Viongozi Tanzania,
Umoja ukaingia,
Maalim na Amani.

61.Hapo tulishangilia,
Serikali kutimia,
Zanzibar ya Tanzania,
Ikaingia amani.

62.Rais Amani nia,
Ni umoja kuingia
Wapinzani kuwatia
Wawemo madarakani.

63.Miaka lipotimia,
Kumi hiyo nakwambia,
Karume akaishia,
Anaishi kwa pensheni.

64.Vyama vingi kuingia,
Tisina mbili sikia,
Chaguzi tuzopia,
Ngumu kule Visiwani.

65.Viti kuvipigania,
Si Bara ya Tanzania,
Kwani huko nakwambia,
Ni mkali ushindani.

66.Lakini twakumbukia,
Elfu mbili sikia,
Damu livyomwagikia,
Isirudie nchini.

67.Kisha Sheni kaingia,
Daktari lotimia,
Kofia twamvulia,
Kwa uongozi makini.

68.Mungu alimjalia,
Vile litutumikia,
Mengi alitufanyia,
Kwapendeza Visiwani.

69.Barabara kama mia,
Dokta katupatia,
Kote kote kipitia,
Utafurahi moyoni.

70.Maendeleo sikia,
Mengi tunajivunia,
Uwanja wa ndege pia,
Sasa huo u kazini.

71.Si mdogo nakwambia,
Na Songwe linganishia,
Wa Kimataifa pia,
Na kisasa Visiwani.

72.Vyuo vikuu sikia,
Yeye katupanulia,
Wasomi amechangia,
Kuwaongeza nchini.

73.Watalii kuingia,
Uchumi kasimamia,
Wengi sasa waingia,
Na mapesa ya kigeni.

74.Mazingira kachangia,
Mitaji kuivutia,
Uchumi twafurahia,
Mashambani viwandani.

75.Kama ukimsikia,
Mpole akichangia,
Lile anashikilia,
Madhubuti na makini.

76.Kumi miaka timia,
Kiti kakiachilia,
Mshauri kasalia,
Tanzania Visiwani.

77.Awamu imeingia,
Ya nane imetulia,
Ndio sasa twatambia,
Serikali Visiwani.

78.Hussein Mwinyi sikia,
Kiti amekikalia,
Yake twayafaidia,
Kama tuko kivulini.

79.Wa kisasa nakwambia,
Kazi anatufanyia,
Tunaona kapania,
Zenj itoke gizani.

80.Uchumi Buluu nia,
Kwetu uweze ingia,
Chini tusijesalia,
Kiuchumi duniani.

81.Huyu anakazania,
Uongozi bora pia,
Wazembe anafagia,
Waishie jalalani.

82.Mwinyi kimuangalia,
Ni nyota ya Tanzania,
Zanzibari angalia,
Inakwenda kileleni.

83.Kile kinachovutia,
Nchi ukiangalia,
Umoja umeingia,
Mambo yenda kwa amani.

84.Ndiyo tuu kaingia,
Mwaka haujafikia,
Heri tunamtakia,
Hapo alipo kitini.

85.Kikubwa kukumbukia,
Wazanzibari sikia,
Mapinduzi shikilia,
Ndiyo dira Visiwani.

86.Kamwe msijeachia,
Yakaanza kutitia,
Hadi mje jikutia,
Mmeingia shimoni.

87.Watoto mejipatia,
Bora kuwafwatilia,
Wajue historia,
Iwakae akilini.

88.Yote wakijifanyia,
Maisha kufurahia,
Wabaki kukumbukia,
Asili yao nyumbani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news